Tuesday, November 5, 2013

Wabunge wa Tanzania wapinga kanuni mpya ya maadili ya kazi

Wabunge wa Tanzania wametoa kauli ya kupinga
kanuni mpya ya maadili ya kazi iliyotolewa na
afisi ya Spika wa Bunge, kwa kusema kwamba
inakandamiza nguvu za kikatiba za wabunge za
kusimamia na kuishauri serikali.
Ofisi ya Spika wa Bunge ilisambaza kanuni hiyo
mpya siku ya Ijumaa (tarehe 1 Novemba).

Inakusudia kuzuia vurugu ndani na nje ya
bunge, kufuatilia tabia za wabunge na kuwazuia
wabunge kupokea au kutoa rushwa.
Wabunge wanaunga mkono kanuni hiyo kwa
jumla, lakini wanapingana na kutakiwa kuomba
ruhusa kutoka kwa maafisa wa serikali ili kuweza
kuona nyaraka za siri, jambo ambalo huko
nyuma haikuwa hivyo.

Deo Filikunjombe, mbunge kutoka chama tawala
Chama Cha Mapinduzi, alisema kuwa dhamiri ya
kanuni mpya ya maadili ya kazi ilikuwa nzuri,
lakini inavuka uwezo wake wa kisheria kwa
kujaribu kukiuka katiba ya nchi.
"Kifungu cha 63 (2) cha katiba yetu kiko wazi
kabisa. Kinasema kwamba mbunge atakuwa na
mamlaka kwa niaba ya watu, kusimamia na
kuishauri serikali ya jamhuri ya muungano,"
Filikunjombe alisema siku ya Jumatatu.
"Sasa, inakuwaje yule unayemtarajia
kumsimamia anatoa masharti ya kukupa habari
kwa kujisikia kwake?"

Godbless Lema, mbunge kutoka chama cha
upinzani Chama cha Demokrasia na Maendeleo,
alisema kwamba kanuni hii imeundwa
ili kuwanyamazisha wabunge wa upinzani
ambao wamekuwa wana uwezo wa kuangalia na
kutumia nyaraka za siri ili kuilazimisha serikali
iwajibike.

"Watakuwa wanajidanganya wao wenyewe
kufikiria kwamba wanaweza kutuzuia kirahisi
sana," Lema alsema. "Ikiwa itapitishwa kwa
sababu chama tawala kina wingi wa kura
bungeni, sisi tutawaambia wapiga kura kwamba
serikali imejigeuza kuwa ufalme na nina hakika
kwamba haitachaguliwa tena.

Tunataka serikali
yenye uwazi."
Kanuni mpya ya maadili ya kazi imepangwa
kujadiliwa bungeni wiki hii.


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score