Sunday, April 7, 2013

Mpasuko wazuka madiwani Ngorongoro kushindwa kujiuzulu


Mh.Ole Telele
Uamuzi wa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kujiuzulu nyadhifa zao kama ishara ya kupinga hatua ya serikali ya kumega eneo lao la ardhi, umezua mpasuko na mgawanyiko mkubwa kati yao huku wengi wakisita kuachia ngazi kama walivyowaahidi wananchi wao.

Mgawanyiko huo ulisababisha mamia ya  wakazi hao ambao ni wafugaji wa kabila la Wamasai kutoka Tarafa za Sale na Loliondo, kupandisha mori, kutupa kadi zao za Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku wakishinikiza viongozi hao kutekeleza ahadi zao.

Mpasuko huo unadaiwa kuzuka baada ya vigogo wa serikalini kuwaita na kuwahoji baadhi ya madiwani waliokuwa wakionyesha msimamo mkali wa kutaka kuachia ngazi, hatua ambayo imewafanya waanze kukimbia ‘vivuli’ vyao.

Kama njia ya kutafuta suluhu, vigogo wa CCM akiwemo Katibu wa Uchumi na Fedha, Mwigulu Nchemba na Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye, wanatarajiwa wakati wowote kufika Loliondo kutafuta suluhu hasa ya madiwani hao kutojiuzulu.

Kujiuzulu kwa madiwani hao kumeelezwa kunaweza kusababisha mpasuko mkubwa ndani ya CCM wilayani humo na upo uwezekano mkubwa wa wanaCCM hao kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Katika mkutano wa hadhara walioufanya wiki iliyopita, madiwani hao waliwahakikishia wapiga kura wao kwamba wangeachia nafasi zao iwapo serikali kupitia Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, angetangaza uamuzi wa serikali wa kumega eneo la kilomita za mraba 1500 ili kulifanya kuwa eneo tengefu na maalum kwa ajili ya  mapito ya wanyamapori na kulinda vyanzo vya maji.

Mbunge wao, Kaika Saning’o Ole Telele, akiunga mkono maazimio ya wananchi hao alisema kama huo ulikuwa ni wakati muafaka wa kufanya hivyo na kama kweli wamedhamiria basi naye yupo pamoja nao.

Moja ya maazimio ya kikao hicho ilikuwa ni kuwataka viongozi wote wa kuchaguliwa kutoka tarafa hizo, kuanzia wenyeviti wa vitongoji, vijiji na madiwani waachia ngazi nyadhifa zao iwapo serikali itatekeleza azma yake ya kumega ardhi yao.

Tayari Waziri Kagasheki amekwishatangaza eneo la kilomita hizo kuwa ni eneo tengefu.
Waziri Kagasheki na Naibu Wake

Akizungumza kwa lugha ya kimasai katika mkutano wa hadhara uliofanyika Jumanne wiki hii huko Loliondo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Elias Ngorisa, aliendelea kudai kwamba uamuzi wao wa kujiuzulu bado upo pale pale, lakini bado taratibu zilikuwa hazijakamilika.

“Tueleweni vizuri, nilinukuliwa vibaya, hatukusema kwamba leo (Jumanne) ndio siku ya kujiuzulu, ila uamuzi wetu bado upo pale pale. Hatuwezi kufanya hivyo sasa kwa sababu bado sisi ndio kiungo cha kuwasilisha malalamiko ya wananchi kwa serikali kuu,” alidai.

Muda wote wa mikutano ya wananchi hao polisi wakiwa ndani ya gari lao walikuwa wakizunguka zunguka kwenye viwanja hali iliyowapa hofu ya kukamatwa ingawa kwa ujasiri waliendelea na mikutano yao na polisi wakiwa kama washiriki.

Halmashauri ya Ngorongoro ina jumla ya madiwani 28, ambapo kati yao saba ni wa Viti Maalum.
utalii

Source Nipashe

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score