Sunday, May 17, 2015

BUNGE LAGEUKA UWANJA WA MIPASHO. MAKALA

BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Kwa takriban wiki moja sasa, Bunge la Jamhuri ya Muungano limegeuzwa uwanja wa kampeni za uchaguzi na watunga sheria wetu wametumia nafasi yao kuonyesha ustadi wao katika mipasho.

Ni Bunge ambalo wananchi wengi waliotaka kulifuatilia walikuwa ni wale waliotaka kusikia vichekesho na ufundi wa kuzima hoja muhimu na kuzifanya kuwa vitu visivyo na manufaa kwa Taifa.

Hayo yote yalitokea wakati Bunge lilipokuwa likijadili Hotuba ya Makadirio na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo imeomba Sh5.8 trilioni, sawa na zaidi ya robo ya bajeti nzima ya Serikali ya mwaka 2015/16 ambayo ni Sh22.4 trilioni.

Hotuba hiyo ilizungumzia zaidi mafanikio ambayo Serikali ya Awamu ya Nne imeyapata katika kipindi cha miaka 10 na haikujikita sana katika kuangalia vipaumbele ambayo Serikali imeviweka kwa mwaka 2015/16.

Jambo kubwa ambalo limeonekana kuwa dhahiri ni jinsi ambayo Serikali ilishindwa kupeleka fedha Tamisemi, ambayo ndiyo inachukua shughuli nyingi za wizara hiyo kutokana na ukweli kuwa inahusika na Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa.

Imedhihirika kuwa katika mwaka wa fedha wa 2014/15 Serikali ilipeleka siyo zaidi ya asilimia 20 kwa Tamisemi, kitu ambacho kilisababisha miradi mingi ya maendeleo isitekelezwa kwa kiwango chake. Au kwa maana nyingine bajeti hiyo haikumgusa mwananchi kwa kuwa wizara iliyo karibu naye haikupewa angalau nusu ya fedha zilizopangwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Kwa kuwa wabunge ni wawakilishi wa hao wananchi, tulitegemea eneo hilo ndilo ambalo lingekuwa msingi mkuu wa mjadala. Tulitegemea waheshimiwa wabunge wangehoji sababu za Serikali kutoipa Tamisemi fedha za kutosha kutekeleza miradi ya maendeleo na nini kifanyike ili udhaifu huo uendelee.

Hata hivyo, kilichotokea ni tofauti. Wabunge waliohoji sababu za Serikali kutoipa Tamisemi fedha za kutosha, wakageuzwa kuwa wanakichokonoa chama na serikali yake na badala ya hoja zao kujibiwa, wakatafutiwa udhaifu wao na ndiyo ukawekwa mbele katika mjadala.

Matokeo yake, mjadala ukapoteza mwelekeo na mambo ya msingi kuhusu maendeleo ya wananchi yakawekwa kando.

Hili linaonyesha dhahiri kuwa wawakilishi wetu hawathamini kodi za wavuja jasho zinazowaweka mjini Dodoma kwa takriban siku 44 ili wajadili maendeleo yao.

Hata mahudhurio yamekuwa ni ya chini na wanaokuwapo ndani ya Ukumbi wa Bunge ni wale wanaosubiri nafasi za kuchangia, wengine wanaendelea kutumbua posho majimboni mwao au sehemu nyingine.

Alipoulizwa kuhusu vitendo hivyo, Naibu Spika Job Ndugai alisema ni vigumu kudhibiti wabunge kufanya kampeni wakati wa kuchangia kwenye mijadala ya hotuba za bajeti, hasa wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Ndugai anamaanisha kuwa hawa wabunge hawakupata nafasi ya kufanya kampeni majimboni mwao kwa kipindi chote bcha miaka mitano waliyokuwa ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria.

Au kwa maana nyingine, Ndugai anatueleza kuwa hali itakuwa hivyo kwa siku zaidi ya 30 zilizobaki kwa kuwa hiki ni kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu na wao kama viongozi hawataweza kuwadhibiti.

Hatudhani kuwa kauli hiyo ni sahihi na hatuamini kuwa wabunge hawana nafasi nyingine ya kupiga kampeni zaidi ya kipindi hiki.

Tunaushauri uongozi wa Bunge ukune kichwa kuangalia ni kwa jinsi gani itaweza kudhibiti tabia hii na tunaendelea kuwashauri wabunge watambue umuhimu na majukumu yao katika Bunge la Bajeti na kuwatendea walipa kodi kile wanachostahili.


Toka Swahili Hub.

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score