Saturday, January 18, 2014

TANZANIA: WILAYA MPYA 31 ZENYE MADINI

Dar es Salaam.Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema, tathimini iliyofanywa na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) imebaini kuwapo kwa madini ya aina mbalimbali katika wilaya 31 nchini.
Profesa Muhongo alisema jana kuwa, kubainika kuwapo kwa madini hayo kutachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa pato la taifa na malengo ya milenia ya nchi ifikapo mwaka 2025 yatafikiwa pasi na shaka.
Alisema katika bajeti ya mwaka huu, wametenga Sh6.3 bilioni ambazo zitakuwa chini ya Shirika la Madini Tanzania (Stamico) ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zao.
Alisema malengo ya Serikali kwa Sekta ya Madini kufikia mwaka 2025 ni ichangie asiliamia 10 ya pato la taifa ambapo sasa inachangia kwa asiliamia 3.3.
“Tunataka kufikia mwaka 2025 sekta ya madini ichangie zaidi ya asiliamia 10 katika pato la taifa, kubainika kwa madini katika wilaya hizo kutachangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla,” alisema Profesa Muhongo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa GST, Profesa Abdulkarim Mruma alisema, nchi ikiwa na migodi mingi sehemu mbalimbali kutasaidia pia maendeleo ya mtu mmoja mmoja.
“Bila shaka pato la taifa nalo litaongezeka, wananchi watakuwa na fursa ya kutumia machimbo hayo kuboresha maisha yao na hiyo itafanikiwa ikiwa mipango ya Serikali ya kuwapa kipaumbele wachimbaji wadogo itafanyika,” alisema.
Baadhi ya wilaya ambazo zimebainika kuwa na madini hayo ni Igunga, Arumeru, Babati, Iramba, Kilosa, Manyara, Bagamoyo, Gairo, Nchemba, Chamwino, Handeni,Kiteto, Kongwa, Mbalali, Ikungi, Manyoni na Mbozi.
Mchimba riziki

Friday, January 17, 2014

Maajabu Ya 2014: Wezi Wavamia Gereza Na Kuiba Mbuzi 43

MAAFISA wa ulinzi katika gereza la Kilifi mjini usiku wa alhamisi walilazimika kufyatua risasi
hewani baada ya wezi kuvamia gereza hilo na kuiba mbuzi 43 wanaofugwa katika gereza hilo.
Kiza hicho cha kufyatua risasi hewani kilileta wasiwasi mkubwa miongoni mwa wakazi wa Kilifi
ambao walidhania kulikuwa na jambo hatari zaidi mjini Kilifi.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, afisa mkuu wa polisi mjini Kilifi Justine Nyaga alisema wezi hao
ambao idadi yao haikubainika walivamia jela hilo mwendo wa saa
saba usiku na kuanza kuiba mbuzi hao.
Hata hivyo afisa wa magereza ambaye alikuwa kazini alipuliza kipenga cha kuashiria hatari ndipo wengine wakaanza kufyatua risasi hewani kuwakimbiza wezi hao.
“Ulikuwa ni mwendo wa saa saba usiku ambapo wakora ambao walikuwa ni zaidi ya watatu walipofika katika gereza hilo na kupenya kabla ya kuanza kuwatorosha mbuzi hao mali ya
gereza hilo.
Hata hivyo afisa wa magereza ambaye alikuwa kazini aliwaona na akapiga kipenga cha kuashiria hatari. Ni hapo ambapo maafisa wengine walianza kufyatua risasi hewani na wezi wakatoroka,” akasema.
Aidha Nyaga alisema kuwa mbuzi wote 43 walipatikana huku wezi hao wakitoroka na bado polisi wanawasaka.
“Tumepata mbuzi wote. Walikuwa hawajafika mbali na baada ya maafisa wa gereza kuanza kufyatua risasi, wezi walitoroka na kuacha mbuzi hao karibu na jela hiyo.Wote 43 ambaowalikuwa wamelengwa na wezi hao wamepatikana,” akasema.
Wakati huo huo, Nyaga alisema kuwa wanachunguza ripoti kwamba kuna soko la siri mjini Kilifi ambapo mbuzi wanaoibwa huuzwa na kisha kusafirishwa hadi maeneo mengine
kuchinjwa ama kuuzwa.
Soko
“Tunajaribu kuchunguza kwa kina tuone hasa jambo hili lilikuwa vipi. Tuko na habari kwamba kuna soko la siri ambapo mbuzi na mifugo
wengine wanaoibwa hupelekwa hapo na kisha baadaye wanunuzi wa siri hufika na kufanya biashara hapo.
Tunataka kuwahakikishia wakazi
wa Kilifi kwamba tuko macho kukabiliana na wezi na wakora ambao watakuwa wakihangaisha
raia wema katika eneo hili,”akasema.
Kufyatuliwa huko kwa risasi na maafisa wa magereza kulizua hofu kuu miongoni mwa wakazi wa Kilifi ambao walidhani maafisa wa polisi walikuwa wakikabiliana na majambazi hatari.
Kulingana na Karisa Charo ambaye ni mwendeshaji piki piki ya boda boda alilazimika 'kutoroka mbio na kujificha baada ya milio hiyo
ya risasi kusikika mfululizo.
“Mazee, nilishutka sana. Mimi hukesha nikiendesha biashara hii lakini punde tu baada
ya mlio wa kwanza, kisha ikafuata mengine ghafla, hata nilivyopeleka pikipiki sikufahamu, nilijikuta eneo la mbali ghafla. Ilikuwa inatisha
sana,” akasema.
Maafisa wa polisi wanaendelea na uchunguzi pia kubaini kiini cha wizi huo katika gereza hilo ambalo daima huwa na ulinzi mkali.
Mchimba Riziki

