Friday, February 7, 2014

Chadema walia hujuma kukamatwa wabunge

Iringa. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimedai kufanyiwa hujuma, Mbunge wa Iringa Mjini kupitia chama hicho, Mchungaji Peter Msigwa amekuwa mbunge wa pili kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kujeruhi.

Msigwa alifikishwa jana katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa akidaiwa kutenda kosa hilo juzi kwa kumjeruhi kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salum Kaita kwenye mikutano ya kampeni ya kumnadi mgombea wa udiwani wa Chadema katika Kata ya Nduli, Ayub Mwenda.

Juzi, katika Mahakama ya Wilaya ya Kahama, Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbayi na wenzake 15, walipandishwa kizimbani kwa tuhuma za kuwajeruhi wafuasi watano wa CCM katika kampeni za udiwani na kulazwa rumande. Wakati hayo yakiendelea, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alijisalimisha polisi kutokana na taarifa za kutafutwa kwake kutokana na tuhuma zinazohusiana na uharibifu wa mali katika kampeni za udiwani. Aliachiwa baadae.

Mashtaka ya Msigwa

Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo Godfrey Isaya, Wakili wa Serikali, Elizaberth Swai alidai kuwa mnamo Februari 5 mwaka huu katika Kata ya Nduli, Msigwa alimjeruhi Kaita kinyume cha sheria sura ya 12 ya mwaka 2002 kifungu cha 225 cha kanuni ya adhabu.

Mchungaji Msigwa alikana mashtaka hayo na kuachiwa kwa dhamana ya Sh2 milioni iliyowekwa na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Chiku Abwao na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Lilian Msomba.

Chadema walia na polisi

Kutokana na matukio hayo, Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa Chadema, Kigaila Benson aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa Jeshi la Polisi linatakiwa kuwatia nguvuni wale wote ambao wanahusika na vitendo kuwajeruhi wanachama wao badala ya kupindisha ukweli.

Akizungumzia vurugu zinazoendelea katika kampeni za kuwania udiwani kwenye kata 27, Kigaila alisema uongozi wa CCM na Polisi kwa pamoja wanajua kinachotokea lakini wanakifumbia macho.

“Watu wetu wanajeruhiwa, wanakamatwa wanawekwa mahabusu na tunapotoa taarifa polisi hazichukuliwi hatua. Inakuaje watu wanaoumiza watu wetu hawakamatwi? Polisi wanatakiwa kuzingatia sheria na kanuni kwa wote,” alisema Benson.

Kasulumbayi apata dhamana

Mahakama ya Wilaya ya Kahama jana mchana ilimwachia kwa dhamana Kasulumbayi aliyekuwa ameshikiliwa kwa tuhuma za kuwacharanga mapanga wafuasi wa CCM kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani wilayani Kahama.

Mchimba Riziki

MABASHA WAZINDUA KITABU NAIROBI

MABASHA Jumatano walizindua kitabu chao kama hatua mojawapo ya kutaka kukubalika nchini Kenya; takriban wiki mbili tu baada ya mwandishi maarufu wa vitabu Bw Binyavanga Wainaina kujitokeza hadharani na kusema kuwa ni shoga.
Nakala Ya Kitabu Cha Mabasha Kilichozinduliwa Nairobi Jumatano. 
Kitabu hicho chenye kichwa: Wasioonekana - Hadithi za Jamii Fiche nchini Kenya, kimeandikwa na aliyekuwa mwanahabari na mwanaharakati wa kutetea haki za mashoga, Bw Kevin Mwachiro.

 Kitabu hicho chenye  kurasa 114 kinajumuisha mkusanyiko wa hadithi za watu ambao wanadaiwa kupitia hali ngumu baada ya kudhihirika kuwa ni mabasha katika maeneo yote nchini.

Kulingana na Bw  Mwachiro, 40, kuna Wakenya wengi ambao hawajaweka hadharani kuwa wana uhusiano na watu wenye jinsia moja kutokana na hofu ya kutengwa  na jamii.

Huku hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho, jijini Nairobi iliyohudhuriwa na wanaharakati mbalimbali wa kueteta haki za mabasha, Bw Mwachiro alisema mabasha wamenyimwa nafasi yao katika jamii nchini Kenya.

