Thursday, October 31, 2013

Kitengo cha kupambana na ujangili Tanzania chatuhumiwa kwa kukiuka haki za binadamu

Kampeni ya kupambana na ujangili Tanzania
imeingia matatani baada ya tuhuma za ukiukaji
wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na
kuteka nyara na kuua mwanamke, gazeti la The
Citizen la Tanzania liliarifu hapo Jumatano
(tarehe 30 Oktoba).

Kitengo cha kupambana na ujangili,
kinachojumuisha polisi, jeshi na maafisa wa
kiintelijensia, kilidaiwa kumtia kizuizini Emaliana
Gasper Maro, mwenye umri wa miaka 46, siku
kadhaa baada ya kumkamata mume wake Elias
Kibuga, mwenye umri wa miaka 56. Kibuga
amekuwa haonekani tangu alipochukuliwa kwa
ajili ya kuhojiwa, lakini mwili wa Muro
ulionekana katika mochuari ya Hospitali ya
Mirara.
Watu wengine wengi wanaripotiwa kutoonekana,
na maafisa pia wanashukiwa kwa kuwachomea
moto nyumba zao.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara Akili
Mpwapwa alithibitisha ripoti hizo na kusema
uchunguzi ulikuwa unaendelea.
Joseph ole Parsambei wa Jukwaa la Wachungaji
Tanzania alisema kwamba kitengo cha
kupambana na ujangili pia kilikuwa
kinawashikilia wachungaji 27 na mifugo 2,169.
"Tutakwenda mahakamani kuzuia zoezi hili ikiwa
ukiukwaji wa haki za binadamu utaendelea,"
alisema.
Waziri wa Maliasili na Utalii Khamis Kagasheki,
ambaye aliripotiwa kuanzisha kampeni ya
kupambana na ujangili, alikataa kutoa maoni
yoyote.

12 wafa wakati basi ilipogongana na treni Nairobi

Watu 12 walikufa na wengine kadhaa kujeruhiwa
baada ya treni ya abiria kuligonga basi kwenye
makutano ya reli jijini Nairobi siku ya Jumatano
(tarehe 30 Oktoba), walisema maafisa wa polisi.

Ajali hiyo ilitokea kwenye wilaya ya Eastlands,
Nairobi, wakati barabara zikiwa zimejaa watu
katika kipindi cha pilika pilika  nyingi za magari
asubuhi, alisema kamanda wa polisi wa eneo
hilo, Benjamin Nyamae, kwa mujibu wa shirika
la habari la AFP.
"Basi hilo lilipita mstari wakati treni likija kwa
kasi kubwa," alisema Mkuu wa Polisi wa Nairobi,
Benson Kibui.
Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilisema
abiria 34 walijeruhiwa na kupelekwa kwenye
Hospitali ya Mama Lucy kwa ajili ya matibabu na
17 wako kwenye Hospitali ya Taifa ya Kenyatta
kwa ajili ya matibabu maalum. Wengine wawili
wanatibiwa kwenye Hospitali ya MP Shah, kwa
mujibu wa gazeti la Daily Nation la Kenya.
"Tutafanya uchunguzi wetu kamili kwa
kushirikiana na polisi ili kujua kipi hasa
kimetokea," alisema mkuu wa kampuni ya Rift
Valley Railways, Darlan David. "Hata hivyo,
popote palipo na alama ya kukata njia, kanuni ni
kwamba magari yote husimama kupisha treni
inayokaribia kufika."
Dereva wa basi hilo, Edward Githae Wanjau,
mwenye umri wa miaka 43, yuko mikononi mwa
polisi na "atafikishwa mahakamani na
kushitakiwa kwa kusababisha vifo vya watu 12
na kujeruhi wengine kadhaa kwa kuendesha gari
katika hali ya hatari," alisema Mkuu wa Polisi,
David Kimaiyo, kupitia mtandao wa Twitter.

Wednesday, October 30, 2013

Maofisa wa Somalia wasifu shambulio la Marekani dhidi ya mtengenezaji bomu wa ngazi ya juu wa al- Shabaab

