Tuesday, January 28, 2014

Kenya si Kama Tanzania "Adhabu Kali Kwa Mchina Kenya".


Mahakama nchini Kenya imemtoza faini ya shilingi milioni 20 au dola laki mbili na thelathini raia mmoja mchina kwa kuhusika na biashara haramu ya pembe za ndovu.

Tang Yong Jian ametozwa faini ya dola laki mbili na thelathini
Adhabu hii inatokana na sheria kali za kudhibiti uwindaji wa wanyama pori.
Tang Yong Jian alikamatwa wiki jana akiwa na Pembe za Ndovu zenye kilo 3.4 katika sanduku lake katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta.
Ikiwa atashindwa kulipa faini hiyo huenda akafungwa miaka saba gerezani.
Kenya iliharamisha biashara ya pembe za Ndovu mwaka 1989, lakini kumekuwa na ongezeko la biashara hiyo haramu katika miaka ya hivi karibuni.

Kuna hitaji kubwa la pembe hizo barani Asia kwa matumizi ya mapambo huku wahifadhi wa mazingira wakishuku kuwa pembe za Vifaru hutumiwa kama dawa Mashariki mwa Bara Asia.

Kenya inakabiliwa na changamoto ya kuwindwa kiharamu kwa Ndovu zake
Nchini Kenya kilo moja ya Pembe za Ndovu, inaweza kukugharimu kati ya shilingi 12,000-18,000.
Uwindaji haramu umetajwa kama bishara haramu ya kimataifa ambapo wawindaji hasa huwawinda ndovu na vifaru kwa wingi. Ni hapo jana tu ambapo kifaru mmoja aliyetambulika kwa jina Josephina, aliuawa katika mbuga ya wanyama ya Nairobi.

Kenya inakabiliwa na changamoto ya kuwindwa kiharamu kwa Ndovu zake
Alikuwa kifaru wa kike mwenye umri wa miaka minne. Maafisa wa kulinda wanyama pori wanasema kuwa, kuuawa kwa Joeshina ni mfano mbaya kwani Vifaru wa kike wana umuhimu mkubwa katika kuongeza idadi ya wanyama hao wanapozaana.

Kwa muda wa wiki moja nchini Kenya, kimeripotiwa matukio manne ya uwindaji haramu katika mbuga tofauti tofauti.
Mkuu wa shirika la kulinda wanyama pori nchini Kenya, bwana William Kipsang, anasema kuwa tatizo la uwindaji linachangiwa na maswala ambayo hawawezi kudhibiti kama shirika.

''Serikali ya Kenya imetumia mamilioni ya fedha kuhifadhi wanyama pori , lakini nchini Kenya na kwingineko barani Afrika raia wengi wangependa kuona usalama wa binadamu ukishughulikiwa kwanza badala ya wanyama pori. Vile vile watu wengi huishi katika miji iliyo mbali na misitu na wanyama hao,'' alisema Kipsang

Mashirika ya kulinda wanyama wanasema ikiwa tatizo la uwindaji haramu halitatatuliwa, basi kwa muda wa miaka ishirini, ndovu na vifaru barani Afrika hawatokuwepo tena.
Asilimia kumi ya uchumi wa Kenya hutegemea utalii, ikiwa Kenya itapoteza Ndovu na vifaru wake, basi sekta ya utalii itaathirika pakubwa.

Chanzo BBC Swahili
Mchimba Riziki

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score