Tuesday, July 1, 2014

Hii Ilikuwa Ni Zaidi Ya Sodoma Na Comora.... Yalisemwa Na Kiongozi Wa Nacada Kuhusiana Na Picha Kadhaa Zilizoonekana Mitandaoni Katika Mashindano Ya Rugby Kenya Iliyofanyika Jumamosi

Mwenyekiti wa NACADA John Mututho amekashifu vikali matukio yaliyoshuhudiwa wikendi katika Kaunti ya Machakos na kuyataja kuwa maovu kuliko yaliyoshuhudiwa Sodoma na Gomora.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kitaifa ya kupambana na matumizi mabaya ya pombe na dawa za kulevya (Nacada) amekashifu vikali matukio yaliyoshuhudiwa wikendi katika Kaunti ya Machakos na kuyataja kuwa maovu kuliko yaliyoshuhudiwa Sodoma na Gomora.
“Siwezi hata kueleza...hayawezi kuelezwa na binadamu yeyote mwenye akili timamu. Yale yaliyotendwa mchana peupe na vijana kwenye uwanja wa kanisa ni mabaya zaidi ya yaliyoshuhudiwa Sodoma na Gomora,” alisema.


Maelfu ya vijana walimiminika Machakos Jumamosi kuhudhuria mchuano wa raga, maarufu kama Masaku 7s, na kujistarehesha mjini humo usiku kucha hadi Jumapili.

Hata hivyo, yaliyoshuhudiwa yalibaini vijana wengi hawakuwa na haja ya kushuhudia mchezo huo bali walivutiwa na uhuru wa kutenda anasa ambao umekuwa kama kawaida wakati michuano hiyo ya raga inapoandaliwa.

“Baada ya kulewa, kulingana na habari nilizopokea, waliingia kwenye uwanja wa kanisa na kutishia kuchoma kanisa kama hawangeruhusiwa kufanya maovu yao ndani ya uwanja wa kanisa,” akasema Bw Mututho.
Unywaji wa pombe kupita kiasi pamoja na utendaji wa ngono kiholela huwa ni kati ya anasa zinazovutia vijana wengi kwenye hafla hiyo.

Wakati mwingine, mtu yeyote hujitolea kuwa 'mhubiri’ ambaye 'hufunganisha ndoa’ watu wawili, ili kuwawezesha 'kuishi kama mume na mke’ japo kwa usiku mmoja tu.

Ingawa michuano hiyo imewahi kuandaliwa katika miji tofauti ikiwemo Nakuru na Nairobi, vituko vya Machakos vilishangaza wengi kutokana na jinsi viliangaziwa pakubwa hasa kwenye mitandao ya kijamii.


Kuvua nguo
Baadhi ya waliokuwepo Machakos walionekana wakijitokeza na kuvua nguo zao mbele ya hadhara.
Bw Mututho alieleza wasiwasi wake kuwa huenda kulikuwepo watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 mahali hapo, na kuongeza tabia hiyo haitaruhusiwa kwenye hafla zingine zilizopangiwa kufanyika Nakuru, Meru na Kakamega baadaye wiki hii.

Alisema ingawa Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua alikuwa na wazo zuri alipoandaa hafla hiyo, kuna walioingilia na kuitumia kuuzia watoto pombe.

Alitoa maoni hayo siku moja baada ya Tume ya Kitaifa ya Huduma za Watoto (NCCS) kutoa wito kwa serikali ipige marufuku disko za mchana, maarufu kama 'jam session’ ambazo hulenga wanafunzi wanapofunga shule.

Tume hiyo ilisema disko hizo hutumiwa kuuzia watoto pombe na dawa za kulevya, huku wengine wao wakishawishiwa kirahisi kushiriki ngono na watu wazima.

Maoni Ya Blogger/Mwandishi
Naomba wasomaji wa blogu hii ambao hamjazoea kuyaona maneno kama haya hapa na picha za kutisha kama itakavyoonekana.. Nimelazimika kuonesha picha kadhaa ambazo nadhani ndio jambo kila mtu anatakiwa kulikemea, Pia lakini nilijaribu kufanya hivyo ili jamii ijue hatari iliyoko mbele yetu.. Kwani tukifichiana maofu kama haya kifo itatuuumbua..

