Sunday, January 26, 2014

Huyu Ndie Diamond Mwanamuziki Gali Afrika Mashariki Kote


Diamond Platinumz ndiye msanii kipenzi cha Afrika Mashariki kwa sasa ambaye kwa maneno matatu ya Kiingereza unaweza kumtaja kama; 'Hitmaker’, 'Heart Breaker’ na 'Moneymaker'.
Diamond Platinums Akiwa Kazini

Kwa ufupi ni mwanamuziki mwenye uwezo wa kuachia fataki wakati wowote kutokana na ubunifu mkubwa alionao, mzuri inapokuja katika suala la mauzo na mtundu inapofikia hatua ya kuwabadili vichuna.

Sifa hizo tatu zimemfanya kuwa msanii kichwa kwenye Ukanda huu akitajwa kuwa mwanamuziki ghali katika eneo hili.Ukweli ulipo ni kwamba umchukie au umkubali, Naseeb Abdul, ni msanii anayeshiriki ligi tofauti kabisa na wengine na wala hana mpinzani kwa wakati huu.
Lakini kama wasemavyo waswahili, safari ndefu huanza kwa hatua moja na licha ya umaarufu pamoja na utajiri mkubwa aliojipatia kwa kipindi kidogo, kuna alikoanzia Diamond Platinumz 'Rais wa wasafi.’

Rais wa Wasafi Diamond Na Timu Yake
HISTORIA
Sababu ya kuwa ghali kwa huduma zake, Diamond hakosi shoo zaidi ya mbili wiki baada ya nyingine, kwani mapromota kila uchao humpapatikia.
Akianza hakuna aliyemwandama kwani alionekana kuwa mbwa wa kubweka tu, ila sasa anang’ata kiasi cha kuhitaji walinzi wa kutosha kuhakikisha kwamba yupo salama.
Wengi hawafahamu alikochimbukia kijana huyu mzaliwa wa Kigoma, aliye na historia ndefu iliyokumbwa na umaskini wa kuogopesha enzi za utoto na ujana wake.
Diamond Na Timu Yake Ya Nyumbani Kigoma All Stars

UTAJIRI
Fataki ya 'Kamwambie’ aliyoifanya 2009 ndiyo iliyomfungulia milango ya rehema na kumwezesha kuwa nyota akiwafukuzia Lady Jay D na Jose Chameleone kwa ukwasi.
Tangu mwisho wa 2011, kwa mujibu wa blogu kadhaa ya Tanzania, akaunti yake ya benki haijawahi kushuka chini ya Ksh5.3 milioni (Tsh100 milioni). Na mali yake kwa ujumla inakadiriwa kuwa yenye thamani ya KSh64 milioni (Tsh1.2 bilioni).
Kutokana na kipato chake kizuri cha muziki, Diamond ameishia kuwa mjasiriamali mzuri akimiliki nyumba kadhaa za kupangisha, maduka ya nguo, vipande vya mashamba na magari makubwa.
Mtaani Tegeta, Dar-es-salaam, msanii huyo anaendelea kujenga jumba lake la kifahari ambalo linakaribia kumalizika na tayari yupo kwenye mchakato wa kujenga hoteli yenye hadhi ya 4-Star.
Aidha ana simu nne za rununu moja ikiwa na laini mbili hivyo basi kumaanisha ana nambari tano za simu. Hivyo wakati mwingi yeye hulazimika kuziweka kwenye milio ya chini kutokana na simu nyingi ambazo hupokea kwa siku.
Kando na hayo, makampuni mengi yanamlipa mamilioni ya pesa ili kutangaza bidhaa zao. Kampuni ya soda, Coca Cola na ile ya huduma za simu nchini Tanzania, Vodacom ni kati ya nembo kubwa zilizoko na mikataba minono naye.