“Naamini kitabu hiki kitaifanya jamii kuamini kuwa mabasha wanapatikana katika maeneo yote nchini Kenya na wala sio Mombasa,”  akasema Bw Mwachiro ambaye alikuwa mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC).

Katiba
 “Kwenye Jarida la kitabu changu kuna mguu wa mtu ambaye huwezi ukatambua ikiwa ni mwanamke au mwanaume, hiyo ina maana kuwa watu unaokutana nao mitaani huwezi hukawatambua kuwa wana uhusiano wa aina gani,” akaeleza.

Kenya ni miongoni mataifa ya Kiafirika ambayo yameharamisha ndoa za jinsia moja. Hata hivyo, mabasha wanadai kuwa ushoga na usagaji vimejumuishwa katika katiba kwani katiba imempatia Wakenya haki ya kushirikiana na  mtu yeyote. Barani Afrika, nchi ya Afrika Kusini ndiyo ilikuwa ya kwanza kuhalalisha ndoa za jinsia moja mwaka wa 2006.

Bw Binyavanga ambaye alikuwepo katika uzinduzi huo aliwataka mabasha ambao wanaona haya kujitangaza wafanye hivyo huku bado wakiwa hai.

Bw Binyavanga alipasua mbarika kuwa ni shoga wiki mbili zilizopita jambo ambalo lilileta mjadala mkali nchini huku baadhi wakimtaja kama shujaa ilhali wengine wakishutumu hatua hiyo.


Chanzo Swahili Hub
Mchimba Riziki

Serikali Ya Kenya Kutumia 27Ksh Bilioni Kuzalisha Umeme Wa Takataka.

Kwa gharama ya shilingi bilioni 27 (dola milioni 314 ) mradi wa kuzalisha umeme kutokana na takataka ulipangwa kuzinduliwa tarehe 24 Februari, maofisa wana matarajio ya matokeo mazuri kwamba hatimaye Nairobi imepata suluhisho la muda mrefu la kudhibiti takataka.

Jalala Kubwa La Taka Dandora Jijini Nairobi
Serikali ya Kaunti ya Nairobi ilitia saini makubaliano tarehe 28 Septemba na makampuni ya Ujerumani Sustainable Energy Management UG na ISO International Development & Consulting GmbH, kujenga mtambo wa kurejeleza taka ngumu kwa kubadilisha mamilioni ya tani za ujazo za taka ngumu, taka zenye kikaboni na zisizo na kaboni kuwa umeme.

Mtambo huo mpya unatarajiwa kuchukua miaka miwili kujengwa na utatoa ajira za moja kwa moja 250 na nyingine 1,000 kwa ajili ya kukusanya, kuchambua na kuweka alama takataka kabla ya uzalishaji wake.

"Udhibiti wa takataka umekuwa ukiumiza vichwa kwa watunga sheria pamoja na wakaazi wa jiji hili kwa muda mrefu," Gavana wa Kaunti ya Nairobi Evans Kidero aliiambia Sabahi. "Kwa kuwa na mradi huu, matarajio yetu yanaonyesha kwamba tunaweza kuzalisha megawati 70 za umeme kwa saa kutokana na takataka zinazozalishwa na jiji hili."

Kidero alisema umeme utakaozalishwa utauzwa kwenye Kampuni ya Umeme ya Kenya kuunganisha na mfumo wa taifa. Utasaidia kushughulikia tatizo la kukatika mara kwa mara kwa umeme na mgao unaotokea wakati wa saa za kuhitajika sana na wakati mabwawa ya kuzalisha umeme yanapokarabatiwa.

Wakaazi wa Nairobi milioni 3.2 wanazalisha tani za takataka 2,000 kwa siku, lakini serikali ya jiji inakusanya kati ya tani 850 na 1,100 tu kila siku, kwa mujibu wa gavana.

"Kiasi kinachobakia kinatupwa katika majalala yasiyoruhusiwa kisheria au hazikusanywi katika maeneo zilipo, Kidero alisema. "Mradi huu utaboresha uwezo wetu wa kukusanya kwa sababu jinsi tutakavyokusanya takataka nyingi, ndivyo hivyo hivyo mtambo huu utazalisha umeme mwingi."