Makundi Kuipasua CCM Viongozi Wahaha.

Makundi ya Urais wa 2015
yanaendelea kuivuruga CCM baada ya Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Singida, Mgana Msindai kuibuka na kusema atamburuta mahakamani Mwenyekiti mwenzake wa Mkoa wa Geita, Joseph Kasheku ‘Msukuma’ asipomwomba radhi kwa
kumchafua kwa kumwita mpuuzi.
Hata hivyo, Kasheku amesema Msindai anaweza kwenda mahakamani huku akisisitiza kwamba hawezi kumwomba radhi
kwa kuwa anaamini kwamba alichofanya ni kinyume cha taratibu za chama na vikao.
Juzi, Kasheku alimponda Msindai mbele ya waandishi wa habari kwa kitendo chake cha kusema kuwa wenyeviti wa CCM wa mikoa yote ya Tanzania wanamuunga mkono, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika safari yake ya urais wa 2015 wakati wa sherehe ya mwaka mpya huko Monduli, Arusha.
Msindai alisema jana kuwa amemtaka Kasheku aitishe mkutano wa waandishi wa habari na kumwomba radhi.
“Asipofanya hivyo ndani ya siku saba nitampeleka mahakamani,” alisema Msindai.
Msindai pia alikanusha kuwa aliwekwa kitimoto katika mkutano wa wenyeviti wa CCM wa mikoa uliofanyika Zanzibar.
Msindai aliyekuwa Mbunge wa Iramba Mashariki kwa miaka 15, alikiri kuwa alialikwa pamoja na wenyeviti wenzake sita katika sherehe ya mwaka mpya iliyoandaliwa na Lowassa huko Monduli.
Katika sherehe hizo, Lowassa alitangaza kuwa ameanza safari ya matumaini, kauli ambayo wachambuzi wa masuala ya kisiasa
waliitafsiri kama tangazo la kuwania urais mwaka 2015.
Msindai alikanusha kutangaza kuwa
wenyeviti wote wa CCM wa mikoa
wanamuunga mkono Lowassa wakati wa sherehe hiyo... “Mimi ni Mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM, lakini sikuwahi kuzungumza kuwa wenyeviti wote wanamuunga mkono Lowassa katika Uchaguzi
Mkuu 2015... kikubwa tulichozungumza ni kumuunga mkono katika safari yake ya
mafanikio katika kuendeleza elimu, maji, ujenzi wa zahanati.”
Msindai alisema wanamwangalia Lowassa kutokana na uwezo wake katika kusimamia mipango yake ya maendeleo na zaidi katika kupigania elimu pana kwa Watanzania.
“Alipokuwa Wizara ya Maji alichangia maji kupatikana Dar es Salaam na mikoani na maendeleo mengi, uwajibikaji kwenye jimbo
lake na aendelee hivyo...hayo ndiyo
tuliyomsifia. Nilizungumza haya na
sitabadilika,” alisema Msindai, ambaye alisema haogopi kufukuzwa.
“Mimi si mpya ndani ya CCM kama
‘Msukuma’. Nina miaka zaidi ya 40,
ninaelewa taratibu zote za chama za udiwani, ubunge na urais.
Kama ni kampeni ni baada ya chama kumpitisha mtu na sisi tutamuunga mkono... hata mimi ninaweza kuwania urais,” alisema.
Siombi radhi
Mchimba Riziki