Naomba Chukua Mda kidogo kuangalia baadhi ya picha/taswira ilivyokuwa usiku huo kwenye hafla hiyo.Kama uko karibu na under 18 please usifungue...

Kumbuka Sii Haiba Yetu kuandika Habari kama hizi lakini tunataka kukemea tabia kama hizi katika jamii.

Monday, June 30, 2014

Pasta Mmoja Afukuzwa Kazi Kwa Kuendekeza Uhuni Mtaani.

Waumini wa kanisa moja la Kaunti ya Murang’a Jumapili walipitisha hoja ya kumtimua pasta wao baada ya  kutiwa rumande kwa madai ya kufanya uhuni katika jamii.
Pasta Simon Kanyoro wa kanisa la Revival Ministries lililoko katika Eneo bunge la Kigumo alitakiwa kwanza kushiriki kesi zake mbili zinazomkabili mahakamani bila ya kujihusisha na shughuli zozote za utumishi wa kanisa hilo.


Kwa kauli moja, waumini wa kanisa hilo walipitisha hoja hiyo kwa kuinua mikono juu, ambapo wote waliokuweko walionekana kuunga mkono pasta wao aondolewe majukumu yake na yakabidhiwe Naibu Pasta wao.

Katika kikao kilichoandaliwa katika tawi la kanisa hilo la Maragua, Kiongozi wa masuala ya ustawishaji wa Injili Bi Hellen Wangui aliwasilisha hoja hiyo kujadiliwa na baraza la wazee wa kanisa na ndipo hatima ya pasta huyo ikatolewa.

Kwa sasa, pasta huyo ako katika rumande ya jela kuu ya Murang’a baada ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani mwishoni mwa wiki jana alipovunja masharti ya bodi aliyokuwa amepewa na mahakama kuhusu kesi nyingine iliyomkabili.

Masaibu yake yalimwandama aliposhtakiwa kati mwa mwezi huu kwa kubomoa nyumba ya ndugu yake mdogo kufuatia mzozo wa shamba.

Aidha, alidaiwa kutisha kumuua ndugu huyo na alipowasilishwa mahakamani, akawachilia kwa bodi ya Sh10, 000, kiasi alicholipa na kuachiliwa huru kesi yake iendelee akiwa hajawekwa kizuizini.

Hata hivyo, Bw Kanyoro alikamatwa tena mwishoni mwa wiki jana baada ya kumpiga mlalamishi na kisha kutangazia maafisa wa polisi waliojitokeza kutuliza hali kuwa alikuwa ameamua kumuua ndugu huyo ili kesi yake mahakamani ipate uzito.

Dhamana
Ndipo alifikishwa mahakamani na akashtakiwa upya hali ambayo ilimfanya apoteze haki yake ya kuachiliwa kwa dhamana na akawekwa rumande.

Bi Wangui alisema kuwa hali hiyo kwa sasa inazua hoja nyeti katika mwongozo wa kanisa hilo na waumini wameanza kuonyesha kutoridhishwa kwao na hali iliyokuwa ikimwandama pasta huyo.

“Imetubidi tuwasilishe hoja ya kutafuta mwelekeo wa kanisa letu kuhusu masaibu yanayomwandama pasta wetu na hatimaye imeafikiwa kuwa kwanza ajitenge na masuala ya injili kutuhusu,” akasema.

Alisema wao hawajamhukumu pasta huyo, ila tu wangetaka kwanza aendelee na kesi zake mahakamani na kisha akifaulu, arejelee majukumu yake ya kanisa.
“Lakini kwa sasa, pasta wetu amesimamishwa kujihusisha na masuala ya kanisa hadi wakati atakapomalizana na kesi zake. Ikiwa atafungwa jela, basi tutakuwa na wajibu wa kutafuta mwongozo mbadala,” akasema.



