Watu 12 walikufa na wengine kadhaa kujeruhiwa
baada ya treni ya abiria kuligonga basi kwenye
makutano ya reli jijini Nairobi siku ya Jumatano
(tarehe 30 Oktoba), walisema maafisa wa polisi.
Ajali hiyo ilitokea kwenye wilaya ya Eastlands,
Nairobi, wakati barabara zikiwa zimejaa watu
katika kipindi cha pilika pilika nyingi za magari
asubuhi, alisema kamanda wa polisi wa eneo
hilo, Benjamin Nyamae, kwa mujibu wa shirika
la habari la AFP.
"Basi hilo lilipita mstari wakati treni likija kwa
kasi kubwa," alisema Mkuu wa Polisi wa Nairobi,
Benson Kibui.
Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilisema
abiria 34 walijeruhiwa na kupelekwa kwenye
Hospitali ya Mama Lucy kwa ajili ya matibabu na
17 wako kwenye Hospitali ya Taifa ya Kenyatta
kwa ajili ya matibabu maalum. Wengine wawili
wanatibiwa kwenye Hospitali ya MP Shah, kwa
mujibu wa gazeti la Daily Nation la Kenya.
"Tutafanya uchunguzi wetu kamili kwa
kushirikiana na polisi ili kujua kipi hasa
kimetokea," alisema mkuu wa kampuni ya Rift
Valley Railways, Darlan David. "Hata hivyo,
popote palipo na alama ya kukata njia, kanuni ni
kwamba magari yote husimama kupisha treni
inayokaribia kufika."
Dereva wa basi hilo, Edward Githae Wanjau,
mwenye umri wa miaka 43, yuko mikononi mwa
polisi na "atafikishwa mahakamani na
kushitakiwa kwa kusababisha vifo vya watu 12
na kujeruhi wengine kadhaa kwa kuendesha gari
katika hali ya hatari," alisema Mkuu wa Polisi,
David Kimaiyo, kupitia mtandao wa Twitter.
0 maoni:
Post a Comment