Alisema kaunti itaongeza magari yake ya kusafirisha takataka kukusanya taka katika maeneo ya jiji na kuunda vituo vya kukusanya takataka huko Nairobi pamoja na lengo la ukusanyaji wa tani za ziada 800 kila siku.

Nairobi safi na yenye afya zaidi
Kidero alisema mradi huo ni wa aina yake pekee katika nchi. "Utatufanya tufikia ndoto yetu ya muda mrefu ya kusaficha jiji ambayo imekuwa changamoto kwa sababu ya ukosefu wa utaalamu wa kiufundi wa kudhibiti takataka," alisema.

"Takataka zinazotokana na mabaki zinafikia asilimia 60 ya taka ngumu katika jiji hili. Machinjio mengi hayawezi kwa ufanisi kutupa takataka zake katika hali ya usafi unaotakiwa au kiwango cha usalama, lakini nina hakika [hawa] watafarijika na kuwa tayari kupeleka taka zao kwenye mradi huu," alisema.

Mtambo wa umeme utajengwa kwenye eneo la jalala la Dandora kwenye vitongoji vya mashariki mwa Nairobi. Ni mojawapo wa jalala kubwa Afrika lenye ekari 30 na maeneo ya kusafisha, na wakaazi wanaoishi karibu wataunga mkono mradi huu kama suluhisho la muda mrefu kwa tishio la afya ambalo linaathiri maisha yao mara kwa mara.

"Imekuwa ikichukiza machoni kwa miaka mingi," alisema Sarah Njoroge, mama wa nyumbani mwenye umri wa miaka 45 ambaye anapanga nyumba karibu na eneo la jalala. "Kunapokuwa na joto, harufu mbaya inachefua na hatuwezi kula kwa amani kwa sababu ya nzi wanaozagaa. Sasa nimepata faraja mtambo unaokuja utakuwa ni suluhisho la kudumu."

Njoroge alisema anaogopa hatari ya afya inayohusiana na maeneo ya jalala kwa sababu inavutia panya, ambao wanaingia majumbani na ndege wanaokula mizoga, ambao wanakula takataka katika makazi ya wakaazi.

"Kuna hatari ya kupata magonjwa kwa sababu kile kinachotupwa hapa hakijapunguzwa makali na kinatokana na taka za viwandani, kilimo, majumbani na hospitali," aliiambia Sabahi.

Kaberia Lula, mhandisi makenika mwenye umri wa miaka 32 ambaye anaishi Nairobi, alitarajia mradi huo kuwa utazidi mategemeo.

"Utekelezaji wa taka kuwa nishati na kuchoma utakuwa mfano kwa kaunti nyingine," aliiambia Sabahi. "Nairobi kutumia utaratibu wa kukusanya taka kutoka katika kaunti nyingine kutahitaji njia ya usambazaji mara mradi huu utakapoanza."

Mradi wa taka kuzalisha nishati 'mfano unaoshamiri'
Ayub Macharia, mkurugenzi wa elimu ya mazingira, ushiriki usio rasmi na wa Umma katika Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira, alisema mradi huo utaonyesha njia kwa ajili ya ukarabati wa eneo la jalala Dandora, ambao utawanusuru watu na mazingira pia.

Kenya inazalisha megawati 1,600 za umeme kila siku dhidi ya mahitaji makubwa ya megawati 1,500, mahitaji yakiwa yanaongezeka kwa wastani wa asilimia 8 kwa mwaka, kwa mujibu wa takwimu kutoka Shirika la Uzalishaji wa Umeme la Kenya (KenGen).

KenGen inazalisha zaidi ya megawati 1,200, wakati kampuni nyingine binafsi zinazalisha kiasi kinachobaki.

"Huu utazalisha megawati 70 zitakazojazia usambazaji wa umeme kwa sababu kwa kuwa na maendeleo ya majengo yanayoibuka, umeme zaidi utahitajika jijini na katika nchi kwa ujumla," Macharia alisema.