Sunday, June 29, 2014

KUFUNGA NI NINI? (MATHAYO 17:14-21)

Bishop Zacharia Kakobe
Katika MATHAYO 17:14-21, tunajifunza juu ya nguvu ya kufunga. Yako mambo ambayo hayawezekani kama kuomba hakuoanishwi na kufunga. Ni kwa sababu hii basi, tunachukua uzito mkubwa kujifunza kwa undani kuhusu kufunga katika mfululizo wa masomo yanayohusu jambo hili kuanzia leo. Tutaliangalia somo la leo katika vipengele vinne:-


(1) MAANA YA KUFUNGA; (2) UMUHIMU WA KUFUNGA; (3) MIFANO YA WATAKATIFU WALIOKUWA WANAFUNGA;
(4) JINSI KUFUNGA KUNAVYOBADILISHA MAMBO.



(1) MAANA YA KUFUNGA Neno “KUFUNGA“ linatokana na neno la Kiyunani “NESTEVO“, ambalo nalo linatokana na maneno mawili ya Kiyunani “NE“ na “ESTHIO“. Neno “NE“ maana yake “BILA“ au “HAPANA“, Kiingereza “NO“ au “WITHOUT“. Neno “ESTHIO“ maana yake “KULA CHAKULA AU KINYWAJI“, Kiingereza “TO EAT SOLID OR LIQUID FOOD“. Neno “NESTEVO” sasa linaunga maneno hayo mawili ya Kiyunani ”NE” na “ESTHIO”, na lina maana “BILA KULA CHAKULA AU KINYWAJI CHOCHOTE”. Hivyo maana ya kufunga, ni “BILA KULA CHAKULA AU KINYWAJI CHOCHOTE”. Kufunga siyo kuacha kusoma gazeti ulilozoea, kuacha kuchana nywele n.k., ni kuacha kabisa kula au kunywa kinywaji chochote. Maana hii ya kufunga, inathibitishwa na maandiko yafuatayo:- EZRA 10:6; YONA 3:7; 2 SAMWELI 3:35; ESTA 4:16; KUMBUKUMBU LA TORATI 9:9; MATENDO 9:9. Kufunga siyo kuacha kula vyakula kama ugali au wali halafu ukawa unakunywa soda, maziwa, uji au kula matunda n.k. Ni kuacha kula chochote wala kunywa chochote kile. Andiko linalotumika kuhalalisha kula vitu vidogo vidogo ni DANIELI 10:2-3. Katika andiko hili “SIKULA CHAKULA KITAMU”, chakula kitamu ni “DESSERTS” kwa Kiingereza au “PUDDING” – ndizi, nanasi, papai, machungwa n.k. Katika mistari hiyo Danieli anasema hakula lolote kabisa.

 (2) UMUHIMU WA KUFUNGA (MATHAYO 6:16-18)
           Yesu Kristo anamtazamia kila mtu aliyeokoka kuwa na maisha ya kufunga pale anapotuambia “TENA MFUNGAPO“, “BALI WEWE UFUNGAPO“. Kwa jinsi hiyohiyo Yesu anamtazamia kila mtu aliyeokoka kuwa na maisha ya kuomba pale anapotuambia, “TENA MSALIPO“, “BALI WEWE USALIPO (UOMBAPO)“ – MATHAYO 6:5-6. Katika mistari hii tunajifunza kwamba Mungu HUWAJAZI wale wafungao, maana yake HUWAPA THAWABU AU ZAWADI au HUWAJAZA PALE WALIPOPUNGUA.


