Thursday, November 14, 2013

KAMA UNA MACHOZI YA KARIBU USISOME..!! SIMULIZI YA KWELI YA KUSISIMUA NA KUSIKITISHA YA MTOTO JANETH..!!

KAMA UNA MACHOZI YA KARIBU
USISOME..!! SIMULIZI YA KWELI
YA KUSISIMUA NA KUSIKITISHA
YA MTOTO JANETH..!!

Kengele ya kutoka darasani iligongwa,
wanafunzi wa shule ya msingi wakaanza
kutoka madarasani huku wakifukuzana
wengine wakipiga kelele ilimradi shwangwe
tu.

Ilikuwa mara yangu ya kwanza kufundisha
shule za hatua hiyo.
Ilikuwa ni shule ya serikali.
Jicho langu liliangukia katika sura ya
msichana mdogo, nguo zake chafu. Alikuwa
analia.
Alikuwa peke yake na hakuwa na yeyote wa
kumbembeleza.
Mimi kama mwalimu sikutaka kujisogeza
karibu naye sana. Kwanza nilikuwa mgeni.
Nikaachana naye.

Siku iliyofuata tukio kama lile likajirudia.
Msichana yuleyule wakati ule uleule wa
kutawanyika, alikuwa analia sana.
Mwishowe aliondoka huku akiwa analia.
“Mbona mwenzenu analia?” nilimuuliza
mwanafunzi mmoja.
“Huyo ni mama kulialia..” alinijibu huku
anacheka.

Haikuniingia akilini hata kidogo kuwa yule
binti analia bila sababu.
Siku ya tatu nikaanza kujiweka karibu naye.
Muda wa mapumziko nilimwita
nikamnunulia chai, alikuwa ananiogopa na
hakutaka kuniangalia machoni.
Sikumuuliza lolote juu ya tabia yake ya kulia
lia kila anaporuhusiwa kurejea nyumbani.

Hata siku hiyo pia alilia vilevile. Wenzake
wakawa wanamzomea.
Akili yangu iligoma kuamini kuwa binti yule
analia bila sababu.
Kwanini alie wakati wa kutawanyika tu??
Hapana si bure.
Nikaendelea kujiweka karibu naye. Mkuu wa
shule akafikishiwa taarifa kuwa nina
mahusiano ya kimapenzi na yule mtoto.

Moyo wangu na Mungu pekee ndio walikuwa
mashahidi. Nilikosa cha kujibu.
Nilijaribu kujiweka mbali naye lakini moyo
ulinambia kuwa kuna jambo natakiwa
kulijua.

Nikaendelea kuwa karibu naye. Hatimaye
mkuu wa shule akanisimamisha kufundisha
pale kwa tabia yangu ya kufanya mapenzi na
mwanafunzi.
Nilijitetea lakini sikueleweka. Nikamwachia
Mungu……
Licha ya kusimamishwa kazi, niliendelea
kufuatilia nyendo za yule binti aliyeitwa
Janeth.
Kila alipotoka shule nilimvizia njiani na
kumnunulia chakula, kisha tunazungumza
kidogo.

Aliponiamini kama kaka yake ndipo
nikajieleza dukuduku langu.
“Janeth…” nilimuita.
“Bee kaka ….” Aliitika huku akinitazama.
“Nyumbani unaishi na wazazi.”
“Ndio naishi na mama..baba huwa anasafiri
safari.”

“Mama yako ana watoto wangapi?”
“Mama yangu alikufa….alikufa nikiwa mdogo
hata simkumbuki” Alijibu kwa sauti ya chini.
“Kwa hiyo unaishi na mama mdogo.”
“Ndio.”
“Unampenda mama mdogo?”
Swali hili likaikatisha furaha ya Janeth.
Akaanza kulia, alilia bila kukoma, Janeth
alilia kwa uchungu hadi nikajisikia vibaya.
Nilimbembeleza kisha sikumuuliza tena.