Thursday, January 16, 2014

Mkurugenzi Atimuliwa Na Madiwani Arusha


BARAZA la Madiwani wa halmashauri ya jiji la Arusha,limemtimua Mkurugenzi wa jiji hilo, Nd. Sipora Liana na wakuu wake wa idara, katika  kikao cha madiwani baada ya kumpigia kura,wakidai Mkurugenzi huyo amezidi kuwadharau na kuwakejeli.

Hali hiyo ilijiri mapema jana wakati madiwani hao walipochachamaa ndani ya kikao wakidai hawawezi kujadili mada yoyote hadi wapate ufafanuzi juu ya dharau wanazodai zinafanywa na Mkurugenzi huyo kwa madiwani.
Naibu Meya, Nd. Prosper Msofe, aliyekuwa akiongoza kikao hicho aliamuru kupigwa kura za kumjadili Mkurugenzi baada ya kutolewa hoja kutoka kwa diwani wa Sekei, Nd. Crisipin Tarimo, kutaka baraza hilo lijigeuze kamati kumjadili Mkurugenzi.

Hoja hiyo ilipokewa na Mwenyekiti wa kikao hicho na aliamuru baraza hilo kujigeuza kamati baada ya nusu ya wajumbe kuunga mkono hoja hiyo ambapo kwa pamoja walimtaka Mkurugenizi na wakuu wake wa idara watoke nje ya ukumbi.Madiwani hao wakiwa kama kamati walianza kumjadili Mkurugeninzi huyo huku kila mmoja akitupa lawama juu yake wakidai wamechoshwa kudharauliwa ikiwemo kutofanyiwa kazi kwa maazimio wanayoyapitisha.

Awali diwani wa viti maalumu kupitia  CCM, Nd. Belinda Kabuje alisema hawataweza kufanya kazi na Mkurugenzi mwenye dharau dhidi ya madiwani na kwamba madiwani palei wanapomfuata ofisini kwa ajili ya kueleza kero zao anawajibu kwa nyodo na dharau kubwa.

“Huyu Mkurugenzi ana dharau sana, ni mwanamke kama mimi lakini amekuwa na dharau utazani si mwanamke ,hatuwezi kukubali kufanya kazi na mtu wa namna hii,” alisema.

Baada ya kamati hiyo kumalizika, Naibu Meya alisema kikao hicho kilikuwa kizito na kwamba makubaliano yaliyotoka katika kamati hiyo ni kwamba madiwani wataandika maoni dhidi ya tuhuma za Mkurugenzi na yatapelekwa kwa mkuu wa mkoa kwa ajili ya kuitisha kikao na kutoa ufafanuzi wa jambo hilo.

Akizungumzia hali hiyo Mkurugenzi, Nd. Sipora Liana aliwashangaa madiwani hao kwa kujigeuza kamati kwa lengo la kumjadili na kueleza kwamba,madiwani hao hawana ubavu wa kumjadili yeye.