Alisema maeneo mengine ya Kenya, hususan majiji makubwa yanapaswa kutumia mkakati wa taka kuwa nishati kwa sababu nishati jadidifu inapunguza matumizi ya nishati asilia na kwa hiyo kuwa suluhisho la kuongezeka kwa joto duniani.

Sehemu ya kitengo cha mtambo mpya itatumika kubainisha vioo, plastiki, chuma, kadibodi na vifaa vingine vinavyoweza kurejelezwa. Kwa sasa urejelezaji unafanywa na kampuni ndogo na watu binafsi katika kiwango cha chini.

"Kimsingi, imetatua mahitaji ya kuhamisha eneo la jalala kama mamlaka ya jiji inavyopendekeza," Macharia aliiambia Sabahi. "Mradi huu utafanya kazi kama mfano unaoshamiri kwa kampuni nyingine za kaunti za Kenya. Ni hatua kubwa kuelekea mwanzo wa upunguzaji, utumiaji tena na urejelezaji wa taka."

Mchimba Riziki

Tuesday, February 4, 2014

Vikosi Vya Usalama Vya Kenya Vyavamia Msikiti Mombasa Kenya

Masjid Mussa, msikiti katika jiji la Mombasa,Kenya, ilikuwa Jumapili (tarehe 2 Februari) eneo la makabiliano mengine kati ya vikosi vya usalama vya nchi na vijana wanaoshukiwa kuwa wenye siasa kali.

Ofisa wa polisi akielekeza kirungu kwa wanaume
waliowekwa chini ya ulinzi nje ya Masjid Mussa huko
 Mombasa tarehe 2 Februari, 2014. [Na Ivan Lieman/AFP]
Vikosi vya usalama vilivamia jengo la msikiti Jumapili jioni katika kukabiliana na kile kinachosemwa kilikuwa jitihada zilizopangiliwa za kuandikisha vijana na kutoa mafunzo kwa vijana kwenye shughuli za jihadi, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Mombasa Robert Kitur aliiambia Sabahi.

Kati ya watu watatu waliouawa katika tukio hilo, mmoja alikuwa ofisa wa polisi ambaye alikufa kutokana na majeraha ya visu, alisema, akiongezea kwamba watu 200 walikamatwa katika mapambano hayo.

Kijana akionyesha ukaidi akiwa ameshikilia bango la jihadi
baada ya kukamatwa katika eneo la Majengo la Mombasa
tarehe 2 Februari, 2014. [Na Ivan Lieman/AFP]
Mahakama Jumatatu, iliagiza kwamba watu 129 waliokamatwa katika operesheni hiyo, ikiwa ni pamoja na wanawake watatu, kuendelea kuwa chini ya ulinzi hadi tarehe 7 Februari kutoa muda kwa polisi kukamilisha uchunguzi, Kitur alisema.

Vijana wa kiume wakiwa wamelala chini nje ya Masjid
 Mussa huko Mombasa baada ya kukamatwa tarehe 2
 Februari, 2014. [Na Ivan Lieman/AFP]
Wakati vikosi vya usalama vikielekea msikitini, vilikutana na vijana wenye silaha, mapanga na fimbo, wakikataa kuwaruhusu kuingia katika eneno hilo, kwa mujibu wa Kitur. Alisema vikosi vya usalama vilivamia msikiti huo baada ya vijana kukataa kutekeleza amri ya kujisalimisha na kuwapiga risasi maofisa polisi.

"Tuliwanyang'anya visu, fimbo na bendera zinazohusiana na al-Shabaab. Polisi walipanda kwenye minara kuondoa bendera zilizokuwa zikipepea," Kitur alisema, akiongezea kwamba iliwachukua vikosi vya usalama zaidi ya saa tano kuweka hali ya usalama katika majengo manne ya jengo la msikiti.

ABaadhi bya watu waliokamatwa wakati wa operesheni
 kwenye Masjid Mussa wakipelekwa mahakamani
Jumatatu na vikosi vya usalama (tarehe 3 Februari) katika
kitongoji cha Shanzu cha Mombasa. 
"Tulipata habari za mkutano wa Alhamisi [tarehe 30 Januari] kupitia dokezo la tahadhari kutoka katika jamii. Mkutano huo ulitangazwa pia kupitia vipeperushi na vyombo vya habari vya jamii," alisema. "Tulitoa tahadhari kwamba hatutaruhusu mkutano kama huo kwa sababu ni kinyume cha sheria."

