MWANAMUME alishangaza familia yake,
marafiki na wanakijiji alipoamua 'kufunga’ ndoa na marehemu mkewe katika kijiji
cha Kadzinuni, tarafa ya Kikambala, Kaunti ya Kilifi wakati wa mazishi yake.
Kiti Mwangudza Chilango aliamua kutimiza
ahadi aliyokuwa amempatia mkewe miaka michache iliyopita kwamba wawili hao
wangefunga ndoa rasmi.
Akiwa amevalia suti, Bw Chilango
alisimama kando ya jeneza la mkewe akiwa pamoja na msafara wa wasimamizi wake
sawa na jinsi inavyofanyika wakati wa harusi.
Pia kulikuwepo na keki ambayo
aliikata na kisha ikagawanywa kwa waombolezaji kabla ya mwili kuzikwa.
Kulingana na rafiki wa
karibu wa marehemu, Bi Mbeyu Mbura, Bw Chilango alikuwa amemuoa kwa
kitamaduni lakini mkewe alikuwa akishinikiza wafanye harusi kanisani.
Bi Mbeyu alifichua kuwa marehemu
ambaye alikuwa akiugua ugonjwa usiojulikana alikuwa amemtaka mumewe aape kuwa
atamheshimu kwa kumfanyia harusi awe hai ama akiwa amekufa, na ndio sababu
mumewe hakuwa na namna nyingine ila kutimiza ahadi hiyo.
“Tunahofia kuwa kitu kibaya huenda
kikatokea kwa mumewe ama familia ikiwa ombi la marehemu halitatimizwa. Mumewe
anaweza hata kufa,” alieleza Bi Mbeyu.
Mzee wa kijiji Kai Mwandeje alisema
kuwa hakuna jambo kama hilo limewahi kutokea eneo hilo na kusema kuwa kitendo
hicho huenda kikaleta matatizo mengine baadaye ikiwa mume ataamua kuwa anataka kuoa
tena katika siku za usoni.
“Kuvalia mavazi ya harusi
kunamaanisha kuwa roho ya mume tayari imeunganishwa na ya marehemu. Itakuwa
vigumu kuoa tena isipokuwa kama ahadi hiyo itavunjwa,” alisema Bw Kai.