Mchimba Riziki

Nasri wiki 8 Nje kutokana na majeraha

KOCHA wa Manchester City, Manuel
Pellegrini amesema timu yake itakosahuduma ya kiungo matata Samir Nasri.
Nasri atakuwa nje kwa wiki nane baada ya kuumia mshipa wa mguu katika goti lake la kushoto kutokana na rafu mbaya aliyochezewa na Mapou Yanga-Mbiwa wakati City ilipoizamisha Newcastle 2-0, Jumapili.
Mfaransa huyo amekuwa muhimu katika kikosi cha City ambayo kimecheza mechi 10 bila kupoteza katika Ligi Kuu ya England na kikiwa pointi moja nyuma ya vinara Arsenal.
Pellegrini ambaye kikosi chake jana kilicheza na Blackburn katika marudiano ya Kombe la FA, alisema Nasri atakumbukwa sana.
“Ni mchezaji muhimu kwetu. Pia alikuwa katika kiwango cha juu kwa sasa, kwa hiyo tuna matumaini atarejea haraka iwezekanavyo,” alisema kocha huyo raia wa
Chile.
“Lakini nafikiri kwamba wiki sita au saba (atakazokuwa nje Nasri) zitakuwa ngumu.”
Kikosi cha City kililazimishwa sare ya bao 1-1 na Blackburn iliyo Daraja la Kwanza na hivyo jana kurudiana kwenye Uwanja wa Etihad.
Pellegrini alizungumzia umuhimu wa Kombe la FA, akisema anataka kushinda kila taji msimu huu.
City hapo jana usiku iliweza kuizamisha Blackburn Rovers kwa magoli tano bila katika kinyaganyiro cha FA.
Magoli hayo yalifungwa na washambuliaji (Negredo 45+1' na 47', E.Dzeko 67' na 79' na Aguero 73').
Mchimba Riziki Michezo

Msigwa wa (CHADEMA) Kunyaganywa Jimbo La Iringa Mjini

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Iringa kimetangaza mpango mkakati wa kulikomboa Jimbo la Uchaguzi la Iringa Mjini.

Mpango huo ulitangazwa katika
mkutano mkubwa, uliofanyika juzi kwenye uwanja wa Mwembetogwa mjini hapa.

Jimbo hilo kwa sasa linaongozwa na
Mchungaji Peter Msigwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyechaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Kwa kupitia mkakati huo, CCM itakuwa ikifanya mikutano ya mara kwa mara katika kata zote 16 za Manispaa ya Iringa.

Lengo la hatua hiyo ni kupokea kero za wananchi na kutoa ufafanuzi wa shughuli za maendeleo, zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na serikali yao.

Mpango huo umebuniwa na Katibu wa CCM Manispaa ya Iringa,Hassana Mtenga ambaye kabla ya kuhamishiwa mjini hapa, alikuwa Katibu wa chama hicho Wilaya ya
Hai mkoani Kilimanjaro.

Mtenga ambaye pia ni Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, alimuagiza Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi wa
CCM kuhakikisha fedha zinazotengwa na halmashauri hiyo kwa ajili ya mikopo ya vijana na wanawake, zinatolewa kwa wakati.

“Wakati mkitoa fedha hizo kwa makundi hayo, wananchi msisahau kumuuliza Mbunge wenu anazitumia vipi fedha za
Mfuko wa Jimbo zinazotolewa na serikali ya CCM kwa ajili ya maendeleo yenu,” alisema
Mtenga huku akishangiliwa.

Agizo lingine alilolitoa kwa madiwani wa Manispaa hiyo, linawataka kuunda Kamati
ya Madiwani wa CCM, watakaofanya kazi ya
kukusanya kero zote zinazowakabili
wananchi wakiwemo vijana wa jimbo hilo.

“Tunaanza kumshughulikia Msigwa kuanzia sasa, hatutalala, tutapita kila mahali na kuwaeleza wananchi kazi zilizofanywa na serikali ya CCM, lakini tutachukua kero zao na kuziingiza katika mipango ya serikali
yetu; lengo la CCM ni kupeleka maendeleo kwa wananchi miaka yote tangu ianze kutawala nchi.

“Nakutahadharisha Mchungaji Msigwa, kiinua mgongo utakachopata kitumie na
familia yako, usirudi Jimbo la Iringa Mjini kwa sababu utapata hasara kubwa,” alisema.

