Wednesday, September 25, 2013

Uchambuzi kuhusiana na shambulizi la kigaidi nchini Kenya Katika duka la kifahari WestgatE Nairobi


Uchambuzi kuhusiana na shambulizi la kigaidi nchini Kenya Katika duka la kifahari WestgatE Nairobi:



Tukio hilo la kigaidi lilianza mchana wa Jumamosi wakati kikundi cha watu wenye silaha, walioripotiwa wakiwa wa mataifa kadhaa, walipoingia katika jengo hilo, kuweka maguruneti na kufyatua bunduki za automatiki, huku wakiua ovyo raia wasio na hatia na kuwafanya  wanunuzi waliochanganyikiwa kutoroka.

Vikosi vya usalama vya Kenya tangu wakati huo vimewekwa katika hali ya mapambano na wanamgambo hao.

Jeshi la Kenya siku ya Jumatatu lilisema kwamba limeshaokoa sehemu kubwa ya jengo la maduka, huku afisa mmoja wa usalama alisema kwamba uvamizi wa mwisho ulikuwa uko njiani dhidi ya ya wanamgambo wa al-Shabaab, wanaoaminika kuwa wamejificha katika sehemu ya duka hilo lakini wanawatumia mateka kama ngao yao.

Zaid ya watu 1,000 walisalimishwa tangu operesheni hizo zilipoanza.

Makisio yanawaweka watu waliouawa wakati wa mzingiro huo wa siku tatu za umwagaji damu kuwa zaidi ya 60, pamoja na takriban watu 200 kulazwa hospitali kutokana na majeraha ya bunduki na majeraha mengine, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilisema kwamba dazeni kadhaa zaidi waliarifiwa kutoonekana.

Al-Shabaab, ambao wamedai kuhusika na shambulio hilo, walisema kwamba shambulio hilo lilikuwa ni kulipiza kisasi kwa uvamizi wa jeshi la Kenya huko Somalia, ambako majeshi ya Umoja wa Afrika yanapambana na wanamgambo.

"Ikiwa mnataka Kenya yenye amani, hiyo haitatokea wakati watoto wenu wakiwa ndani ya ardhi yetu," msemaji wa al-Shabaab Ali Mohamud Rage alisema katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wa wanajihad.

Rage alionya kwamba mateka "wataathirika kwa mashambulizi yoyote yatakoelekezwa dhidi ya mujahidina".

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, hata hivyo, aliapa kuwa washambuliaji "wasingesalimika na matendo yao ya kuchukiza na ya kinyama".

Katika hotuba kwa taifa kupitia televisheni siku ya Jumamosi usiku, Kenyatta aliyeonekana kushtushwa, alisema, "Tutawasaka wakosaji popote watakapokimbilia. Tutawapata na tutawaadhibu kwa uhalifu huu wa kutisha."

Kenyatta alisema kuwa shambulio hilo la kigaidi lilikuwa na athari ya moja kwa moja familia yake. Siku ya Jumapili, rais alibainisha kuwa mpwa wake Mwangi Mbugua na mchumba wake Rosemary Wahito waliuawa katika shambulizi hilo.

"Ninahisi maumivu kwa kila maisha yaliyopotea na ninaungana nanyi katika huzuni na upotevu wa taifa," Kenyatta alisema, na kuwaelezea jamaa zake waliouwawa kama "vijana, wenye upendo na mimi binafsi niliwajua na kuwapenda".

"Ugaidi ni falsafa ya waoga," alisema.

Westgate, moja ya maduka ya kisasa nchini Kenya, ilifunguliwa miaka sita iliyopita na iko katika eneo la Westlands, takriban kilomita 5 kutoka katikati ya jiji. Kituo hicho cha maduka chenye ukubwa wa futi za mraba 350,000 kinatembelewa na Wakenya wakwasi, wataalamu kutoka nje na watalii huku Jumamosi ikiwa siku ya harakati zaidi.

Hasira miongoni mwa Wakenya; viongozi waomba watu kujizuia, kuwa na umoja

Shambulio hilo limechochea hasira zilizoenea miongoni mwa Wakenya huku wengi wao wakielezea ka uwazi chuki zao dhidi ya Waislamu na raia wenye asili ya Somalia.

Viongozi wa kidini na wanasiasa, hata hivyo, wanaomba uvumilivu, umoja na kujizuia kulaumu sehemu zote za jamii.

"Ninaungana na familia za waliofariki na ninawatakia majeruhi wapone haraka," alisema Sharrif Mohamed Khatamy, mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu la Kenya.

"Pamoja na hayo, ninawaomba Wakenya kuonesha uvumilivu na kuungana licha ya tofauti zao za kidini," alisema Sharrif. "Kilichotokea Westgate hakikubaliki. Ni matendo ya kudharaulika na ninayalaani kwa maneno makali sana yanayowezekana."

Kama njia ya mshikamano, Khatamy aliwaomba viongozi wengine wa Kiislamu kulaani shambulio hilo na kuungana na Wakenya wengine kwenda kuchangia damu. "Pia tunahubiri ujumbe wa upendo katika misikiti yetu na hata ya kuwa raia wanaofuata sheria na kuichukua dini yetu katika namna ya kuheshimika," alisema.

