Friday, February 28, 2014

Kisirani Kasarani:UCHAGUZI WA ODM WAKUMBWA NA VURUGU

UCHAGUZI wa Kitaifa wa ODM ulikumbwa na kisirani leo hii Ijumaa katika uwanja wa Kasarani ghasia zilipozuka muda mchache baada ya shughuli za kupiga kura kuanza na kupelekea shughuli hiyo kufutiliwa mbali.

Mgombea wa wadhifa wa katibu mkuu katika ODM Ababu Namwamba Februari 28, 2014. Picha/DENISH OCHIENG 

Vurugu hizo zilizopelekea masanduku ya kura kuvunjwavunjwa na kura zilizokuwa zimepigwa kutawanywa sakafuni, zilianza pale Mbunge Maalum Bw Isaac Mwaura aliposimama juu ya meza na kulalamika kwamba jina lake halikuwepo kwenye karatasi ya uchaguzi.

Bw Mwaura, ambaye alikuwa anawania kiti cha naibu wa katibu mkuu, alisema jina lake lililokuwa liwe la sita katika karatasi hiyo liliondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na lile la Peter Ole Musei.

Alidai kwamba kulikuwa na njama ya kumuondoa katika kinyang’anyiro hicho na kuongeza kuwa alilazimika kusimama juu ya meza baada ya malalamishi yake kwa wasimamizi wa uchaguzi huo kupuuzwa.

“Nilienda mpaka kwa wanachama wa bodi ya uchaguzi na kuwaelezea kuhusu hitilafu hiyo lakini hakuna mtu aliyenisikiliza. Ndio maana nikasimama juu ya meza. Wajumbe wengi waliniunga mkono na kusimama nami,” alisema Bw Mwaura akiongeza kwamba tukio hilo halikuwa limepangwa.

Mbunge huyo kijana alisema kuwa aliwasilisha malalamishi yake hadi kwa kinara wa chama Bw Raila Odinga.

Hali ya mguu niponye ilishuhudiwa huku wajumbe wakitumia chochote walichokuwa nacho ili kujikinga na viti na vitu vingine vilivyorushwa hewani.

Maafisa wa GSU walilazimika kuingia ndani ya ukumbi wakiwa wamejihami tayari kutuliza vurumai hiyo.

Maafisa wakuu wa ODM walionekana wakijaribu kumtuliza Bw Maura ambaye alikuwa amejawa na hasira. Aidha kulikuwa na madai kwamba orodha mpya ya wajumbe ilisambazwa ili kuwapendelea baadhi ya wawaniaji.

Njama

Wajumbe waliohojiwa baada ya ghasia hizo walisema kwamba wanataka uchaguzi huo ufanywe kwa njia huru na wazi huku wakidai kwamba kulikuwa na njama ya kuwapendekeza viongozi fulani kwa lazima.

Awali mbunge wa Dagoreti Kaskazini, Bw Simba Arati  alizomewa alipoingia ukumbini hata akashindwa kuhutubu. Bw Arati alikuwa mpinzani wa kinara wa chama hicho, Bw Odinga katika wadhifa wa kiongozi wa chama.

Kufikia wakati wa kwenda mitamboni, wajumbe wote walikuwa wamefurushwa kutoka uwanjani humo na haikuwa imebainika kama kikao cha leo kitaendelea.

Uwanja huo wa Kasarani ulipata jina la 'Kisirani’ (mahali ambapo mambo huenda kombo) mnamo 2002, pale Rais wa wakati huo Daniel arap Moi, alipowatenga hadharani Katibu Mkuu wa chama cha Kanu, Joseph Kamotho na kumpendelea aliyekuwa kiongozi wa National Democratic Party (NDP), Raila Odinga.

Mwezi Oktoba mwaka huo, Bw Moi alisimama hadharani kwenye mkutano mwingine wa wajumbe katika uwanja huo wa Kasarani, na kumchagua Uhuru Kenyatta kuwa mrithi wake, badala ya aliyekuwa makamu wake, marehemu Prof George Saitoti.

Swahili Hub
Mchimba Riziki

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score