Friday, October 25, 2013

Kimaiyo Atishia Kuwakamata Waandishi Wa Habari Wakiwemo Wa KTN Ya Kenya

The truth Behind Westgate Siege

Mkuu wa Polisi wa Kenya, David Kimaiyo, amewatishia waandishi wa habari kwamba atawakamata baada ya kuripoti wizi na mkanganyiko miongoni mwa vikosi vya usalama wakati wa mzingiro wa al-Shabaab kwenye jengo la maduka la Westgate mwezi uliopita.

"Ni wazi kwamba kuna kikomo" cha uhuru wa kujieleza na haki za vyombo vya habari, Kimaiyo aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatano (tarehe 23 Oktoba).

"Hamuhitajiki kusambaza propaganda ya kivita, hamupaswi kuwachochea Wakenya, hamupaswi kusambaza au pengine kutoa taarifa ambazo zinaweza kuwa sawa sawa na kauli za chuki, na hamupaswi kutoa taarifa au ripoti ambazo zinaweza kuyaathiri maisha ya mtu mwengine," alisema.

"Tunawafuatilia kisheria kwa karibu sana wale watu ambao kwa njia moja ama nyingine wanaweza kuwa wametenda matendo ya kihalifu....ambao karibuni watatiwa nguvuni na kupelekwa mahakamani, na kukabiliana na matokeo ya jambo hili," alisema Kimaiyo.

Picha za kamera za usalama kutoka siku ya pili ya kuzingirwa kwa jengo hilo, ambapo ni jeshi tu lililokuwa na fursa ya kuingia kwenye jengo hilo, zinawaonesha wanajeshi wenye silaha wakibeba mifuko meupe ya plastiki kupeleka nje ya duka.

Licha ya hayo, Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Kenya, Julius Karangi, alisema siku ya Jumanne kwamba wanajeshi hao walichukuwa vinywaji tu kwa ajili ya "kusinza kiu zao" na bidhaa nyingine "ili kuhakikisha usalama wake".

Waandishi wa habari kutoka kituo cha televisheni cha KTN nchini Kenya ni miongoni mwa wale wanaoitishiwa kukamatwa.

Vyanzo vya polisi siku ya Alhamisi vilisema timu maalum imepewa jukumu la kuwahoji waandishi wawili wa KTN akiwemo Mohammed Ali. KTN ilisema kipindi chake maalum cha saa moja kinachochunguza mashambulizi ya Westgate kilimuudhi Kimaiyo.

Onyo hilo linakuja huku bunge likitayarisha mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya vyombo vya habari ambayo itawabana sana waandishi wa habari.

Chama cha Sheria cha Kenya kilisema sheria hiyo lilikuwa "jaribio la kuingilia haki ya kikatiba ya uhuru ya vyombo vya habari na kujieleza," huku Tume ya Haki za Binadamu ya nchi hiyo ikisema ilikuwa na "wasiwasi sana".

"Vyombo vya habari vinavyoinuka kwa kasi nchini Kenya havipaswi kuandamwa kwa sababu tu ya kutangaza ukweli," alisema Tom Rhodes wa Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari. "Badala yake, polisi wa Kenya wanapaswa kuchunguza wahalifu hasa wa Westgate, na sio wajumbe."

By Mchimba Riziki

Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score