Aliwaomba vijana waache kudandia maneno ya Mbunge huyo, bila kuyatafakari kwa kina kwa sababu yamekuwa yakipingana na mambo anayofanya.

Akinukuu taarifa iliyotolewa na Mchungaji Msigwa katika mkutano wake alioufanya hivi karibuni mjini Iringa, Mtenga alisema;
“anawadanganya wananchi wa Iringa kwamba amepata fedha za kujenga uwanja wa Ndege wa Nduli na mradi wa maji katika Kata ya Nduli, wakati yeye na wabunge
wote wa Chadema huwa wanapinga bajeti ya serikali kila mwaka.

“Muulizeni anapata wapi fedha kwa ajili ya maendeleo ya Iringa, wakati kila awapo bungeni huwa anapinga bajeti ya serikali, ambayo ndio msingi mkuu wa maendeleo
anayoyazungumza,” alisema.

Jumla ya maswali 25 yaliulizwa na kujibiwa na madiwani mbalimbali, waliohudhuria mkutano huo, mojawapo likiwa ni kuhusu
msimamo wa CCM baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupandisha bei ya umeme.

Mtenga alisema wananchi wanatakiwa kuwa wavumilivu, wakati serikali ikiendelea
kujipanga kuongeza uzalishaji wa nishati hiyo kupitia miradi mbalimbali inayoanzishwa, ikiwemo ya gesi asilia.

Wengine waliopata fursa ya kuhutubia mkutano huo ni vijana waliojitoa Chadema na kujiunga CCM, Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya CCM Taifa (NEC), Mahamudu
Madenge, Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM Ritta Kabati, Mwenyekiti wa CCM
Manispaa ya Iringa Abei Kiponza, Meya wa Manispaa ya Iringa na madiwani.

Habari Leo (Chimbuko)
Mchimba riziki

Wednesday, January 15, 2014

ACT-TANZANIA KUISAMBARATISHA CHADEMA

CHAMA kipya cha siasa cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania), ambacho tayari kimeshapata usajili wa muda kinatajwa kuwa ndio tishio la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokana na kuundwa na idadi kubwa ya vigogo wa chama hicho ambacho kwa sasa kimo ndani ya mgogoro mzito na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wao,
Zitto Kabwe.

Taarifa za uhakika zilitufikia kutoka
kwa mmoja wa watu watakaokiongoza chama hicho kipya, kimebainisha kuwa idadi kubwa ya wanachama wa Chadema wanaoheshimika na kukubalika ndani na nje ya chama wamekubali
kwa hiyari zao kuwa ndani ya ACT-Tanzania na kwamba wanasubiri muda ufike ili wajiunge rasmi.

Hatua hiyo imeonesha dalili za wazi za kukimaliza Chadema na kwamba huenda chama hicho kikafika mwaka 2015 kikiwa mahututi kutokana na kuondokewa na wanachama wake wote wenye mvuto.

Mtoa taarifa wetu ameliambia MTANZANIA Jumatano kwamba ACT-Tanzania tayari kina usajili wa muda mkononi na kwamba kinachofanyika sasa ni kuzunguka kwenye mikoa 10 ili kukusanya wanachama 200 watakaokiwezesha kupata usajili wa kudumu.

Lengo la kufanya ziara hizo ni kuhakikishna chama hicho kinatimiza masharti ya usajili ili
kumpa nafasi Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kufanya ukaguzi kabla hakijaendeleza harakati zake.

Taarifa za uhakika zimebainisha kuwa safu ya uongozi wa chama hicho itaundwa na idadi kubwa ya wanachama kutoka Chadema, ambapo Samson Mwigamba anatajwa kuwa Katibu Mkuu, huku Zitto Kabwe akipewa nafasi
ya kuwa Mwenyekiti wakisaidiwa kwa karibu na wanachama mahiri na wasomi kutoka Chadema.

Amesema Zitto atajiunga na chama hicho mara baada ya Bunge la Katiba kumalizika, ambapo kama atavuliwa uanachama atakuwa tayari kujiunga na chama hicho.

Imebainishwa kuwa mkakati wa chama hicho ni kuhakikisha kinakuwa mbadala wa Chadema na
kwamba dhamira yao kubwa ni kuhakikisha wanaendesha siasa zao kwa kutumia demokrasia ya kweli na hawako tayari kukifanya chama hicho kuwa cha watu wachache.