 (3) MIFANO YA WATAKATIFU WALIOKUWA WANAFUNGA
1. YESU KRISTO – Yesu Kristo baada ya kujaa Roho Mtakatifu, alifunga siku arobaini na baada ya mfungo huo alirudi kwa “NGUVU ZA ROHO“ (LUKA 4:1,14);
2. MUSA – (KUTOKA 34:28); 3. EZRA – (EZRA 10:6); 4. ELIYA – (1 WAFALME 19:8); 5. DAUDI – (ZABURI 109:24); 6. PAULO – (MATENDO 9:8-9; 2 WAKORINTHO 11:27); 7. PAULO NA BARNABA (MATENDO YA MITUME 14:23); 8. KANISA LA KWANZA (MATENDO YA MITUME 13:1-3). Ikiwa watakatifu wengi walifunga katika maisha yao, sisi nasi hatuwezi kupuuza kufunga na tukadai kuwa ni wakristo wa Biblia, vile vile kupuuza kufunga, kutasababisha tuwe dhaifu tukilinganishwa na watakatifu wa zamani.

 (4) JINSI KUFUNGA KUNAVYOBADILISHA MAMBO Sehemu nyingi sana katika Biblia, tunaona jinsi ambavyo mambo yalivyobadilika baada ya kufunga na kuomba. Angalia mifano mitano ifuatayo:- 1. Wana wa Israeli walipigwa mfululizo katika vita na wana wa Benyamini. Baada ya kushindwa mfululizo, wakaamua kufunga na kuomba (WAAMUZI 20:20-22, 24-26). Baada ya kufunga na kuomba matokeo yakabadilika, Benyamini wakapigwa sana, na wana wa Israeli wakashinda vita (WAAMUZI 20:34-35, 41-45, 48). Tunaweza kuitia moto miji yote ya Shetani tukiwa wafungaji, na siyo kinyume cha hapo; 2. Ezra hakumtegemea mfalme, bali alifunga, na matokeo ya kufunga yakawa kwamba mkono wa Mungu ulikuwa pamoja naye na yeye na wenzake wakaokolewa na mkono wa adui (EZRA 8:21-28, 31-33). Ikiwa Kanisa linahitaji kuokolewa kutoka katika mkono wa adui, ni lazima liwe na wafungaji. 3. Yehoshafati alipata taarifa za majeshi kombaini ya Maadui waliotaka kumpiga. Akatangaza kufunga na kuomba (2 MAMBO YA NYAKATI 20:1-4), matokeo yake wakashinda vita kirahisi mno kwa sifa tu (2 MAMBO YA NYAKATI 20:22-25). 4. Nehemia alivyopata taarifa za kubomolewa kwa ukuta wa Yerusalemu na malango yaliyoteketezwa kwa moto, alifunga na kuomba (NEHEMIA 1:3-4), na matokeo yake ukuta ulijengwa tena (NEHEMIA 6:15-16). 5. Hasira ya Bwana kwa Kanisa, Taifa, kutokana na uovu wa watu, inaweza kufanywa kuwa AMANI kwa KUFUNGA NA KUOMBA (1 WAFALME 21:27-29; YONA 3:7-10; EZRA 10:6).

 …………………………………………………………………. Mpendwa msomaji, unaona sasa! Hakuna haja ya kusema, “Hivi kweli nitaweza kushinda dhambi duniani? Hivi kweli maisha ya wokovu nitayaweza?” Ni Neema juu ya Neema. Unalotakiwa kufanya ni kutubu dhambi zako tu kwa kumaanisha kuziacha; kwa imani tu, na mengine yanayofuata mwachie Yesu; na leo hii utashangaa kuona maisha yako yamebadilika ghafla na kwa urahisi utaona unaweza kufanya mapenzi ya Mungu, bila jitihada za kibinadamu. Je, uko tayari kutubu dhambi zako? Najua uko tayari. Basi sema hivi, “Mungu wangu, natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha kuanzia leo. Asante kwa neema yako ambayo kwa hiyo tunaokolewa kutokana na kazi aliyoifanya Yesu. Niokoe sasa na kunipa neema ya kufanya mapenzi yako kuanzia sasa na wakati wote ujao. Asante kwa kuniokoa katika Jina la Yesu. Amen”. Ili uzidi kuukulia wokovu ulioupokea leo, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!!


. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
            Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook, Twitter, n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.


Mtumishi wa Bwana Bishop Zakaria Kakobe.
Imechapishwa na Mchimba Riziki Media
Imehaririwa na Mathayo Tajiri Ngotee 

Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score