Mkuu wa polisi wa mkoa wa Pwani Aggrey Adoli alisema vikosi vya usalama vilikuwa tayari kumaliza mara moja vurugu ili kuleta hali ya kawaida kwenye mji.

Alisema vikosi vya usalama vilikuwa katika tahadhari endapo mkutano na ulinzi wa usalama unaofuatia ulikuwa ni hila za kuvizuia vikosi vya usalama kutokana na mashambulizi ya al-Shabaab pengine popote.

"Mkutano wa watu wenye msimamo mkali ulikuwa ukiendelea tangu asubuhi. Pia tunachunguza kwamba mkutano ulifanyika Ijumaa," aliiambia Sabahi. "Tunaamini vijana walitaka kuleta hali ya vurugu idumu kwa saa au siku kadhaa au hata miezi kuleta uzingativu. Vijana waliasi agizo la vikosi vya usalama kuondoka bila ya masharti kwenye mkutano na kutawanyika."

Polisi walitaka kuutawanya mkutano kwa amani, na kuepuka kuwa na majeruhi na uharibifu kwenye sehemu takatifu, alisema.

Adoli alisema viongozi wa usalama wanapanga kufanya mkutano na wahubiri wa Kiislamu katika mkoa ili kujadili hali inayoendelea. Sehemu ya ajenda ya mkutano itakuwa kujadili uwezekano wa kufunga Masjid Mussa kwa sababu ya kutumiwa kwake na vijana na wahubiri wenye msimamo mkali kuleta vurugu nchini, alisema.
"Tunaamini kikundi cha wenye msimamo mkali kinatumia msikiti katika kujaribu kuvutia utumiaji nguvu wa usalama ambao matokeo yake unavutia upinzani dhidi ya vikosi vya usalama," alisema.

Katika kujibu uwezekano wa kufunga msikiti, Seneta wa Kaunti ya Mombasa Hassan Omar Hassan alisema Jumapili kupitia Facebook, "Nina matumaini ya dhati kwamba ripoti kama hizo sio za kweli kwa kuwa hakuna serikali inayoweza kufanya tukio kama hilo la uvunjaji mkubwa wa sheria dhidi ya dini yoyote. Kitakuwa ni kitendo cha uchokozi ambacho ninakipinga kabisa."

"Ninawaomba viongozi wote na raia wetu wote wa Mombasa kutumia jitihada zetu nzuri ili kutafuta suluhisho kwa masuala haya," alisema, akiongeza kwamba suluhisho "lazima lipatikane kwa uhusishaji na majadiliano".

Masjid Mussa unafahamika kwa kusambaza msimamo mkali na unajulikana kufuatwa mara kwa mara na wafuasi wa marehemu Aboud Rogo Mohammed aliyeuawa kwa kupigwa risasi akiendesha gari mwezi Agosti 2012, tukio ambalo lilichochea siku kadhaa za vurugu Mombasa.

Rogo na wafuasi wake mara nyingi walitumia msikiti kama mahali pa kutolea hotuba, mahubiri na mihadhara kuhusu uadilifu wa jihadi.

Uvamizi wa Msikiti wasababisha Kero




Abdi Mwashumbe, 34, mkazi wa Mombasa, alisema alikuwa ndani ya msikiti wakati makabiliano kati ya vijana na vikosi vya usalama yalipoanza.

Alisema wasiwasi ulianza kujengeka wakati maofisa wa polisi walipotumia vipaza sauti kuamrisha waumini kuondoka msikitini huku wakiinua mikono yao juu.

Amri zote zilifuatiwa na kundi la vijana ndani ya msikiti kukariri kaulimbiu za kidini, alisema.

"Baadhi ya waumini walikuwa hawajui kama mikutano ya wenye msimamo mkali ilikuwa ikiendelea katika eneo hilo," Mwashumbe aliiambia Sabahi. "Wote tuliokuwa hatuna taarifa ya chochote tulitaka kufuata amri ya polisi na kutoka nje, lakini baadhi ya vijana ndani walitutaka tuondoke."