Siku zikaenda bila kumuuliza chochote..
Baada ya siku kumi, ilikuwa siku ya michezo
pale shuleni, hivyo hapakuwa na masomo.
Janeth alichelewa kuja shule, nilimngoja
uwanjani, hadi alipofika majira ya saa nne.
Nikamwambia twende kunywa chai.
Siku hiyo nilimpeleka mbali kidogo,
tukanywa chai, kisha tukakaa mahali
palipokuwa wazi.
Nikaleta tena mjadala mezani.
Ni kuhusu maisha ya Janeth.
Alikataa kabisa kusema lolote, nilimshawishi
sana.

“Usiogope mimi ni kaka yako.” Nilimpooza.
Janeth badala ya kusimulia akaanza kulia
tena.
“Ataniua mama nikisemaaaa” alilalamika.
Nikambembeleza hatimaye akanieleza jinsi
anavyonyanyaswa na mama yake.

“Mama hanipendi hata kidogo, ananipiga na
kuninyima chakula, hapendi nije shule,
vyombo tunavyotumia usiku hataki nivioshe
usiku na hataki niwahi kuamka asubuhi,
nikiamka natakiwa kufanya kazi zote,
kufagia uwanja, kudeki nyumba, kuosha
vyombo kisha ndipo nije shule. Baba
akiwepo anajidai kunijali sana…”
Alijieleza.
“Ni hayo tu Janeth….niambie kila kitu.”
“Akijua ananiua alisema….”
“Kwani amewahi kukutesa vipi..”
Ni hapa Janeth alivyozungumza huku analia
kilio ambacho hakitatoka masikioni mwangu
kamwe.

Siku moja, alichelewa kuamka, ilikuwa siku
ya mapumziko.
Mama yake alipomwamsha, aliitika na
kupitiwa usingizi tena.
Mama aliporejea mara ya pili, alikuwa na mti
mkavu, alimpiga nao kichwani na popote
pale katika mwili, alipoona hiyo haitoshi
akamvua nguo, akausokomeza katika sehemu
za siri, aliuigiza hovyohovyo, ukuni huo
ulikuwa wa moto.

Yeyote mwenye moyo wa nyama ajifikirie
ukuni wa moto ukazamishwa sehemu za siri
za mtoto wa darasa la sita.
Nilitokwa machozi.
Nikawahi kujifuta hakuona.
“Baba yeye alisemaje….”
“Baba ni mkali na hapendi kunisikiliza na
mama aliniambia nikiambia mtu ananiua
mara moja.” Alijibu kwa huzuni.
“Nikija na dada yangu tunaweza kukuona
ulivyounguzwa..”
“Ndio…” alinijibu.
Sikutaka kulaza damu nikampigia simu rafiki
yangu wa kike.
Nikamuuliza kama yupo kwake, alikuwepo.

Nikaongozana na Janeth.
Tukafika, Janeth akatoa nguo zote.
Ilihitaji moyo wa kiuaji sana kutazama mwili
wa Janeth mara mbilimbili.
Alitisha, hakika alikuwa ameunguzwa vibaya
na vidonda vilikuwa havijapona vizuri.

Dada yule alishindwa kujizuia alimlazimisha
Janeth twende kwa mama yake amkabiri na
kumpa kipigo. Nikamzuia.
Hata mimi nilikuwa na hasira kali. Lakini
sikutaka kuiruhusu ifanye kazi.
Nikachukua kamera, nikampiga picha Janeth
katika yale makovu.

Mbio mbio nikaenda polisi, kituo cha haki za
watoto nikaelezea mkasa ule huku
nikishindwa kujizuia machozi.
Nikawaonyesha na picha.
Tukaongozana nao hadi nyumbani kwao
Janeth.
Mama yule akakamatwa bila kutarajia.
Nilitamani kumrukia nimng’ate lakini
haikuruhusiwa.
Sheria ikafuata mkondo. Janeth akaanza
kupokea tiba.

