Wednesday, March 12, 2014

Atambelea Mochwari Kila Wiki Kisa Mkewe.................Soma hapa Ndani Kwa Habari Zaidi

MWANAMUME kutoka Kinango, Kwale ambaye amekatazwa na wakwe zake kumzika mkewe aliyefariki zaidi ya miaka miwili iliyopita sasa anasema amelazimika kumtembelea mochari kila wiki ili kuepuka kusumbuliwa usiku akilala.
Bw Eric Mwatela wakati wa mahojiano na wanahabari mtaa wa Jomvu, Mombasa Machi 11, 2014.


Bw Erick Guni Mwatela, mwenye umri wa miaka 28, ana kibarua cha kuzuru chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali kuu ya Pwani, Mombasa ili kuona mwili wa mkewe ambaye anasema si mwili tena kutokana na muda mrefu ambao umekuwa hapo.

“Ninalazimika kwenda katika chumba hicho kwa sababu nikikosa mke wangu marehemu Francisca Wawuda hunifuata nikilala na kutaka kujua ni kwa nini nimemuacha,” akaambia Taifa Leo hapo jana.

Bi Wawuda alifariki mnamo Februari 2012 akijifungua na sasa Bw Mwatela amebaki na mwanawe wa kike aliyezaliwa siku ya kifo hicho.

Alisema alikutana na mkewe akifanya kazi katika kiwanda cha EPZ eneo la Mazeras, wakachumbiana kisha wakaoana.

“Mke wangu aliniambia yeye ni yatima. Nyanya yake pia alisisitiza hilo na dada yake mkubwa pia akasema wao yatima. Lakini niligundua ana baba nilipoenda mochari kuchukua mwili wake ili kuuzika kuzika. Watu ambao sikuwajua walijitokeza na kusema sisi ni wezi wa maiti,” akasema.

Akaongeza: “Kulizuka kizaazaa kikubwa na hata tukaenda kortini. Kinachosikitisha ni kwamba tunapozozana, mwili wa mke wangu unaendelea kuoza na gaharama ya mochari inapanda kila siku.”
Gharama ya kuhifadhi maiti hiyo sasa imefika Sh350,000.
Jadis Munga ambaye ndiye baba ya marehemu Wawuda, anasisitiza ndiye anayestahili kumzika bintiye akisema Mwatela hakulipa mahari mkewe alipokuwa hai.

Alishinda kesi kortini akini alipoenda kuchukua mwili kuuzika akapata barua ya kumzuia kuuchukua.

“Nakumbuka nyanya ya marehemu akimuuliza baba yake sababu yake kuninyima mwili ilhali yeye pia hakulipa mahari. Sijui ni kwa nini anafanya hivyo. Naomba kusaidiwa,” akasema Mwateka na kuongeza kwamba alilazimika kuziba kaburi alilokuwa amechimba kumzika mkewe.

Alisema alilipa Sh5,000 za 'kifungua mlango’ kwa nyanya ya marehemu ndipo akawapa idhini ya kuishi kama mume na mke.

Mahakama maalum

Mnamo 2011, mkewe alipata mimba lakini akapata matatizo wakati wa kujifungua. Alilazwa katika hospitali ya wilaya ya Port Reitz mjini Mombasa na baadaye akahamishwa hadi hospitali kuu ya Pwani ambako alifariki Februari 27, 2012.

Bw Mwatela anaomba serikali imsaidie kulipa deni la mochari na kuingilia kati suala hilo ili mkewe azikwe.

Anasema Kenya inafaa kuwa na korti maalumu ya kushughulikia kesi za kimila, ada na desturi za jamii za humu nchini.

“Kuna kitu ambacho kinafichwa. Ni kwa nini baba mkwe anasisitiza anataka mwili wa mke wangu ilhali aliwatoroka? Ama ni mwanachama wa chama kimoja cha jamiiya Wachonyi chenye desturi mbaya inayoitwa wahula watu?” akauliza.

Bw Munga anasema kulingana na mila ya jamii ya Wachonyi, mwanamke ambaye hajajulisha wazazi wake kwa mchumba ama mume wake huwa hajaolewa. Kwa hivyo mume hana idhini ya kumzika hadi pale atakapotimiza mila hiyo.

Hata hivyo anasisitiza kuwa hataki hata ndururu ya Bw Mwatela kwa kuwa kimila bintiye hakuwa ameolewa.

Mchimba Riziki

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score