Wakati ukubwa wa mzozo huo ukiendelea kujulikana, wanasiasa wa Kenya walitumia vyombo vya habari vya kijamii kwa kutoa wito kwa wananchi kwenda kuchangia damu, ambayo inahitajika kwa vile mamia ya watu waliojeruhiwa walikimbizwa katika hospitali kadhaa.

"Nimekuja hapa kuchangia damu kwa sababu hiki ndicho ninachoweza kufanya," alisema Nduati Ngethe, mwenye umri wa miaka 51, wakati akipanga foleni huko Kencom, moja ya vibanda vya kutoa damu mjini Nairobi.

"Mimi ni mchuuzi mnyonge, lakini vilio vya watoto wachanga ambao wangeweza kufa kwa kukosa damu kumenifanya nichukue hatua," alisema Nduati Ngethe .

"Shambulio hilo la kikatili limewaunganisha Wakenya bila ya kujali makabila, mbalimbali au dini zao," alisema Rose Mueni, mwenye umri wa miaka 25, mhudumu katika Creamy Inn kwenye maduka ya Westgate, akionesha mikono yake liliyochubuka baada ya kudondoka ngazini alipokuwa anakimbia. "Natumani kuwa tutaweza kutumia janga hili kama somo la kuwa wazalendo na wavumilivu wa maoni mbalimbali  kila mmoja na tofauti za kidini duniani.

Viongozi wa kidini walaani ugaidi

"Mashambulizi haya ya kusikitisha hayana uhusiano na dini yoyote," alisema Ally Ahmed, makamu mwenyekiti wa Msikiti wa Riadha ya Pumwani. "Hii kabisa ni kazi ya magaidi wenye uchu wa damu za watu na vikosi vyetu (vya Kenya) vinafanya kazi bila kuchoka kumaliza utekaji nyara huu na kuwaokoa mateka wasiokuwa na hatia."

"Sisi kama wahubiri na viongozi wengine wa Kiislamu tuko mstari wa mbele kuwapa muongozo kaka zetu wa Kiislamu dhidi ya imani kali," alisema Ally. "Kuua ni kinyume dhidi ya mafundisho ya Uislamu na ugaidi ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Watu hawapaswi kuua kwa sababu ya dini. Hakuna wa milele duniani, hivyo natuyafurahie maisha kama zawadi kutoka kwa Mungu bila ya kuwadhulumu wengine."

Abdullahi Abdi, mwenyekiti wa Jukwaa la Kitaifa la Viongozi wa Kiislamu, alisema kwamba ingawa magaidi walio kwenye jengo la Westgate wanadaiwa kuwa Waislamu, hilo haliwafanyi Waislamu wote kuwa magaidi.

"Sisi sote ni Wakenya wapenda amani," alisema Abdi Abdullahi.

"Hao waliouwa na kulemaza watu kwenye jengo la Westgate ni wahalifu na magaidi... sio Waislamu wa Kenya au Wakenya wa Kisomali," alisema Abdi. "Hivyo, tupendane na tusichochee uhasama wa kidini kwenye nchi hii nzuri."

"Wakristo na Waislamu wameishi kwa pamoja kwa salama kwa miaka nyingi nchini Kenya," alisema Askofu Joel Waweru wa Kanisa Anglikana nchini Kenya. "Hatupaswi kuwaruhusu magaidi kupandikiza mbegu ya chuki kwenye nyoyo zetu."

"Tumewaona maulamaa na viongozi wa Kiislamu wakijitokeza kuelezea bayana kwamba Waislamu na Uislamu hauhusiani kabisa na mauaji haya ya kikatili, mateso na uharibifu wa mali," alisema"Ningependa kuwatolea wito wanasiasa kutokutia mafuta kwenye cheche za uadui."

"Kuua watu wasiokuwa na hatia kama ilivyotokezea kwenye jengo la Westgate ni tendo la woga wa hali ya juu," alisema Sheikh Mohammed Khalifa, katibu wa Baraza la Maimamu na Wahadhiri la Kenya. "Nawatolea wito Wakenya wote kuungana kuwalaani wale wanaotenda matendo ya kigaidi dhidi ya watoto, wanawake na wanaume wasio hatia bila kujali dini zao."

"Katika Uislamu, kumwaga damu na kuharibu mali ni mambo yaliyoharamishwa kabisa. Kunaweza kuwa kichochea cha kuingia kwenye uhasama wa kidini na hilo litakuwa limekidhi maslahi ya magaidi, jambo ambalo sisi wahadhiri na maimamu lazima tuwe na hadhari nalo sana," alisema.

"Ningelipenda kaka na dada zetu wapenzi wasiokuwa Waislamu kujua kwamba Uislamu uko kwenye mambo matatu: imani kwa Mungu mmoja, huduma kwa umma, na mafundisho ya uvumilivu, haki na huruma," alisema Khalifa.