Yule mama akahukumiwa kwenda jela miaka
sita..hadi sasa yupo jela.
Mume wake alitozwa faini kubwa kwa kosa
la kutofuatilia maendeleo ya mtoto wake
kiafya……..

Mimi nilirudishwa kazini, kwa heshima
kubwa. Heshima ya nkumkomboa mtoto.

***Akina JANETH wapo mtaani
kwako…..usiwaangalie na kuwaacha tu…
hebu jaribu KUWA SAUTI YAO… .hawawezi
kusema…hebu sema badala yao…….wanalia
kisikie kilio chao…….

KAMA UMEGUSWA NA MKASA HUU SHARE
NA NDUGU JAMAA NA
MARAFIKI ZAKO ILI WAONE.

SOURCE Kandilihuru Blog.

Warioba Atoa Rambirambi kwa Familia Ya Dr Mvungi

Wakili wa Tanzania na mjumbe wa Tume ya
Kupitia Katiba (CRC) Sengondo Mvungi ,
aliyekuwa amejeruhiwa vibaya mapema mwezi
huu Alipovamiwa nyumbani kwake karibu
na jiji la  Dar es Salaam, alifariki siku ya Jumanne katika hospitali moja
nchini Afrika Kusini.

Kiasi cha watu sita wanaoshukiwa kuwa wezi
waliokuwa wamebeba mapanga walimshambulia
Mvungi nyumbani kwake siku ya tarehe 2
Novemba.

Alipelekewa kwa haraka kwenye
Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Muhimbili
jijini Dar es Salaam ambako alikuwa kwenye
chumba cha wagonjwa mahututi hadi tarehe 7
Novemba,
aliposafirishwa kwenda Hospitali ya
Milpark jijini Johannesburg kwa matibabu zaidi.
Polisi hadi sasa wamewakamata washukiwa tisa.

Mwenyekiti wa CRC, Jaji Joseph Warioba,
alipeleka salamu zake za rambirambi kwa
familia ya Mvungi. "Alikuwa mtafiti ambaye
daima alikuwa na hamu ya kile alichokifanya.

Nilimjua na kufanya naye kazi hata kabla ya
kuwa mjumbe wa CRC, hivyo kifo cake kwa kweli
kimeniumiza," alisema Warioba.

Washukiwa Wawili Wa Ugaidi Wauwa Eastleigh Nairobi.

Polisi ya Kenya hapo jana walifanikiwa  kuwapiga risasi na kuwauwa watu
wawili wanaoshukiwa kuhusika na mashambulizi
dhidi ya msikiti mmoja uliopo Jam Street
Eastleigh, jijini Nairobi, mwaka jana,

"Ni vijana na tumepata guruneti la mkono na
bastola moja kutoka kwao. Tunaamini walikuwa
sehemu ya genge kubwa ambalo limekuwa
likiwatisha watu," alisema Kamanda wa Polisi wa
Kaunti ya Nairobi, Benson Kibui.

Washukiwa hao waliuawa karibu na kituo cha
kurekebisha magari yaani Garrage  hapa Eastleigh.

Bado haifahamiki kama
walikuwa wanadhamiria kutumia bomu hilo
kufanya mashambulizi ya kigaidi.
Walikuwa wanasindikizwa na kijana wa tatu,
ambaye polisi sasa wanamtafuta, alisema Kibui,
kwa mujibu wa kituo cha Capital FM.

Wanaaminika kuwa sehemu ya kundi
linalohusika na mashambulizi dhidi ya waumini
waliokuwa wakitoka kwenye msikiti wa Al Hidaya
baada ya sala ya Ijumaa mwezi wa Disemba
2012, ambapo watu watano waliuawa na 16
kujeruhiwa, akiwemo mbunge wa Kamukunji,
Yussuf Hassan.

