Tuesday, April 28, 2015

Mwana Chama Wa Al-shabab Aliyepanga Kulilipuwa Bunge La....


POLISI wanamzuilia mfanyakazi wa bunge Bwana Ali Abdulmajid baada ya ripoti ya ujasusi kumhusisha na njama ya kundi la Al-Shabaab kulipua Bunge. 
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kutathmini hali, kundi hilo la kigaidi pia linasemekana kupanga kushambulia soko la Muthurwa, makanisa ya Nairobi Pentecostal Church, Holy Family Basilica, St Andrews PCEA, na Chuo Kikuu cha Nairobi.
Ripoti hiyo ambayo hutayarishwa na Mkuu wa Polisi wa Nairobi Central, Bw Paul Wanjama, ilimuagiza afisa mkuu msimamizi wa kituo cha polisi bungeni, Samson Chelugo, aimarishe usalama.
Ripoti hiyo iliyoandikwa Aprili 23 ilisambazwa sana Jumatatu katika mitandao ya kijamii.
Iliongeza kuwa mshukiwa huyo anayefanya kazi Bunge la Seneti anahusishwa na msikiti wa Riyadh eneo la Pumwani, ambao awali ulitajwa na ripoti ya Umoja wa Mataifa kama mmoja wa misikiti inayotumiwa na kundi hilo la kigaidi.
Mwekahazina wa msikiti huo Dkt Iddi Waititu Abdallah aliambia Taifa Leo kwamba Bw Ali Abdulmajid aliitwa na polisi Jumapili na akakamatwa na kufungiwa kituo cha polisi cha Kilimani baada ya kujiwasilisha kwao.
Alipuuzilia mbali ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa na kusema msikiti huo hauna uhusiano na  Al-Shabaab.
“Al-shabaab wametuma majasusi wa Amniyat kupanga mashambulio makubwa katika nchini katika siku mbalimbali. Nairobi maeneo yanayolengwa ni pamoja na Bunge kwa kuweka bomu majengo ya Bunge. Kundi hili linapanga kutumia mtu aliye na ushirika na msikiti wa Riyadh wa Pumwani na ambaye ni mfanyakazi wa Seneti kufanikisha shambulio hilo,” ripoti hiyo ya polisi ilisema.
Amniyat ndicho kitengo cha Al-shabaab kinachohusika katika kukusanya habari za kijasusi na kutekeleza mashambulio ya kujitoa mhanga.

Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score