Friday, December 5, 2014

2017 Haitafika Bila Taji "Arsen Wenger" Anena

Kocha wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger ana imani anaweza kuongoza vijana wake kunyakua taji la ligi kuu kabla ya kandarasi yake kuisha mwishoni wa msimu wa 2016/17.

Arsen Wenger

Imani yake ya msimu huu ilipigwa jeki hata zaidi na ushindi wao mwembamba wa 1-0 dhidi ya Southampton Jumatano usiku na hivyo kuzidi kumpa moyo licha ya kuwa wangali katika nafasi ya sita kwa alama 23, ikiwa ni pointi 16 nyuma ya viongozi Chelsea.

Timu hiyo imeandikisha mwanzo wao mbaya zaidi katika ligi ya EPL tangu 1982 na wamejikuta nyuma mno kwa pengo hilo kubwa la alama ikilinganishwa na muhula uliopita ambapo hadi kufikia wakati huu walikuwa uongozini kabla ya kufifia kufikia mwisho wa kampeni na kunusurika kwa kumaliza wa nne.
“Kuna ushindani mkubwa Uingereza na Chelsea wameanza vyema, hilo tunakubali. Itakuwa vigumu kuwafikia lakini kila mmoja atapigania kuwalaza sisi pia tukiwemo. Huwezi kusema kuwa harakati za kuwania taji zimekwisha baada ya mechi 14 pekee tulizocheza hadi kufikia sasa,” Wenger akasema.
“Hatukuanza vyema msimu huu ila usisahau kwamba hatukuwa na kikosi chote pamoja tangu musimu kuanza kwani ulifuatia Kombe la Dunia. Ni lazima tupambane  ili kurudia uwaniaji wa taji kwa haraka katika kila mechi,” akajitetea.

Licha ya yote, Wenger anaonekana kuwa kakalia kuti kavu baada ya mashabiki kuanza kumshurutisha aondoke kama ilivyoshuhudiwa wikendi iliyopita kwenye ushindi wao wa 1-0 dhidi ya West Brom.

Kesi Ya Uhuru Kenyatta Imetupiliwa Mbali.

Wakenya Wakionyesha Furaha Baada Ya Uhuru Kufutiwa Kesi
Habari zilizofika mapema hivi leo zinasema mwendesha mashitaka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC Fatou Bensouda, ametupilia mbali mashitaka dhidi ya Rais wa Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Mapema wiki hii mahakama ya kimataifa ya uhalifu  ICC ilimpa wiki moja mwendesha mashitaka huyo kuongeza  kasi ya uchunguzi ama kuyatupilia mbali mashitaka dhidi ya Rais Kenyatta.
Mh.Uhuru Kenyatta
Kesi hiyo iliahirishwa mara kadhaa na mahakama hiyo ya The Hague, na Jumatano ilisema kwamba kuchelewa zaidi kungeweza kuwa kinyume na maslahi ya haki katika mazingira yaliyokuwepo.
Rais Kenyatta alikabiliwa na mashitaka dhidi ya ubinadamu akishutumiwa kupanga ghasia za  baada ya uchaguzi mwishoni mwa mwaka 2007 na mapema 2008. Ghasia hizo zilisababisha vifo vya watu 1,100 huko Kenya na kuwakosesha makazi wengine zaidi ya nusu milioni.
Rais Kenyatta mara kadhaa amesema yeye hana hatia.


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score