Mashambulizi dhidi ya raia hapa Eastleigh yalikithiri mwishoni  mwaka jana kwa kundi lisilojulikana kushambulia
Sehemu yenye mkusanyiko ya watu wengi lakini polisi wa kulinda raia walithibiti hali hiyo mpaka sasa hali ya usalama wa kutosha ipo katika mtaa huu.

Mchimba Riziki

Tuesday, November 12, 2013

Ligi Kuu Somalia Yashika Kazi.

Mchimba Riziki Michezo.

Ligi Kuu ya Somalia ilianza kwenye Uwanja wa
Michezo wa Benadir, Mogadishu, siku ya Ijumaa
(tarehe 8 Novemba), kwa mechi ya kwanza kati
ya timu za Heegan na Gaadiidka kumalizika kwa
ushindi wa 3-2 wa Heegan.

Ligi hiyo kuu inafanyika kwenye uwanja wa
kisasa ukiwa na nyasi bandia kwa mara ya
kwanza baada ya shirikisho la mpira la
kimataifa, FIFA, kuufanyia matengenezo Uwanja
wa Benadir .

Timu nane za mpira wa miguu za Somalia
kutoka mikoa ya Benadir, Shabelle ya Chini na
Shabelle ya Kati zitashiriki kwenye ligi hii, Katibu
Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la
Somalia, Abdiqani Said Arab, alidokeza.

"Uwanja wa Michezo wa Benadir ulijengwa
mwaka 1956, lakini ukakumbwa na maharibiko
makubwa [wakati wa vita vya wenyewe kwa
wenyewe]," alisema Arab. "Hata hivyo, baada ya
matengenezo yaliyofanyika miaka miwili iliyopita,
umeboreshwa na kuwa na viwango vya kisasa.
Matengenezo hayo yalimalizika tarehe 1
Novemba, na ligi kuu ilianza tarehe 8
Novemba."

"Naishukuru FIFA kwa kuweka nyasi za bandia
uwanjani hapo, ambazo zinakidhi viwango vya
kimataifa kwa kipimo na ubora wake,"
aliongeza.
Alisema matengenezo hayo ya uwanja
yanazifanya mechi ziwe bora zaidi.

"Kutakuwa na ongezeko la vipaji vya
wanariadha, hamasa ya mashabiki na uzuri wa
uwanja. Sasa tuko kama yalivyo mataifa
mengine duniani na tuna fursa sawa kama
walizonazo," alisema.

Arab alisema sasa wako kwenye mchakato wa
kupanga matengenezo ya viwanja vingine kwani
uwanja mmoja hautoshi kwa mechi za mpira wa
miguu nchini Somalia.
"Matengenezo ya uwanja huu yalipokamilika,
tuliiomba FIFA kutengeneza uwanja mwengine,"
alisema. "Walikubali na tunataka kuufanyia
matengenezo uwanja wa [Chuo Kikuu cha Taifa
cha Somalia]," alisema, akiongeza kwamba
watajaribu kuhakikisha matengenezo
yanafanyika kwenye viwanja vingine hadi wawe
wametengeneza viwanja kumi.

Wasomali Nusu Millioni Kurudishwa Somalia

Wakimbizi wa Kisomali nchini Kenya
wanalazimika tu kurudi nyumbani kwa hiari,
ulisema Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu
(tarehe 11 Novemba) baada ya kusaini makubali
yanayolainisha hofu ya kuwepo urudishwaji wa
lazima wa wakimbizi zaidi ya nusu milioni .