“ACT-Tanzania kitakuwa chama cha wote na ndio maana tutakuwa na wanachama kutoka kila mkoa na tutakuwa tayari kupomkea mwanachama kutoka chama chochote cha siasa, hatuwalengi waliofukuzwa, sisi tunalenga
wanasiasa wote wenye uwezo wa kuendesha siasa safi,”alisema mtoa habari wetu.

Aidha chama hicho katika kujiimarisha hakina mpango wa kuwania urais kwenye uchaguzi
Mkuu ujao na kwamba nia na malengo yao ni kuwa na idadi kubwa ya wabunge na madiwani,
ambapo wanaangalia kama mikakati yao itafanikiwa mwaka huu, watashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Tuna uhakika wa kuchukua majimbo mengi na moja ya majimbo hayo ni lile la Kigoma
Kaskazini, Arusha Mjini na Iringa Mjini, tunauhakika wa kufanya maajabu, tuache muda ufike,”aliongeza.

Kwa mujibu wa mtoa habari wetu alibainisha kuwa chama hicho kwa sasa kipo chini ya vijana wawili na mmoja kati yao ni Leopold Mahona
ambaye aliwahi kugombea ubunge katika Jimbo la Igunga mwaka 2010 kwa tiketi ya Chama cha Wananchi CUF na baadaye kugombea tena
katika uchaguzi mdogo katika jimbo hilo mwaka 2011.

“Mahona akiwa na kijana mwenzake kutoka Zanzibar walianzisha chama hicho kwa nia ya nchi kuwa na chama chenye siasa safi yenye uwazi, bila shaka nia hiyo itafanikiwa,”aliongeza.

Mahona alitafutwa kupitia simu yake ya kiganjani ili kuzungumzia chama hicho, hata hivyo alishangazwa na mwandishi wa habari hii kuwa na taarifa hizo.

Mshangao huo ulimfanya ashindwe kukubali ama kukataa juu ya uwepo wa chama hicho na kumtaka mwandishi wetu kuacha muda useme.

“Kwanza wewe hiyo habari umepata wapi… ‘I have no comment’ tuache muda utasema, lakini ni vema ukawauliza zaidi hao waliokwambia,”alisema Mahona kwa kifupi.

Kuhusu kujua uwepo wa taarifa za kuanzishwakwa chama hicho, alipatwa na kigugumizi zaidi
kwa kujibu kuwa “aaaaaaaa…sijui…
sijui…,”alisema

Alipotafutwa Mwigamba ili kuzungumzia taarifa hizo, ambapo alicheka na kusema kuwa hawezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa na kwamba ni vema likaachwa kwani
kwa upande wake bado hajaamua nini cha kufanya kwenye siasa.
“Natafakari, bado sijajua
nifanyeje, hili tuliache kwanza,”alisema kwa
kifupi.

Alipotafutwa Zitto ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi, hakuweza kupatikana.

Mwigamba na Dk. Kitila Mkumbo walivuliwa uanachama Januari 5 mwaka huu na Kamati Kuu ya Chadema.

Zitto alishindwa kuvuliwa uanachama kutokana na kukimbilia Mahakamani kuweka zuio kwa Kaamati Kuu kutoujadili uanachama wake.

Dk. Kitila, Mwigamba na Zitto wanashutumiwa na uongozi wa juu wa Chadema kuwa ni wasaliti na kwamba wameandaa waraka wa siri
wenye lengo la kufanya mabadiliko ya uongozi ndani ya chama hiyo hali iliyoibua mgogoro
mzito.

Mchimba riziki

Arsenal Yaweka 5bl Kumsajili Van Persie Mpya

VIONGOZI wa Ligi Kuu ya Uingereza, Arsenal
wameyatarisha Sh5 bilioni kumnunua chipukizi
wa Schalke 04, Julian Draxler aliyebandikwa jina
'Van Persie mpya:

Mwanasoka huyo hodari kutoka Ujerumani aliye na umri wa miaka 20 amewekwa kileleni mwa orodha ya wanasoka wanaowindwa na Arsenal.

