Friday, September 20, 2013

Vyombo vya habari na Wanablogu Nchini Kenya Wapewa Onyo kali na ICC

Vyombo vya habari na wanablogu nchini Kenya wametaja utambulisho wa mwanamamke aliyejitokeza kama shahidi anayelindwa kwenye kesi ya uhalifu dhidi ya ubinadamu ya Naibu Rais wa Kenya, William Ruto, wakichochea onyo kali kutoka kwa Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) na hasira kali kutoka kwa makundi ya haki za binadamu.

Mwanamke huyo alikuwa ni shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka katika kesi dhidi ya Ruto, na siku ya Jumanne (tarehe 17 Septemba) alitoa mbele ya mahakama hiyo ushahidi wa namna alivyopata mateso huku akilia alipokuwa akielezea alivyofungiwa ndani ya kanisa moja akiwa na watu wengine kiasi cha 2,000 na kumiminiwa mafuta na kuchomwa moto baada ya uchaguzi uliozozaniwa wa mwaka 2007.

Shahidi huyo alitajwa tu kama "Shahidi P0536", uso wake ulifichwa na sauti yake kugeuzwa. Lakini ndani ya kipindi ambacho mahakama ilikuwa ikiendelea na kikao chake, iliyorushwa moja kwa moja na vituo kadhaa vya televisheni nchini Kenya, watazamaji walianza kukisia jina lake halisi kwenye mtandao wa Twitter na mitandao mingine ya kijamii, liliripoti shirika la habari la AFP.

Kufikia Jumatano, taarifa kadhaa kwenye Twitter zilitoa lile linaloweza kuwa jina lake halisi, ambapo mwanablogu mmoja wa Kenya na mtandao wa gazeti moja walichapisha hata picha walizosema ni za shahidi huyo. Maoni kadhaa pia yalimtaja mwanamke huyo kama "muongo".

ICC ilisema inaweza kuchukua hatua za kisheria.

"Ubainishaji wowote wa utambulisho wa shahidi ambaye utambulisho wake umelindwa... ni sawa sawa na kosa la jinai," alisema jaji kiongozi wa ICC, Chile
Eboe-Osuji. "Mambo hayo yatachunguzwa na watuhumiwa watafunguliwa mashtaka."

Jaji huyo alisema onyo hilo linamuhusu "kila mtu ndani ya chumba cha mahakama, kwenye eneo la umma, nchini Kenya, na kwengineko kote duniani", na kuwatolea wito "wanahabari, wanablogu, watumiaji wa mitandao ya kijamii au washiriki na wenye mitandao... kujitenga na lolote linaloweza kubainisha au kujaribu kubainisha utambulisho wa mashahidi wanaolindwa."

Shirika la haki za binadamu la Amnesty International lilisema "limetiwa wasiwasi sana" na kutoa wito kwa "ICC na mamlaka nchini Kenya kuchukua hatua madhubuti za kulinda usalama na afya ya shahidi huyu na familia yake."

Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya, jumuiya huru isiyo ya kiserikali, ilisema mashahidi wengine sasa wanaweza kujitoa kwenye kesi hiyo.

"Kwa kuwa sasa shahidi huyu ametambuliwa, itakuwa ni shida kuwahakikishia wengine kwamba wao na familia zao watakuwa salama. Na nchini Kenya, hakuna familia ndogo tu: kuna mashangazi, mama wadogo na wakubwa, wajomba na baba wadogo na wakubwa, binami na wapwa," alisema msemaji wa Kamisheni hiyo, Beryl Aidi.

"Mashahidi wana haki ya kuhisi kwamba familia na jamaa zao wanaweza kuwa hatarini na wakataka kujitoa," alisema.

Endelea kuperuz ndani ya Mchimba riziki kwani baadaye kidogo tutawaletea maoni ya Wakenya kuhusu "Nini maoni yao kuhusiana na majina ama bahasha aliyonayo jaji Philip Wako ya watu wengine wanaotajwa kuhusika katika ghasia ya mwaka 2007/2008 Je kuna umuhimu wa majina hayo kuwekwa hadharani kabla ya kufika The Hegue {ICC}.


By Mchimba Riziki

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score