Serikali imesema usajili mpya unaotarajiwa kufanywa utahusisha Wakenya wote wenye umri wa miaka 12 na zaidi. Usajili huo utakaogharimu Sh8 bilioni hautaanza kwa kutolewa kwa vitambulisho vya kitataifa lakini utanakili habari zote zitakazohitajika kutoa vitambulisho.
|
Naibu Wa Rais Kenya Willium Ruto. |
SERIKALI imesema usajili mpya unaotarajiwa kufanywa utahusisha Wakenya wote wenye umri wa miaka 12 na zaidi.
Katibu katika Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia Joseph Tiampati alisema usajili huo hautaanza kwa kutolewa kwa vitambulisho vya kitataifa lakini utanakili habari zote zitakazohitajika kutoa vitambulisho..
Kuanzia miaka 12 mtu huwa na alama wazi za vidole hivyo tayari kuwa na kitambulisho cha kitaifa,” alisema Bw Tiampati.
Kulingana na Bw Tiampati wale wako chini ya umri wa miaka 12 watatambuliwa kupitia vyeti vya kuzaliwa vyenye majina ya wazazi wao.
Katibu huyo aliongeza kuwa kando na alama za vidole, serikali itatumia macho kama sehemu za kujitambulisha hasa kwa walemavu.
Wakazi wengi wa maeneo yayochunwa chai hawana alama wazi za vidole hivyo tutawatambua kupitia macho,” alisema Bw Tiampati.
Vilevile serikali ilitangaza kuwa itakuwa na hifadhi spesheli ya habari za wageni walio nchini kihalali.
“Tutakuwa na sajili ya wale wanaoishi nchini kwa sababu zinazokubalika kisheria.”
Akizungumza Jumanne wakati wa kongamano la Connected Kenya 2014 mjini Mombasa, Bw Tiampati alisema mchakato huo utagharimu serikali Sh8 bilioni.
“Tunataka kwanza kutengeneza mfumo mwafaka wa kuweka habari na baadaye Wizara ya Usalama wa Ndani itaendeleza mchakato wa kutoa vitambulisho upya kwa Wakenya wote,” alisema Katibu huyo.
Jumatatu Naibu wa Rais William Ruto alisema hatua hiyo ya kuwasajili Wakenya upya ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usalama nchini.
“Tutaanzisha mpango wa kuwapa Wakenya vitambulisho vya kidigitali vitakavyorahisisha kutambua wanaojisajili na kuingia humu nchini kinyume na sheria,” alisema Bw Ruto.
Bw Ruto alifichua kuwa mpango huo unaopaniwa kukamilika katika kipindi cha miezi sita ijayo, unatarajiwa kupunguza visa vya ugaidi na utovu wa usalama nchini unaosababishwa na watu ambao uraia wao unatiliwa shaka.
Aidha chama cha ODM Jumanne kilitilia shaka mpango huo na kuitaka serikali kueleza kwa kina jinsi mchakato huo utakavyofadhiliwa.
Katika taarifa iliosomwa na Mwakilishi wa Wanawake kaunti ya Taita Taveta Joyce Lay,viongozi wa ODM walishangaa vipi serikali itamudu kufadhili mpango huo ilhali miradi mingine kama vile reli na vipatakilishi imekwama.
“Serikali itatoa fedha za huu mradi wapi na tayari imeshindwa kukamilisha miradi mingine. Hatuwezi kubali Wakenya kuumizwa zaidi kulipa ushuru ili kufadhili miradi ambayo haitawahi kukamilika,” alisema Bi Lay.
Bi Lay ambaye alikuwa ameandamana na mbunge wa Ugunja Opiyo Wandai na mwenzake wa Busia Florence Mutua, alisema hatua hio haina manufaa yoyote hadi serikali kwanza ikabiliane na kukomesha ufisadi miongoni mwa maafisa wake.
Serikali tayari imeunda vikundi kutoka wizara kadhaa ili kutathmini jinsi mpango huo utakavyoendeshwa kabla ya kuzinduliwa rasmi.