Maskauti wa klabu hiyo wamefanya kazi usiku na mchana kumsaka
straika anayechipukia, na habari za kuvutia akapatikana nchini Ujerumani.

Wakuu wa Arsenal wanaamini kuwa Draxler anayechezea Schalke kama kiungo mshambulizi ana uwezo mkubwa kucheza kama fowadi wa
kati.

Ametajwa kuwa na ujuzi sawa na Robin van Persie na Thiery Henry ambao waliwasili jijini London kama mawinga na kukua kuwa
mastraika hodari.

Van Persie aliyejiunga na
maadui wa Arsenal, Manchester United mnamo 2012 alisaidia klabu hiyo kushinda taji la Ligi Kuu msimu uliopita.

Wenger anatarajiwa kumwendea Draxler mwezi huu lakini kandarasi yake haitamruhusu kuhama hadi mwisho wa msimu.
Kwa hivyo, kuna uwezekano mkubwa kuwa Wenger atawasilishaombi ya kumsajili kisha aendelee kuchezea klabu yake kwa muda uliosalia katika msimu.

Baada ya kukosa saini ya Luis Suarez na Wayne Rooney, Agosti, Wenger ameweka kipaumbele
shughuli ya kumtafuta fowadi wa kati.

Tegemeo kuu
Olivier Giroud ameanza mwaka vizuri kwa kufunga dhidi ya Aston Villa katika ushindi wa 2-1 lakini kwa kuwa yeye ndiye tegemeo kuu,
klabu itakuwa taabani iwapo atapata jeraha.

Nicklas Bendtner huenda akakaa nje kwa majuma matatu zaidi huku Mjerumani Lukas Podolski amejitahidi kufunga baada ya kupona jeraha.

Arsenal pia inamsaka nyota wa Real Madrid, Alvaro Morata katika dirisha la uhamisho la sasa.
Wakati huo huo, Wenger ana wasiwasi kuhusu nyota wake Tomas Rosicky aliyeumia puani baada ya kugongwa na Gabriel Agbonlahor
katika mechi dhidi ya Aston Villa.

“Hatujui iwapo jeraha ni kubwa. Nimezungumza naye na amenieleza kuwa aligongwa.”
Difenda wake Nacho Monreal pia ana jeraha alilopata katika mechi hiyo iliyochezwa Jumatatu.

Mchimba Riziki Michezo

Tuesday, January 14, 2014

Simanzi Watu 200 wazama mto Nile S.Sudan

Zaidi ya watu 200 raia wa Sudan Kusini
wamezama katika ajali ya boti kwenye mto
Nile wakikimbia vita vinavyoendelea katika
mji wa Malakal.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Sudan Kusini.
Boti hiyo iliyozama, ilikuwa imewabeba watu wengi kupindukia.

Watu hao walikuwa wanatoroka vita vinavyotokota katika mji wa
Malakal.

Mapigano yalizuka Sudan Kusini mwezi Disemba mwaka jana baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu aliyekuwa makamu wake wa Rais
Riek Machar, kwa kuwa na njama ya
kumpindua.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa zaidi ya watu
1,000 wameuawa tangu ghasia kuanza nchini

Zitto: Namsubiri Mh.Mbowe kwa hamu Mahakamani.

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amesema anamsubiri Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe mahakamani.

Zitto ametoa kauli hiyo siku moja
baada ya Mbowe kutangaza kumburuza mahakamani, kutokana na kile kinachodaiwa kumzushia tuhuma za uongo. “Nasema sitaki
malumbano na kiongozi yeyote, nachotambua masuala ya mahakamani yanajibiwa
mahakamani na si vinginevyo,” alisema Zitto.

Zitto alitoa kauli hiyo, baada ya MTANZANIA kutaka kujua msimamo wake kutokana na kauli
ya Mbowe kukusudia kumshitaki, kutokana na madai ya kusema uongo dhidi yake.

Zitto ambaye yuko nchini Nigeria anakohudhuria vikao vya Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali
kwa nchi za Afrika, alisema pamoja na hali hiyo, mahakama ndiyo njia pekee ambayo haki ya mtu inaweza kupatikana.