"Urejeshwaji wa wakimbizi lazima ufanyike kwa
usalama na heshima," alisema Raouf Mazou,
mwakilishi wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa
Mataifa (UNHCR) nchini Kenya, akiongeza
kwamba shirika hilo litasaidia katika kuandaa
uhamishwaji huo ikiwa tu "hali iko sahihi,"
liliripoti shirika la habari la AFP.
Makubaliano hayo ya pamoja - yaliyowekwa
saini siku ya Jumapili jijini Nairobi na Kenya,
Somalia na UNHCR - yanakuja kukiwa na hofu
za mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya
wakimbizi wa Kisomali kufuatia al-Shabaab
kulizingira jengo la maduka la Westgate mnamo
mwezi Septemba .
Tume yenye wawakilishi kutoka pande zote tatu
itaamua lini uhamishwaji huo uanze na kiasi gani
cha pesa anakachohitaji kila mkimbizi
atakayehamishwa ili kufanikisha kipindi cha
mpito.
"Serikali ya Somalia itaendelea kujenga
mazingira salama kwa wakimbizi kurudi nchini
Somalia ili kuwawezesha kujiimarisha kwa
wepesi na kujenga upya maisha yao, wakiwemo
wakimbizi milioni 1.8 wa ndani ya Somalia,"
alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia,
Fowsiyo Yusuf Haji Aadan, wakati wa kuwekwa
saini kwa makubaliano hayo, kwa mujibu wa
gazeti la The Standard la Kenya.

By Mchimba Riziki

Waziri Wa Mambo Ya Nje Wa Kenya Aitembelea Tanzania Kuitoa Shaka Juu Ya Suala La Kutengwa EAC

Dar es salaam, Tanzania

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina
Mohamed, ametetea mkutano wa Kenya na
Rwanda na Uganda mjini Kigali mwezi uliopita
bila ya wanachama wenzao wa Jumuiya ya
Afrika ya Mashariki (EAC) Burundi na Tanzania ,
liliripoti gazeti la Daily News la Tanzania siku ya
Jumatatu (tarehe 11 Novemba).

Mohamed, aliyekwenda jijini Dar es Salaam siku
ya Jumapili, alisema mkutano huo ulijadili
masuala yenye maslahi ya moja kwa moja ya
pande hizo mbili na kulenga kwenye maeneo
ambayo yanaweza kuwa yaliachwa kwenye
mkutano wa kikanda wa EAC.

Mkutano huo ulijadili ukosefu wa ufanisi wa
bandari ya Mombasa ambao ulikuwa ukiziathiri
Rwanda na Uganda ambazo hazina bahari,
alisema Mohamed, akiongeza kwamba ulifanyika
kwa mujibu wa sheria za jumuiya ya EAC na
hauakisi kutengwa kokote kwa wanachama
wengine.

Pia aliisifu hotuba ya hivi karibuni ya Rais Jakaya
Kikwete wa Tanzania ambayo ilizikosoa Kenya,
Rwanda na Uganda kwa "kujibagua zenyewe "
kutoka wanachama wengine wa EAC kwa
kuunda "muungano wa wenye dhamira" na
kusaini makubaliano kati yao.

Alisema Kenya itahakikisha inaimarisha
mafungamano na wanachama wote wa EAC
katika siku zijazo. "Tutafanya kila tuwezalo
kuhakikisha kwamba EAC inaimarika chini ya
mataifa matano wanachama wa EAC na kuleta
maendeleo kwa watu wote," alisema Mohamed.

By Mchimba Riziki

Vyombo Mbalimbali Vyazidi Kuipinga Mswada Wa Sheria Kwa Vyombo Vya Habari Kenya, Uhuru Akataa Kuitia Saini.

Nairobi, Kenya

Sauti za kutoelewana zinaendelea kuongezeka
juu ya mswada wenye utata wa vyombo vya
habari ambao bunge la Kenya liliupitisha
mwishoni mwa mwezi uliopita, huku ikiripotiwa
kwamba rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
aliurudisha kwenye chombo cha kutunga sheria
kufanya mabadiliko.

Mswada wa Habari na Mawasiliano wa Kenya
(marekebisho) wa mwaka wa 2013, ambao
unahitaji saini ya Kenyatta kuwa sheria,
umeweka faini kubwa ya hadi shilingi milioni 1
(dola11,700) kwa mwandishi wa habari binafsi
na shilingi milioni 20 (dola 234,000) kwa chombo
cha habari kwa ukiukaji wa kanuni za maadili.
Waandishi wa habari pia wangepewa adhabu
kwa kufutiwa usajili na akaunti zao za benki
kufungwa.

