Monday, April 14, 2014

Chuo Kikuu Nairobi Mtihani Wafurugwa Na Kuchanwa Mbele Ya Wahadhiri Waliokuwa Wasimamizi.

WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Nairobi Jumatatu walirarua karatasi za mitihani wakitaka waongezewe wiki moja zaidi ili kujiandaa vyema kwa ajili ya mtihani huo.
Chuo Kikuu Nairobi
Kundi la wanafunzi waliokuwa wakiongozwa na kiongozi wa wanafunzi, Paul Ongili maarufu Babu Owino, lilienda katika kila darasa ambamo mitihani ilikuwa ikifanyika na kurarua karatasi za maswali na vijitabu vya kuandikia majibu.

Mtihani wa somo la hisabati wa wanafunzi wa mwaka wa tatu na nne ambao tayari ulikuwa karibu kukamilika, ulikatizwa ghafla na wanafunzi hao ambao waliwataka wenzao kuondoka katika chumba cha mtihani.
Baadhi ya wanafunzi walilalamika walipoteza mali zao zikiwemo kadi za mtihani wakati wa rabsha hizo.
“Nimepoteza kadi yangu ya kufanyia mtihani, sijui nitapata wapi nyingine,” akasema Kennedy Nzioka, mwanafunzi wa uhandisi wa mwaka wa tatu.

Wahadhiri waliokuwa wakisimamia mitihani hiyo waliachwa mdomo wazi huku wakiwa wamejawa ghadhabu.
“Sina jambo la kuwambia wanahabari,” akasema Dkt Jeremiah Musuva ambaye alikuwa akisimamia mtihani wa somo la hisabati wa wanafunzi wa mwaka wa tatu.
“Mimi nilikuwa nimejiandaa vyema kwa ajili ya mtihani huu. Hata maswali yalikuwa rahisi,” akasema Edward Mailu, mwanafunzi wa Uhandisi mwaka wa tatu.
  Kulingana na Bw Ongili, wanafunzi hao wanataka uongozi wa chuo hicho kuwapatia wanafunzi muda zaidi ili kufidia wiki mbili ambazo wahadhiri walipoteza walipokuwa wamegoma.
“Tunataka wiki moja zaidi ya kujiandaa kwa ajili ya mtihani huo ili kufidia wiki mbili za mgomo wa wahadhiri,” akasema kiongozi huyo wa wanafunzi wakati wa mahojiano na waandishi wa habari
Bw Ongili ambaye alichaguliwa kuongoza wanafunzi wa chuo hicho, alidai kuwa wanafunzi hawakuwa wamejiandaa vyema kwa ajili ya mtihani huo baada ya kutatizwa na mgomo.
Alidai kuwa wiki iliyopita, wanafunzi waliwasilisha maombi yao kwa utawala wa chuo hicho wakitaka kuongezewa muda wa wiki moja kuwapatia wakati wa kutosha kusomea mtihani huo.

Maombi Rasmi
Hata hivyo, utawala wa chuo hicho ulikanusha madai hayo na kusema kuwa viongozi wa wanafunzi hawakuwasilisha maombi rasmi wakitaka kuongezewa muda.
“Uongozi wa chuo unapenda kushutumu kitendo hicho cha wanafunzi wachache kutatiza mtihani kwa madai kuwa hawajajiandaa vyema. Seneti ya chuo ndiyo ina mamlaka ya kusitisha mtihani ,” akasema afisa ambaye hakutaka kutajwa kwa sababu za kiusalama. 
“Kiongozi wa wanafunzi ni wanafunzi kama wengine na kulingana na sheria hakuna mwanafunzi ambaye ana mamlaka ya kuahirisha tarehe ya mtihani bila kupitia kwa seneti,” akaongezea.
Alisema kuwa tayari uongozi wa chuo umeanzisha mazungumzo na viongozi ili kutafutia suala hilo ufumbuzi.
Mitihani ilivurugwa ndani ya bewa kuu pekee lakini inaendelea vyema katika mabewa mengineyo tisa ya chuo kikuu cha Nairobi.


0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score