"Ilionekana kama hali ya mateka kwa sababu tulikuwa tukitumikia kama ngao," alisema, akiongeza kwamba baada ya saa mbili alikuwa na uwezo wa "kutembea kawaida na kupenya kimyakimya kutoka nje ya msikitini".

Mwashumbe alisema kwamba muda ya saa 9 alasiri, baada ya kuondoka, alisikia bunduki na mabomu ya machozi yakirushwa.

"Ninaamini polisi watawahoji kikamilifu wale waliowakamatwa kwa sababu baadhi yao hawana hatia," alisema.

Sheikh Abdallah Kheir, imam na mhadhiri wa sosholojia katika Chu Kikuu cha Kenyatta, alishutumu matumizi ya nguvu msikitini.

Alisema mkutano msikitini ulitangazwa kama mhadhara wa dini na polisi haikuwa na sababu ya kuuvuruga.

"Msikiti ni mahali patakatifu, lakini polisi waliingia msikitini wakiwa na viatu vyao na kufyatua risasi zao na mabomu ya machozi ndani ya msikiti," aliiambia Sabahi.

Kwa mujibu wa vyanzo vya polisi, maofisa walifyatua silaha zao nje ya msikiti.

Kheir alisema serikali inapaswa kushughulikia msimamo mkali kwa kutoa fursa kwa vijana.

"Vijana wengi hawana cha kufanya na wapo hatarini kwa wanaitikadi ambao wanabadilisha mawazo yao. Serikali pia inahitaji kushughulikia uonevu wa kihistoria na kutengwa kwa vijana katika mkoa wa Pwani," alisema.

Chanzo Sabahi
Mchimba Riziki

Sunday, February 2, 2014

MWANAMKE AMWACHA MTOTO MCHANGA KWA KONDAKTA NA KUTOWEKA

Kulizuka kizaazaa katika kituo cha mabasi mjini Karatina mwanamke alipomuachia kondakta mtoto mchanga na kutoweka.
Kulingana na walioshuhudia kisa hicho, mwanamke huyo alimuacha mtoto akisema ameenda kutoa pesa katika duka la M-Pesa ili kumnunulia mwanawe chakula.
Kondakta aliye achiwa mtoto

“Aliniomba nimshikie mtoto ili aweze kutoa hela katika duka la M-Pesa za kumnunulia mwanawe maziwa,” alisema Bw Karungaru.
Kondakta huyo alieleza kuwa baada ya kumuacha mtoto huyo, mama alitoweka kabisa na ilimbidi kukaa na mtoto siku nzima huku akiomba angalau mama mtoto arejee.

Baada ya kuona mama harejei, kondakta aliamua kumpelekea mkewe mtoto huyo ili amtunze.
Baadaye alienda katika kituo cha polisi cha Karatina kupiga ripoti ambapo maafisa walimwambia aendelee kuishi na mtoto huyo huku wakiendelea kufanya uchunguzi zaidi kuhusu kisa hicho.

Kulingana na Bi Milka Muthoni, ambaye ni mkewe Bw Karungaru, wako tayari kuendelea kumtunza mtoto huyo.
“Mimi sina shida kulea mtoto. Iwapo mama yake atakataa kurudi nitamchukua kama mwanangu,” alisema Bi Muthoni.

Kumlea

Hata hivyo, Bw Karungaru anahofia kuwa hata kama wanaweza kumlea, jamaa wa mtoto wanaweza kuamua kumchukua atakapokuwa mtu mzima.

“Hofu yetu ni kuwa kwa vile hatujui alipotoka mama huyo, tunaweza kumlea mtoto huyu lakini baada ya miaka kadha familia yake idai kupewa mtoto wao,” alisema Bw Karungaru.

Hata hivyo, alisema kuwa wanafanya kila juhudi kuhakikisha wamefuata sheria na kumchukua na kuishi naye kwa njia halali.
Maafisa wa polisi wanafanya uchunguzi ili kufahamu alipotorokea mama mtoto.

MCHIMBA RIZIKI

Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score