Msemaji wa waziri mkuu wa Somalia Ridwan
Haji Abdiwali alisema serikali ya Somalia ilikuwa
na taarifa kuhusu mipango ya Marekani
kumshambulia mtendaji mwandamizi wa al-
Shabaab Ibrahim Ali Abdi, ambaye pia
alijulikana kama Anta Anta, katika kijiji cha
Dhaytubaako.
"Tulifanya kazi kwa kushirikiana na serikali ya
Marekani kufanya aina hizi za mashambulio,
kama tunavyofanya na yeyote yule [anayejaribu]
kuondoa kikundi hiki cha ugaidi,"
Anta Anta alihusika na misheni za kujitoa
mhanga za al-Shabaab na kuwa tishio kwa
umma, alisema Abdiwali, akiongezea kwamba
operesheni hiyo ilikuwa ni mafanikio kwa serikali
ya Somalia na watu wake.
"Tuna furaha [kuhusu matokeo ya shambulio
hilo] na tunayakaribisha," alisema. "Tuna
matumaini ya kuwazuia [watendaji] wengine
kama huyo."
Anta Anta anasemekana kujulikana vizuri kwa
kutengeneza fulana za milipuko na kutayarisha
mabomu ya kwenye magari yanayotumiwa mara
kwa mara na al-Shabaab.
Wakaazi waliokuwa karibu na eneo la
mashambulio waliripoti kuwa watu wapatao
watatu walikuwa kwenye magari yaliyoungua,
ambayo yalilipuka kwa moto muda mfupi baada
ya sauti ya ndege kusikika hewani, kwa mujibu
wa AFP.
Mashambulio ya ndege isiyo na rubani yalifuatia
operesheni nyingine ya Marekani ya mapema
mwezi huu, wakati kitengo cha wataalamu cha
makamanda wa Marekani kilipokuja kwenye
ufukwe wa mji wa Somalia ya kusini wa Barawe
katika jaribio la kumkamata Abdulkadir
Mohamed Abdulkadir "Ikrima" , Mkenya mwenye
asili ya Somalia na anayedaiwa kuwa kamanda
wa al-Shabaab wa wapiganaji wa nje.
Operesheni zote za Marekani zimekuja baada ya
uzingiraji wa siku nne wa al-Shabaab wa kituo
cha maduka ya biashara cha Westgate cha
Nairobi mwezi Septemba ambapo watu wapatao
67 waliuawa.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Somalia
Abdikarin Hussein Guled aliiambia Redio
Mogadishu kwamba shirika la upelelezi la nchi
yake limekuwa likimfuatilia Anta Anta kwa muda
fulani.
"Operesheni ambayo mtu huyu aliuawa ilikuwa
muhimu sana kwa serikali," alisema Guled. "Mtu
huyu alikuwa na dhima kubwa katika vifo vya
raia wengi wasiokuwa na hatia na kifo chake
kitasaidia kurejesha amani."
Kushirikiana na wabia wa kimataifa
Mbunge wa zamani Mohamud Weheliye Waqaa,
ambaye alitumikia katika Serikali ya Mpito ya
Shirikisho, alisema mashambulizi ya ndege
zisizokuwa na rubani ni njia nzuri ya
kuunganisha mafanikio ya usalama wa Somalia
na kuiunga mkono serikali ya Somalia.
"Serikali ya Somalia inapaswa kushirikiana
taarifa na [wabia] wanaofanya mashambulizi
hayo ili kuwatoa magaidi,"
Kwa kuzingatia ukweli kwamba jeshi la Somalia
bado halijafanikisha uwezo wa kiufundi kufanya
operesheni hizo, alisema, ni muhimu kwamba
jeshi la Somalia lifanye kazi kwa kushirikiana na
wabia wa kimataifa wakikusanya taarifa katika
maeneo huku wakiomba msaada wa kufanya
aina hizi za mashambulizi inapohitajika.
Hata hivyo, mbunge Mohamed Abdi Yusuf
alisema utawala wa Rais Hassan Sheikh
Mohamud haukupaswa kuidhinisha
mashambulizi hayo bila kushauriana kwanza na
bunge.
"Ubia kama huu unaohusisha ushirikiano kati ya
utawala na nchi za kigeni unapaswa
kuwasilishwa [kwa ajili ya mjadala] bungeni,"
Alisema mapambano yanaweza kusababisha
madhara ambayo hayakukusudiwa kama vile
vifo vya raia, hivyo makubaliano ya wazi
yanapaswa kufikiwa kabla ya kuanza.
Kuimarisha uwezo wa kiintelijensia
Wananchi wa Somalia pia wana maoni
mbalimbali kuhusiana na operesheni hiyo.
Sado Dahir, mwenye umri wa miaka 26
mwanafunzi wa sayansi ya jamii katika Chuo
Kikuu cha Somalia, alisema mashambulizi ya
kutumia ndege zisizokuwa na rubani yalikuwa
ushindi kwa umma wa Somalia.
"Kwanza, hii ni mara ya kwanza kabisa kumsikia
mtu mwenye jina hili, na mwanzo nilidhani
kwamba hakuwa maarufu sana ndani ya al-
Shabaab. Hata hivyo, niliposikia kwamba
alihusika katika kufanya milipuko, nilitambua
jinsi alivyokuwa hatari katika umma," "Hii ni operesheni nzuri sana ambayo
ilifanyika kwa mafanikio na ninaipongeza."
Dahir pia alisema ilikuwa ni muhimu kwa serikali
ya Somalia kuimarisha uwezo wake wa
kiintelijensia.
"Uimarishaji pekee hautafanikisha jambo lolote.
Kila shambulio lililofanyika dhidi ya al-Shabaab
linapaswa kuwa lililopangwa kwa makini ili
lifanikiwe kama hili, na serikali inapaswa
kufanya kazi na serikali zote duniani kuhusu
kuimarisha kitengo chake cha intelijensia,"
alisema.
Lakini Mohamed Jimale, mwenye umri wa miaka
57, alisema ingekuwa afadhali
kumkamata Anta Anta badala ya kumuua.
"Kama serikali ya Somalia na Marekani ilijua
kuhusu anakopatikana mtu huyu anayeitwa Anta
Anta ambaye ni mwanachama wa al-Shabaab,
ninadhani ingekuwa vizuri zaidi kumkamata ili
aweze kuhojiwa na kupata taarifa zaidi, kwani
yeye siye kiongozi hatari peke yake wa al-
Shabaab," alisema. "Hata hivyo, ninaunga
mkono jitihada za kupambana na kila kitu
ambacho kinaleta tishio katika umma."

By Mchimba Riziki


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score