Tuesday, June 3, 2014

Siri Kubwa Yafichuliwa Na Rais Museven. Ni siri Gani Hiyo?

Na Mathayo Ngotee

Siri ya utajiri ni kuepuka wanawake, pombe na sigara, kulingana na Rais wa Uganda Yoweri
Museveni. 

Rais Museveni Jumapili alieleza kuwa aliepuka anasa hizo akiwa bado ni kijana na badala yake akahifadhi pesa zake, hali iliyomwezesha kuwa na utajiri mkubwa alio nao hivi sasa.  “Sikuwa napenda wasichana. Nilikuwa nawapungia mkono tu kwa mbali kwa kuwa sikutaka kuharibu pesa zangu kwao,” akasema.

Aliongeza ilikuwa rahisi kwake kuweka pesa kwa akiba kwa vile hakuwa mnywaji pombe wala mvutaji
sigara.

Akizungumza wakati wa kufungwa kwa kongamano ya kibiashara mjini Mbiriizi, Wilaya ya Lwengo, Uganda, rais huyo alisisitiza kuhusu umuhimu wa kuhifadhi pesa huku akisema ilimsaidia kuwa tajiri hadi sasa hahitaji kuongezwa mshahara.

Katika kongamano hiyo, alizindua vyama vya mashirika 370 vilivyo vijijini, ambavyo vinatarajiwa kuhamasisha wanakijiji kuhusu umuhimu wa kuhifadhi pesa.

Aliwaambia wananchi wa Uganda wawe na desturi ya kuhifadhi pesa ili wao pia wawe matajiri kama yeye. “Ni muhimu muwe na desturi ya kuhifadhi pesa. Ninapozungumza kuhusu kuhifadhi pesa, najua kile ninachosema kwa kuwa nilianza kuweka kwa akiba pesa tangu nilipokuwa na umri wa miaka 21. Ni pesa hizo zilizoniwezesha kuwa tajiri nilivyo hii leo,” akasema.

Alizidi kusema, “Siku hizi ninasikia watu wakijadili kuhusu kuniongeza mshahara lakini ninahitaji mshahara kufanyia nini?” 

Bw Museveni ni mmoja wa viongozi wa mataifa ya Afrika ambao wamekuwa mamlakani kwa miaka mingi zaidi. Aliingia mamlakani mwaka wa 1986 baada ya kuhusika kwenye vita vilivyopelekea kupinduliwa kwa serikali za Idi Amin na Milton Obote.

Utawala wake umekumbwa na madai ya kuwa wa kiimla, kutokana na jinsi katiba ilivyobadilishwa kumruhusu aweze kuwa mamlakani kwa zaidi ya awamu mbili ilivyotakikana awali. Mwanasiasa wa upinzani nchini humo Kizza.

Besigye amekuwa akifungwa gerezani mara kwa mara kutokana na madai ya kuchochea ghasia anapoendeleza juhudi zake za kupigania kuwepo kwa haki za kidemokrasia Uganda.

Uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi uliandaliwa 2006, ingawa ulikumbwa na matukio ya ghasia huku Dkt Besigye pia akikamatwa.

Rais Museveni pia amekuwa mstari wa mbele kati ya viongozi wa Afrika wanaokashifu mataifa ya Magharibi kwa kudai yanaingilia utawala wa mataifa ya Afrika.

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score