Tuesday, February 17, 2015

Umaarufu Huu Utaleta Majonzi Tanzania. Tunangamizwa Na Siasa Chafu Kwa Kukosa Maarifa.

Kuanzia mapema mwaka jana wa 2014 chama tawala cha CCM na Msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania wameshindwa kwa pamoja kumchukulia hatua Mh.Edward Ngoyai Lowassa Aliyetangaza nia ya kugombania Urais kupitia chama tawala CCM. Mh. Lowasa ametembea nchi nzima akitoa misaada mbalimbali makanisani na misikitini pia kupiga kampeni kabla ya wakati.Kiukweli mimi ninaona hapa CCM na Mh. Lowasa wanadhihirisha na kuturudisha katika enzi zile; eti bado tuko kwenye chama kimoja. Mbaya zaidi, katika tafrija moja ya kutoa shukrani mwaka jana kanisani Monduli Lowasa alitangaza nia wasi wasi kuwa atagombania urais na hakuna yeyote aliyewahi kumuonya juu ya kitendo kile. Waziri mkuu huyu wa zamani aliyejiuzulu alinistaajabisha pale anapozunguka nchi nzima kujinadi watu wasimame wahesabiwe ili ndoto yake itimie.

CCM wanaonesha kutojali kabisa uwepo wa vyama vingine vya siasa hasa katika suala la haki sawa za mchezo wa kisiasa. Hii inanikumbusha moja ya tawala dhalimu zilizopita miongo kadhaa huko Jamhuri ya watu wa China: mwanamapinduzi—De Xio Peng—alipokuja na kauli mbiu: “Haijalishi kama paka ni mweusi au mweupe bali kama anaweza kukamata panya”. Ni mbinu ya kidhalimu na kizandiki isiyojali sheria na taratibu za mchezo haki kisiasa zinatumiwa na chama tawala. Ili mradi mgombea wao atangazwe kwa wananchi katika staili ya kupiga kampeni kwa kutumia rasilimali za serikali naweza kuhisi.

Baadhi ya magazeti yalifananisha na mikutano ya kuimarisha chama ambayo inafanywa pia na vyama vingine kila siku. Lakini mimi najiuliza: nimeona mheshimiwa Lowasa akijitambulisha na kutambulishwa na wanaojiita Watiifu wa Lowasa, Wanasiasa wengi wanamkumbatia Lowasa tena kutoka chama chake cha CCM. Panakuwepo na lundo la askari karibu wa kila aina, utaona rasilimali mbalimbali za serikali pale na hata baadhi ya viongozi wa asasi za serikali. Haijalishi hiki ni chama tawala ila kama nikifananisha na mikutano ya uimarishaji chama ya hivi vyama vya siasa vya upinzani naona kabisa hakuna usawa.

Nafikiri kipindi cha kampeni kila chama kinapewa fungu la shughuli hiyo na angalau kunakuwa na usawa ambao nafikiri msajili kauona. Nimesoma matangazo mengi yenye salam za pongezi kwa mheshimiwa Lowasa; haya yanatolewa na makampuni, mashirika, na hata idara za serikali. Mwanasiasa ama mwanaharakati kama mimi  akihoji anaonekana kama mwehu na vyombo vya habari. Hakuna chombo chochote cha habari kilichoandika juu ya athari za kitendo hiki cha pongezi kutoka taasisi mbalimbali. Uwezekano wa michezo michafu kati ya mgombea anayepongezwa na asasi zilizompongeza tuutizame iwapo atachaguliwa. Vyombo vya habari labda kwa minajili ya kupata fedha za matangazo vimeona hii itawaathiri kimapato. Uandishi makini upo hapa kweli? Wapi magazeti ya serikali, television ya serikali na radio ya serikali zote zinazungumzia maendeleo ya ccm na Lowasa pekee. Labda nimtahadharishe msajili wa vyama vya siasa aionye CCM na Lowasa dhidi ya tabia ya kuturudisha katika enzi ya chama kimoja ambapo haya yanayotokea ilikuwa ni utamaduni.

Yanayoandikwa sana na magazeti hapa ni juu ya kutabiriwa ushindi wa kizilzala—yaani Tsunami wa mheshimiwa Lowasa. Changamoto kwa vyombo vyetu vya habari ni hii: jamani hivi hamwoni huu ni wakati wa kuwakumbusha watanzania—wadanganyika—juu ya mengi yaliyotokea katika muongo huu unaokwisha wa mheshimiwa Kikwete? Kwa mfano, ile habari ya umeme ya IPTL, mkataba wa Network Solution, Escorow,RichMond pamoja na huu uvunjaji wa mkataba kati ya serikali na kampuni ya City Water kama dhihirisho la utendaji mbovu ambao wananchi wanapashwa waeleweshwe kwa kina ili waweze kuitumia kura yao kwa utashi makini?

Upinzani wetu ni dhahiri ni hoi ila ni lazima tuhakikishe katika serikali ijayo ya CCM wale wote waliohusika kwa njia moja au nyingine hawapewi dhamana tena ndani ya serikali. Katika madhila nilizotaja hapo juu ni wazi wapo mawaziri au hata wabunge; ni jukumu la vyombo vya habari kutoa habari za upelelezi za kina juu ya matukio hayo kwa wananchi ile nao wawajibishe kupitia kisanduku cha kura hapo mwishoni mwa octoba.

Nimegundua kwamba CCM kutuletea mgombea Maarufu imefunika rekodi zote chafu za CCM. Vyombo vya habari naviona vimeamua ‘kufunika kombe mwanaharamu apite’. Japo vyama vya upinzani viko hoi taabani, lakini ipo haja ya ukosoaji unaozingatia haki. Kwani ni wazi kama CCM ingekuwa safi tungetarajia nchi yenye maendeleo makubwa kuliko sasa. Nasema hivi kwasababu nchi ya Uganda pamoja na kuwa vitani kwa muda mrefu iko karibu sawa kiuchumi na nchi yetu. Hatutofautiani sana, nashindwa kuelewa sisi na amani yetu ya muda mrefu kunani jamani? Wanahabari amkeni jamani, igeni wenzenu kwa mfano wa Nation Media na The Standard wa Kenya, The Monitor, Vision na The Observer wa Uganda. Wanakosoa kwa manufaa ya umma.

Mchimba Riziki Kwa swali au Maoni niandikie
Barua pepe: mchimbariziki@gmail.com
Whatsapp: +254715323229

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score