Watunga sheria ambao walipitisha sheria hiyo
pia waliunda Mahakama ya Rufaa ya
Mawasiliano na Vyombo vya habari, iliyopewa
jukumu la kusikiliza malalamiko na kutoa
adhabu kwa waandishi wa habari
watakaogunduliwa kuvunja sheria.
Hivi sasa
Baraza la Vyombo vya habari la Kenya
hushughulikia malalamiko kama hayo.
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia
iliteua wajumbe wa mahakama hiyo, ambayo
kazi yake ni kuunda kanuni za maadili kwa
waandishi wa habari na vyombo vya habari.

"Kwetu sisi, hii ni sheria ya uonevu ambayo
inarudisha nchi nyuma kwenye enzi za giza,"
alisema Sekou Owino, mkuu wa huduma za
kisheria wa kampuni ya Nation Media Group.
Ukweli kwamba mahakama imeundwa na
wateuliwa wa serikali, pasipo wawakilishi wa
waandishi wa habari, inalifanya lisiwe huru
hususani wakati serikali inapokuwa na maslahi
na suala hilo, aliteta.
:
Mswada huo pia unahitaji vyombo vya habari
kutumia asilimia 60 ya programu zake kwenye
"habari za ndani ya nchi", alisema. Hili ni suala
lenye ubishi kwa sababu mswada huo
haufafanui "habari za ndani ya nchi" na mahitaji
hayo yanaingilia uhuru wa vyombo vya habari,
aliongezea.
Kenyatta na Ruto wajibu kuhusiana na
wasiwasi
Wakati alipojitokeza katika Kaunti ya Kajiado
tarehe 2 Novemba, Kenyatta alisema hatasaini
mswada wa sheria hadi masuala yenye ubishi
yashughulikiwe.
"Tunakusudia kushawishi vyombo vya habari
kama hiki kuwa mstari wa mbele katika uhuru
wa kujieleza ambao wote tunaupigania," alisema
Kenyatta.

Siku ya Ijumaa (tarehe 8 Novemba), Makamu wa
Rais William Ruto alikariri kusudio la rais.
"Bunge letu lilipitisha mswada ambao tunakubali
una ubishi," aliliambia kusanyiko la viongozi wa
vyombo vya habari Afrika katika mji mkuu wa
Ethiopia Addis Ababa, kwa mujibu wa AFP.

"Rais wa Kenya amerejesha mswada kwa bunge
ili masuala haya yashughulikiwe," alisema,
akiongeza kwamba "mjadala unaandaliwa kati
ya wadau mbalimbali -- bunge la utendaji na
vyombo vya habari -- kutatua masuala yenye
ubishi."

"Uhusiano kati ya serikali na vyombo vya habari
hauhitaji ushindani," alisema Ruto.
Sheria ina lengo la 'kuwanyamazisha
waandishi wa habari'
Lakini wawakilishi wa vyombo vya habari na
wawakilishi na watetezi wanaendelea kuukosoa
mswada huo.

Kifungu cha 19, shirika la utetetezi wa haki za
binadamu lenye makao makuu huko London
ambalo linapambana na udhibiti wa habari na
kukuza uhuru wa kujieleza na wa habari.
aliielezea sheria hiyo kuwa ni ya "kizamani".
Muswada huo unakiuka vifungu vya katiba ya
Kenya na kuanzisha vifungu vya viwango vya
kimataifa vya habari, Mkurugenzi wa Kifungu
cha 19 Pembe ya Africa Henry Maina alisema.