Alisema kwa msingi huo, hivi sasa hayuko tayari kuruhusu malumbano ambayo hayana tija kwa taifa.

“Nipo Nigeria na bahati mbaya ninaumwa sana,ila hivi leo ninamshukuru Mungu nimepata
nafuu kidogo. Kama nilivyosema mwanzo sitaki malumbano na mtu.

Pamoja na kusema anaumwa, hakuwa tayari kufafanua ni ugonjwa gani unaomsumbua.
“Huu muda nahitaji kutafakari maisha yangu kisiasa na kwa vyovyote vile masuala ya
mahakamani yatajibiwa mahakamani,” alisisitiza
Zitto.

Juzi Kurugenzi ya Habari na Uenezi ya CHADEMA, ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari
na kusema, Mbowe amezushiwa tuhuma zisizokuwa na ukweli wowote, zikilenga kumchafua kwa nafasi yake ya uongozi na kuipaka matope taasisi anayoiongoza.

Kutokana na hali hiyo, tayari Mbowe kwa mujibu wa taarifa hiyo, ameshawasiliana na wanasheria wake kwa ajili ya kuchukua hatua
za kisheria dhidi ya aliyezusha uongo huo.

Ingawa taarifa hiyo haikutaja jina la Zitto, lakini hivi karibuni mbunge huyo katika ukurasa wake
wa facebook, aliibua tuhuma nzito dhidi ya Mbowe.

Zitto, Samson Mwigamba na Dk. Kitila Mkumbo,
walivuliwa nyadhifa zao na Kamati Kuu (CC).

Baadaye CC iliwatimua uanachama, Mwigamba na Kitila kwa tuhuma za kukisaliti na kukihujumu chama, huku Zitto akikimbilia mahakamani kuzuia asijadiliwe.

Katika tuhuma hizo, Zitto alidai Mbowe alipokea michango ya fedha kutoka kwa makada wa CCM, Nimrod Mkono na Rostam Aziz, kusaidia kampeni za CHADEMA mwaka 2005 na 2010.

Pia Zitto, alidai Mbowe alipokea Sh milioni 40 mwaka 2005 kutoka kwa Mkono ili asifanye kampeni katika Jimbo la Musoma Vijijini, na
kwamba mwaka 2008 alimpatia Sh milioni 20 kusaidia CHADEMA ishinde uchaguzi mdogo wa
Tarime.

Kutokana na tuhuma hizo, CHADEMA kupitia Ofisa Habari Mwandamizi, Tumaini Makene,
iliamua kujibu mapigo.
Katika taarifa hiyo, ilieleza tuhuma hizo ni moja ya mikakati ya Zitto na wenzake wanaotaka kuhamisha mjadala wa makosa yanayowaandama ya utovu wa maadili na usaliti dhidi ya chama.

“Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe, amezushiwa tuhuma zisizokuwa na ukweli wowote, zikilenga
kumchafua kwa nafasi yake.

“Tuhuma hizo ni pamoja na kwamba, Mbowe mwaka 2005 eti alichukua fedha kutoka kwa
Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono kiasi cha Sh milioni 40 ili Mbowe asifanye kampeni
katika jimbo hilo.

“Mwaka 2008, Mbunge Mkono alimpatia Mbowe Sh milioni 20 kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Tarime, kisha akazitoa kwenye chama kama
mkopo na akalipwa.”

Zitto alidai mwaka 2010, wakati wa uchaguzi mkuu Mkono alimpatia Mbowe Sh milioni 200 kwa ajili ya kampeni za mgombea urais, huku
akipokea Sh milioni 100 kutoka kwa Rostam.

Kutokana na hali hiyo, Idara ya Habari ya CHADEMA, ilisema kupitia taarifa yake kuwa hakuna ukweli hata mmoja katika tuhuma hizo,
bali ni uongo na uzushi uliopangiliwa kama moja ya mikakati ya watu wenye malengo ya
kutaka kuilaghai jamii kwamba viongozi wa CHADEMA hawana tofauti na wale wa CCM.

Mchimba riziki


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score