Mashambulizi mawili ya kiharamia wiki iliyopita kwenye upwa ya Somalia yamezusha wasiwasi kwamba kitisho cha uharamia kwenye Pembe ya Afrika hakijaisha, liliripoti jarida la Seatrade Global siku ya Jumatano (tarehe 16 Oktoba).
Ijumaa iliyopita, maharamia waliokuwa kwenye mashua mbili waliirushia risasi meli ya mafuta inayopepea bendera ya Hong Kong, MV Splendor, likiwa ni tukio la kwanza la aina hiyo tangu mwezi Aprili, kwa mujibu wa Shirika la Ujasusi wa Baharini la Dryad lenye makao yake nchini Uingereza. Siku nne baadaye, genge hilo hilo la maharamia liliishambulia meli nyengine kubwa umbali wa maili 270 za majini kutoka mahala yalipotokea mashambulizi ya awali.
"... Mashambulizi hayo dhidi ya meli mbili ndani ya kipindi cha siku nne yanathibitisha kwamba biashara ya uharamia ya Somalia bado haijavunjwa," alisema Ian Millen, mkurugenzi wa upelelezi wa Dryad.
Millen alisifu hadhari na utaalamu wa timu ya walinzi wa MV Splendor katika kukabiliana na mashambulizi hayo, ambapo walifanikiwa kukinusuru chombo, na kuzitolea wito meli nyengine kwenye eneo hilo kudumisha viwango vya hali ya juu vya ulinzi.
Hata hivyo, uharamia kwenye bahari uko kiwango cha chini kabisa katika kipindi cha miaka saba, liliripoti Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (IMB) siku ya Alhamisi. Kwenye upwa wa Somalia, kulifanyika mashambulizi 10 ya kiharamia katika miezi tisa ya mwanzo ya mwaka huu, ikilinganishwa na mashambulizi 70 kwenye kipindi kama hiki mwaka 2012, ilisema IMB.
"Jukumu kubwa linalotekelezwa na wanajeshi wa majini kwenye upwa wa Somalia halipaswi kudharauliwa. Kuwepo kwao kunahakikisha kwamba maharamia hawafanyi kazi zao wakiwa na hisia za kutokuchukuliwa hatua kama mwanzoni," alisema Mkurugenzi wa IMB, Pottengal Mukundan.
"Ingawa idadi ya mashambulizi imeshuka kwa ujumla, kitisho cha mashambulizi kingalipo, hasa kwenye bahari ya Somalia na Ghuba ya Guinea," alisema. "Ni muhimu kwamba manahodha wa meli waendelee kuwa na hadhari wanapopita kwenye bahari hizi."
By Mchimba Riziki