"Qur'an Tukufu inafunza kwamba yeyote anayemuua mwengine isipokuwa akiwa ameua au amefanya uhalifu, ni sawa na kwamba amewauwa wanadamu wote. Na yeyote anayenusuru maisha ya mtu mmoja ni kama aliyeokoa maisha ya watu wote."

"Kwa hivyo, Qur'an inatutolea wito wa kulinda utukufu wa maisha ya mwanadamu," alisema Khalifa.

Jibu la Somalia

Nchini Somalia, wafanyakazi na viongozi wa serikali pia waliyalaani mashambulizi hayo.

Sheikh Osman Ibrahim wa Jumuiya ya Maulamaa wa Kiislamu aliyalaani mashambulizi hayo na kuyakana madai ya al-Shabaab kwamba Kenya inaupiga vita Uislamu au kuipiga vita Somalia.

"Kenya na Somalia hazipigani vita, ni majirani ambao wana maslahi ya pamoja ya kidiplomasia na kiuchumi, kwa hivyo mashambulizi hayo hayakuwa kwa maslahi ya Wasomali," alisema

"[Al-Shabaab] inamuita kila mtu kuwa si Muislamu ili kuhalalisha umwagaji damu," alisema Ibrahim. "Kila mtu anajua kuwa al-Shabaab haitetei dini yoyote ile."

Mbunge Dahir Amin Jesow alisema watu wa Somalia wako pamoja na Wakenya kwenye kipindi hiki kigumu.

"Tatizo la ugaidi linatuathiri na sisi hapa [Somalia] pia, hivyo lazima tupambane nao na tuuharibu,"

Ugaidi hauna mipaka ya kitaifa wala kikabila; ni kitisho kwa ubinadamu, alisema Jesow. Watu kote duniani lazima waungane kupambana na ugaidi kwa pamoja, alisema.

Qasim Moge Abdullahi, mkurugenzi wa Jumuiya ya Amani na Maendeleo ya Iniskoy, pia alilaani mashambulizi hayo, akiyaita ukikaji mkubwa dhidi ya Uislamu na haki za binadamu.

"Watu wanaouliwa na al-Shabaab ni raia wasio na silaha, ni wanawake na watoto, hivyo tunalaani kitendo hiki," alisema.

Abdullahi alisema nchi zinapaswa kushirikiana kuyaangamiza makundi kama al-Shabaab, lakini akaitolea wito serikali ya Kenya kutowalaumu watu wasiokuwa na hatia kwa matendo ya al-Shabaab na pia iwalinde Wasomali na Waislamu nchini Kenya dhidi ya uwezekano wa mashambulizi ya kulipiza kisasi.


Usalama kwenye majengo yenye maduka waangaliwa upya.

"Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba tumepoteza maisha ya watu wengi na wale wote waliojeruhiwa," alisema Shah Noor, mmiliki wa duka la vifaa kwenye jumba hilo la maduka.

"Natamani kungelikuwa na namna ya serikali yetu kuweza kuepusha mashambulizi haya ya kigaidi,"  . "Biashara yangu na za wenzangu zitadorora kwa sababu watu watayahusisha majengo haya ya maduka na hatari na hivyo kujitenga kando."

Noor alisema Jumuiya ya Majengo ya Maduka Makubwa ya Kenya na serikali lazima wahakiki usalama wa majengo hayo mara moja.

Mbali na Wastegate, majengo mengine yenye maduka mengi jijini Nairobi ni Sarit Centre, The Village Market, Yaya Centre, Nakumatt Lifestyle, Thika Road Mall, Capital Centre, Galleria Shopping Mall, The Junction Mall na Prestige Plaza.

Baada ya mashambulizi kwenye jengo la Westgate, mengi ya majengo hayo yalifungwa kwa muda kama hatua ya tadhari kiusalama huku polisi wenye silaha wakipelekwa.

"Ni hatua ya muda ya kiusalama na jambo la busara kufanya kwenye hali iliyopo sasa, alisema Alfred Ng'ang'a, msemaji wa mtandao wa maduka makubwa ya Nakumatt, ambao unamiliki mengi miongoni mwa majengo hayo.

"Najua wateja hawatojisikia vizuri, lakini natarajia wanafahamu kuwa ni kwa ajili ya usalama wao wenyewe," alisema

Maduka mengi yalifunguliwa tena siku ya Jumatatu kwa muda maalum, huku oparesheni ya Westgate ukiendelea.

Wizara ya Usalama wa Ndani na Uratibu wa Serikali Kuu ya Kenya iliwaomba raia kukaa mbali na eneo la jengo la Westgate siku ya Jumatatu, kwani bado lilikuwa eneo la uhalifu. Wizara hiyo ilitoa nambari kadhaa za simu ambazo raia wanaweza kuulizia taarifa za jamaa na marafiki zao: 0202724154, 020310225, 0203226771, 0203532198 na 0203556780.

Poleni sana ndugu zetu wakenya:
Tupo pamoja katika wakati huu mgumu
Mchimba Riziki

Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score