Katiba ya Kenya inahakikisha "uhuru na
kujitegemea kwa vyombo vya habari vya
kielektroniki, uchapishaji na aina nyengine za
habari".
"Taifa halitapaswa kutekeleza udhibiti au
kuingilia kati mtu yeyote anayajihusisha na
utangazaji, utoaji au usamabazaji wa chapisho
au usambazaji wa habari kwa njia yeyote; au
kuadhibu mtu yeyote kwa maoni au mtazamo
wa yaliyomo katika habari, chapisho au
usambazaji wa habari," inaeleza.
"Lakini kile ambacho bunge imepitisha ni jaribio
la makusudi la serikali na vyombo vyake
kudhibiti vyombo vya habari kinyume na katiba,"
Maina alisema.

"Kuna vitisho vya kutosha kwa jina la usalama
wa taifa, ambapo katika hali halisi serikali
inataka kufunga nafasi za kidemokrasia za
watu," Mwenyekiti wa Chama cha Sheria cha
Kenya Eric Mutua alisema. "Hili
linapaswa kupingwa na Wakenya wote."

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wahariri wa
Kenya David Ohito alisema ukali wa adhabu kwa
uvunjaji wa sheria unaweza kusabibisha vituo
vya redio na kampuni nyengine za vyombo
vyengine kufungwa kwa sababu vingi vyao
haviwezi kulipa faini hizo zinazotarajiwa.

"Kile ambacho sheria imetolewa ni
kuwanyamazisha waandishi wa habari na
vyombo vya habari, kumaanisha kwamba
wananchi hawatakuwa na uwanja wa kujielezea
kwa uhuru dhidi ya watawala wasiokuwa
wawajibikaji. Inamaanisha kwamba nchi nzima
itakuwa imenyimwa haki ya kuieleza uhuru,"
Ohito alisema.

"Nyingi ya kampuni zetu za habari zina bajeti ya
uendeshaji kwa mwaka chini ya shilingi milioni
40 [dola 468,000]," alisema. "Ikiwa utavitwanga
na angalau faini tatu kila mwaka, maana yake
utakuwa umekula bajeti yao yote. Hawatakuwa
na chaguo lingine zaidi ya kufunga."

Na, adhabu ambazo waandishi wa habari binafsi
wanazoweza kukabiliana nazo, pia zitakuwa
kubwa mno, alisema Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Maripota wa Kenya, William Oloo Janak.
"Faini hizi ni kubwa kupita kiasi," Janak alisema . "Hakuna sheria nyengine yeyote katika
nchi hii ambayo ina faini kubwa ya utovu wa
adabu kibinadamu inayoamuliwa na mahakama.
Kwa sisi, hili ni jaribio la serikali la
kuwanyanyasa waandishi wa habari."

'Hakuna chochote cha kibabe au kinyume
na katiba katika mswada'
Hata hivyo, Jamleck Kamau, mbunge ambaye
aliupeleka mswada huo katika Bunge la Taifa,
alivishutumu vyombo vya habari vya Kenya kwa
kupotosha ukweli.

"Suala hili limekuwa likitangazwa vibaya. Kwa sisi
hakuna chochote cha kibabe au kinyume na
katiba katika mswada huo," Kamau, ambaye pia
ni mwenyekiti wa kamati ya Mawasiliano na
Habari ya bunge alisema.

"Tunawaomba rais kutia saini iwe sheria kama
ilivyo kwa sababu vipengele vya vilivyomo humo
ni vizuri kwa nchi hii kwa kuwa vitavifanya
vyombo vyetu vya habari kuwajibika zaidi na
kuwa na malengo katika kazi yao ambazo kwa
upande mwengine utaibadilisha Kenya," alisema.
"Inapotosha kweli [kusema] kwamba Mahakama
ya Rufaa ya Mawasiliano na Vyombo vya habari
itakuwa na nguvu kupita kiasi za kuwatia
mbaroni waandishi wa habari na kuvamia ofisi
za vyombo vya habari. Lakini kama tulivyosema
kabla, suala hili limetatuliwa na mswada umo
njiani kuelekea kuwa sheria," alisema, na
kukataa kufafanua zaidi.

Mchimba Riziki


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score