Kampala,Uganda
Magaidi walioishambulia Kenya na Kutishia kuivamia Tanzania na Rwanda sasa waigeukia Uganda ,hapo jana walitoa vitisho balaa kuhusina na suala la kutaka kuivamia Uganda saa yoyote ile. Jeshi la Uganda nalo lipo Rada kuwathibiti wasifanikiwe kufanya shambulizi lolote na kuleta hasara
Uganda ilikuwa kwenye hali ya tahadhari siku ya Ijumaa (tarehe 18 Oktoba) kutokana na hofu za mashambulizi kama yale ya al-Shabaab katika jengo la Westgate jijini Nairobi, ambako bado wapelelezi wanaendelea kufukua miili iliyooza takriban mwezi mzima baadaye, liliripoti shirika la habari la AFP.
"Kuweni na tahadhari na chunguzaneni hatua na matendo ya kila mmoja, kwani bado tunatishwa na ugaidi," ulisema ujumbe wa polisi ya Uganda, huku vikosi vya usalama vikifanya doria nje ya maduka kwenye mji mkuu, Kampala.
Hatua hii ilifuatia ujumbe wa siku ya Jumanne kutoka ubalozi wa Marekani nchini Uganda ambao ulisema ubalozi huo ulikuwa ukiendelea "kutathmini ripoti kwamba mashambulizi kama yale ya Westgate yatatokea mjini Kampala hivi karibuni". Ubalozi huo ulisema hakukuwa na taarifa zaidi juu ya wakati na mahala wa mashambulizi yoyote.
Siku ya Alhamisi, wapelelezi walipata fuvu la kichwa lililoharibika kwenye mabaki ya jengo la Westgate, walisema polisi wa Kenya, wakiongeza kwamba kipimo cha DNA kitafanywa ili kusaidia kulitambua. Bunduki pia zilipatikana.
Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya linasema kuwa watu 23 walipotea baada ya kuzingirwa kwa jengo hilo.
Kuna wasiwasi mkubwa kwamba al-Shabaab watatekeleza kitisho chao cha kufanya mashambulizi zaidi, baada ya wanamgambo hao wenye mafungamano na al-Qaida kusema kupitia mabango kwenye maandamano nchini Somalia kwamba "Westgate ulikuwa ni mwanzo tu."
Mkanda wa vidio ya propaganda pia ulitolewa wiki hii na al-Shabaab ukikipongeza kikosi chake cha wapiganaji wa kigeni, ukionesha waasi kadhaa ambao wanadaiwa kuwa walitoka Uingereza na waliouawa kwenye mapigano.
Hapana shaka, vidio hiyo ilifanywa kabla ya mashambulizi ya Westgate kwani haizungumzii mashambulizi hayo, ingawa inataja juu ya "mateso ya Waislamu nchini Kenya" na pia kwenye nchi nyengine.
Vidio hiyo inayosimuliwa na mwanamme aliyevalia sare ya kijeshi na uso wake ukiwa umezibwa kwa kitambaa na anayezungumza lafudhi ya Kiingereza safi, inadai wapiganaji kutoka mataifa kadhaa ikiwemo Ethiopia, Eritrea, Lebanon, India na Pakistan wote wamepigana upande wa al-Shabaab.
By Mchimba Riziki
Saturday, October 19, 2013
Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved