Friday, January 3, 2014

AMRI JESHI MKUU AMWAPISHA IGP MANGU IKULU

Kamishna wa Polisi, Ernest Mangu,

Juzi, Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete,
alimwapisha Ernest Mangu kuwa Inspekta
Jenerali wa Polisi (IGP) akichukua nafasi
iliyoachwa na Said Mwema ambaye amestaafu
kwa mujibu wa sheria.

Mbali na Mangu, Rais pia alimwapisha
Abdulrahman Kaniki kuwa Naibu Inspekta
Jenerali wa Polisi, cheo kipya katika mfumo
wa jeshi hilo.

Tunapenda kuwapongeza
makamanda hao wawili kwa uteuzi huo, pia
kumtakia heri ya kustaafu, Mwema.

Hata hivyo, pamoja na pongezi hizo,
tunaamini kwamba wanazifahamu vyema
changamoto zinazowakabili katika kutimiza
majukumu yao hasa ikizingatiwa kwamba
‘wamekulia’ ndani ya jeshi hilo.

Mara baada ya kuapishwa, Mangu alikaririwa
na vyombo vya habari akisema kwamba
ataanza kazi kwa kupambana na uhalifu wa
aina zote pamoja na ajali za barabarani.

Kimsingi hayo ndiyo masuala makubwa
ambayo jeshi hilo lililo na wajibu wa kulinda
raia na mali zao linapaswa kuyasimamia.

Akilihutubia Taifa juzi usiku, Rais Kikwete
alisema Jeshi la Polisi limeendelea kupambana
na ujambazi wa kutumia silaha na mafanikio
yameendelea kupatikana na kusema kwamba
matukio ya ujambazi yalipungua mwaka 2013
ikilinganishwa na mwaka 2012.

Alisema mwaka 2012 matukio ya ujambazi
yaliyoripotiwa yalikuwa 6,872 na kwa mwaka
2013 yalikuwa 6,409. Tunasema upungufu huo
ni mdogo na tunaamini kwamba hiyo ndiyo
changamoto kubwa inayomkabili Mangu na
Kaniki katika kuwahakikishia wananchi
usalama wao.

Tunasema hivyo kwa kurejea kauli ya Rais
katika hotuba yake hiyo kwa Taifa juzi
kwamba Julai mwaka jana, aliamua
kulihusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), katika kupambana na
ujambazi wa kutumia silaha na utekaji wa
magari katika Mikoa ya Geita, Kagera na
Kigoma.

Tunadhani kwamba ipo haja sasa kwa Serikali
kuliwezesha jeshi hilo kushika hatamu za
usalama wa ndani ya nchi na kuwafanya
wananchi watekeleze majukumu yao ya kila
siku.

IGP Mangu pia aligusia suala la usalama
barabarani. Hakuna ubishi kwamba ajali za
barabarani zimekuwa na mchango mkubwa
katika kuongeza idadi ya vifo na ulemavu
kwa wananchi.

Katika hili, moja ya sababu kubwa za
kuendelea kutokea kwa ajali katika mtindo
unaofanana ni kutozingatiwa kwa Sheria za
Usalama Barabarani, pia kutosimamiwa vyema
na waliopewa dhamana.
Tunaamini kwamba kwa kuwa IGP Mangu
ameliona hilo, tutaona jitihada zaidi
zikiwekwa katika kuzuia ajali badala ya
kusubiri zitokee ndipo hatua za zimamoto
zichukuliwe.

Katika hilo la ajali za
barabarani, IGP Mangu anapaswa kutafuta
mwarobaini wa kudhibiti ajali zinatokana na
uendeshaji wa pikipiki za biashara maarufu
kama bodaboda.

Licha usafiri huu kuwa mkombozi kwa
wananchi hasa wa kipato cha chini,
umekuwa janga kubwa kutokana na kuongeza
idadi ya vifo vinavyotokana na ajali za
barabarani na ulemavu.

Source Mwananchi

Share by Mchimba Riziki

Mashambulizi mengine Mombasa yajeruhi 10

Mashambulizi mengine Mombasa yajeruhi 10

Nchini Kenya watu 10
wamejeruhiwa wakati
washambuliaji waliporusha
guruneti ndani ya mkahawa
mmoja katika mji wa pwani
wa Mombasa na kuzusha
hofu ya usalama katika
eneo hilo tete.

Mkuu wa polisi mjini Diani,
Jack Ekakuro, amesema
washambuliaji hao
waliilenga baa moja iitwayo
Tandoor mjini Diani
mapema leo, wakati
ilipokuwa bado imefurika
watu waliokuwa
wakiendelea kusherehekea
mwaka mpya.

Hii ni
sehemu ya mlolongo wa
mashambulizi, ikiwa ni
pamoja na lile la bomu
kwenye basi moja katika
mtaa wa Eastleigh mjini
Nairobi mwezi uliopita, hali
inayowatia wasiwasi
Wakenya wengi.

Mchimba Riziki

Tuesday, December 31, 2013

BAADA YA OPARESHINI YA TOKOMEZA MAJANGILI KUSITISHWA, VIFO ZA TEMBO VYAONGEZEKA ZAIDI TANZANIA

Kiasi cha tembo 60 wameuawa nchini Tanzania
ndani ya miezi miezi tangu serikali
ilipolazimishwa kusitisha operesheni yenye utata
ya kupambana na ujangili, alisema Naibu Waziri
wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalangu siku ya
Jumapili (tarehe 29 Disemba).

Rais Jakaya Kikwete aliwafukuza kazi mawaziri
wanne mwezi huu kukiwa na tuhuma kwamba
operesheni hiyo ya nchi hiyo dhidi ya ujangili
ilipelekea vikosi vya usalama kufanya matendo
kadhaa yaliyovunja haki za binadamu ikiwemo
kuwauwa washukiwa, mateso na ubakaji.

Lakini Nyalandu alisema angalau operesheni
hiyo ilikuwa imepelekea kupungua kidogo kwa
ujangili. Chini ya operesheni hiyo ya kupambana
na ujangili, vikosi vya usalama vilifanya kazi kwa
sera ya "kupiga risasi na kuua" na kukamata
watu wengi.

"Ndani ya kipindi chote cha operesheni, tembo
wawili tu waliripotiwa kuuawa ambapo sasa
tembo 60 walichinjwa kati ya tarehe 1 Novemba
na 28 Disemba," alisema Nyalandu kwa mujibu
wa shirika la habari la AFP.

Alisema sasa Tanzania itaziomba serikali na
taasisi za mataifa mengine kwa msaada wa
namna gani ya kuendelea nayo.
"Wale watakaoombwa ni pamoja na Umoja wa
Ulaya na nchi za Asia.

Nchi za Asia zinaripotiwa
kuwa watumiaji wakubwa wa pembe za ndovu
na mambo yanatokanayo nazo," alisema
Nyalandu, akiongeza kwamba idara ya
wanyamapori ya Tanzania na shirika la ulinzi wa
wanyama hao vinapaswa kuimarishwa.

Mchimba Riziki


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score