MAISHA YA MUZIKI
Diamond Juu Ya Mchuma Moja ya Mali zake
Ndiyo kazi yake inayompa riziki na vile vile kumfanya kutoa ajira kwa timu yake kubwa ya zaidi ya watu 12, inayojumulisha madansa wake, msaidizi wa kibinasfi, wapiga picha na wapambaji.
Kila juma Diamond hupata shoo mbili hadi nne ambazo huhakikisha anakusanya ujumla wa zaidi ya KSh2 milioni ndani ya Tanzania hesabu za haraka zikionyesha kuwa kwa shoo moja huwagharimu mapromota Ksh350,000.
Anapoalikwa kutumbuiza nje, malipo yake kwa shoo moja huwa haipungui dola 25,000 (Ksh2 milioni). Miaka miwili iliyopita, alitumbuiza nchini Rwanda kwenye tamasha kubwa la uwanjani na kupokea Ksh10 milioni.
Katika taaluma ya muziki, amerekodi zaidi ya nyimbo 133 na mwanamuziki anayemuhusudu sana ni Usher Raymond wa Marekani.
Baada ya kutumbuiza kwenye ufunguzi wa shindano la Big Brother Africa 2012, wakati huo akitamba na 'Mbagala’, msanii huyo alitangaza ada mpya ya kufanya kazi naye.
Kupitia Facebook yake alisema mwanamuziki yeyote ambaye angetaka kumshirikisha katika wimbo wake, angelazimika kumlipa Ksh265,000 kwa audio na ikiwa ni video, ada hiyo inakuwa maradufu.
“Nimefanya colabo nyingi ila nyimbo hizo huwa hazitokei katika albamu yangu na wala hazininufaishi kwa lolote. Sasa hivi muziki una maana ya biashara na ndio maana najipa thamani hii. Ikiwa wasanii wa mbele wanalipisha kwa collabo kwa nini mimi nisifanye hivyo,” alisema.
Diamond alianza muziki kwa kujaribu kuwa rapa lakini marafikize wakamshauri ajaribu mtindo mwingine kwani huo wa kufoka hakuwa akiumudu.
Nguli huyo humtaja mamake kuwa kigezo cha mafanikio yake kwani aliishi kuandamana naye kwenye tamasha nyingi za kusaka vipaji na talanta na angemsubiri muda wote.
Wimbo wa 'Mawazo’ alimwandikia mwigizaji wa filamu za bongo Jacqueline Wolper aliyewahi kuwa mpenzi wake. Ule wa 'Kamwabie’ na 'Mbagala’ alimtungia mpenziwe kwa jina Sarah, aliyemkataa sababu hakuwa na uwezo. 'Ukimwona’ alimwimbia mchumba wake Wema Sepetu waliyerudiana, baada ya kumsaliti.

MAISHA NA VICHUNA
Diamond Vs Wema
Pamoja na sifa nzuri za kuwa 'hitmaker’ maisha yake upande wa pili yamekuwa yakiandamwa na kashfa nyingi za kimapenzi kwa tabia yake ya kuwabadilisha wanawake kila anapohisi kufanya hivyo.
Japo aliwahi kudai kuumizwa sana na Wema aliyemtuhumu kwa kutokuwa mwaminifu kwenye uhisiano wao, kisura huyo ambaye ni staa wa filamu za bongo pia aliwahi kudai kulizwa na Diamond kwa maana moja wanafanana inapokuja kwani wanawezwa kutajwa kuwa 'heartbreakers’.
Uhusiano wao umekuwa wa kukosana na kurudiana na hata wakati ambapo walikuwa njia panda, mara kwa mara waliripotiwa kutafutana na kuendelea na usuhuba.
“Mimi na Naseeb tuliachana baada ya yeye kunidanganyia na Jokate (Mwegelo) baada ya mimi kuwafumania wakipigana busu wakati huo tukiishi pamoja. Muda wote nimekuwa naye sikuwahi kumsaliti na nilijichunga sana kwa ajili yake maana nilikuwa nisharidhika naye licha ya ugomvi wetu wa kila mara,” Wema alinukuliwa na gazeti la Mzuka walipotemana mara ya kwanza.
Kwa sasa wawili hao wamerudiana na uhusiano wao ni wa mtu na mchumbake na wala sio mpenzi tena.
Wakati ambapo Diamond anakutana na mtangazaji Jokate, mrembo huyo alikuwa tayari yupo kwenye uhusiano na mwanavikapu wa NBA, Hasheem Thabeet uliodumu kwa miaka miwili na Jokate alikiri kuwa alikuwa akimpenda sana mchezaji huyo.
Hata hivyo kutokana na uhusiano huo wa mbali Jokate akiwa Tanzania na mwenzake Marekani, kichuna huyo alijipata kwenye hali ya upweke na hivyo kumpa nafasi Diamond.
“Ilitokea tu kwani nilikuwa kwenye hali fulani akatumia nafasi au fursa hiyo lakini angenitongoza mwaka huu (2013) nisingemkubali,” gazeti la Ijumaa lilimnukuu Jokate, Oktoba mwaka jana.
Ni uhusiano ambao Diamond alikiri kuwepo katika mojawepo ya mahojiano na Clouds TV, kitu ambacho alionekana kujutia.
Kuachana huko kukawa ndio mwisho wao licha ya mwanamuziki huyo kumnunulia gari la thamini ya Ksh800,000. Ukaribu kati ya Diamond na Wema uliendelea licha ya tofauti zao.
Ni ukaribu ambao kwa kiasi kikubwa uliwaumiza wengi, muhusika mkubwa akiwa mtangazaji Penny Mungilwa ambaye kwake msanii huyo alikuwa mwanaume wa kipekee.
Penny aliishi kusikia uvumi akawa anaupuuzia kutokana na jinsi alivyomwamini Diamond lakini picha za mwanamuziki huyo wakiwa na Wema, Hong Kong zilipovuja, zilivunja moyo wa hidaya huyo ambaye tayari alikuwa kahamia nyumbani kwake.

Diamond Kazini 

Mchimba Riziki Makala



0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score