Waumini wa kanisa moja la Kaunti ya Murang’a Jumapili
walipitisha hoja ya kumtimua pasta wao baada ya kutiwa rumande kwa
madai ya kufanya uhuni katika jamii.
Pasta Simon Kanyoro wa kanisa la
Revival Ministries lililoko katika Eneo bunge la Kigumo alitakiwa kwanza
kushiriki kesi zake mbili zinazomkabili mahakamani bila ya kujihusisha
na shughuli zozote za utumishi wa kanisa hilo.
Kwa kauli moja, waumini wa kanisa hilo
walipitisha hoja hiyo kwa kuinua mikono juu, ambapo wote waliokuweko
walionekana kuunga mkono pasta wao aondolewe majukumu yake na
yakabidhiwe Naibu Pasta wao.
Katika kikao kilichoandaliwa katika
tawi la kanisa hilo la Maragua, Kiongozi wa masuala ya ustawishaji wa
Injili Bi Hellen Wangui aliwasilisha hoja hiyo kujadiliwa na baraza la
wazee wa kanisa na ndipo hatima ya pasta huyo ikatolewa.
Kwa sasa, pasta huyo ako katika
rumande ya jela kuu ya Murang’a baada ya kukamatwa na kufikishwa
mahakamani mwishoni mwa wiki jana alipovunja masharti ya bodi aliyokuwa
amepewa na mahakama kuhusu kesi nyingine iliyomkabili.
Masaibu yake yalimwandama aliposhtakiwa kati mwa mwezi huu kwa kubomoa nyumba ya ndugu yake mdogo kufuatia mzozo wa shamba.
Aidha, alidaiwa kutisha kumuua ndugu
huyo na alipowasilishwa mahakamani, akawachilia kwa bodi ya Sh10, 000,
kiasi alicholipa na kuachiliwa huru kesi yake iendelee akiwa hajawekwa
kizuizini.
Hata hivyo, Bw Kanyoro alikamatwa
tena mwishoni mwa wiki jana baada ya kumpiga mlalamishi na kisha
kutangazia maafisa wa polisi waliojitokeza kutuliza hali kuwa alikuwa
ameamua kumuua ndugu huyo ili kesi yake mahakamani ipate uzito.
Dhamana
Ndipo alifikishwa mahakamani na
akashtakiwa upya hali ambayo ilimfanya apoteze haki yake ya kuachiliwa
kwa dhamana na akawekwa rumande.
Bi Wangui alisema kuwa hali hiyo kwa
sasa inazua hoja nyeti katika mwongozo wa kanisa hilo na waumini
wameanza kuonyesha kutoridhishwa kwao na hali iliyokuwa ikimwandama
pasta huyo.
“Imetubidi tuwasilishe hoja ya
kutafuta mwelekeo wa kanisa letu kuhusu masaibu yanayomwandama pasta
wetu na hatimaye imeafikiwa kuwa kwanza ajitenge na masuala ya injili
kutuhusu,” akasema.
Alisema wao hawajamhukumu pasta
huyo, ila tu wangetaka kwanza aendelee na kesi zake mahakamani na kisha
akifaulu, arejelee majukumu yake ya kanisa.
“Lakini kwa sasa, pasta wetu
amesimamishwa kujihusisha na masuala ya kanisa hadi wakati
atakapomalizana na kesi zake. Ikiwa atafungwa jela, basi tutakuwa na
wajibu wa kutafuta mwongozo mbadala,” akasema.
0 maoni:
Post a Comment