Wednesday, October 30, 2013

Maofisa wa Somalia wasifu shambulio la Marekani dhidi ya mtengenezaji bomu wa ngazi ya juu wa al- Shabaab

Msemaji wa waziri mkuu wa Somalia Ridwan
Haji Abdiwali alisema serikali ya Somalia ilikuwa
na taarifa kuhusu mipango ya Marekani
kumshambulia mtendaji mwandamizi wa al-
Shabaab Ibrahim Ali Abdi, ambaye pia
alijulikana kama Anta Anta, katika kijiji cha
Dhaytubaako.
"Tulifanya kazi kwa kushirikiana na serikali ya
Marekani kufanya aina hizi za mashambulio,
kama tunavyofanya na yeyote yule [anayejaribu]
kuondoa kikundi hiki cha ugaidi,"
Anta Anta alihusika na misheni za kujitoa
mhanga za al-Shabaab na kuwa tishio kwa
umma, alisema Abdiwali, akiongezea kwamba
operesheni hiyo ilikuwa ni mafanikio kwa serikali
ya Somalia na watu wake.
"Tuna furaha [kuhusu matokeo ya shambulio
hilo] na tunayakaribisha," alisema. "Tuna
matumaini ya kuwazuia [watendaji] wengine
kama huyo."
Anta Anta anasemekana kujulikana vizuri kwa
kutengeneza fulana za milipuko na kutayarisha
mabomu ya kwenye magari yanayotumiwa mara
kwa mara na al-Shabaab.
Wakaazi waliokuwa karibu na eneo la
mashambulio waliripoti kuwa watu wapatao
watatu walikuwa kwenye magari yaliyoungua,
ambayo yalilipuka kwa moto muda mfupi baada
ya sauti ya ndege kusikika hewani, kwa mujibu
wa AFP.
Mashambulio ya ndege isiyo na rubani yalifuatia
operesheni nyingine ya Marekani ya mapema
mwezi huu, wakati kitengo cha wataalamu cha
makamanda wa Marekani kilipokuja kwenye
ufukwe wa mji wa Somalia ya kusini wa Barawe
katika jaribio la kumkamata Abdulkadir
Mohamed Abdulkadir "Ikrima" , Mkenya mwenye
asili ya Somalia na anayedaiwa kuwa kamanda
wa al-Shabaab wa wapiganaji wa nje.
Operesheni zote za Marekani zimekuja baada ya
uzingiraji wa siku nne wa al-Shabaab wa kituo
cha maduka ya biashara cha Westgate cha
Nairobi mwezi Septemba ambapo watu wapatao
67 waliuawa.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Somalia
Abdikarin Hussein Guled aliiambia Redio
Mogadishu kwamba shirika la upelelezi la nchi
yake limekuwa likimfuatilia Anta Anta kwa muda
fulani.
"Operesheni ambayo mtu huyu aliuawa ilikuwa
muhimu sana kwa serikali," alisema Guled. "Mtu
huyu alikuwa na dhima kubwa katika vifo vya
raia wengi wasiokuwa na hatia na kifo chake
kitasaidia kurejesha amani."
Kushirikiana na wabia wa kimataifa
Mbunge wa zamani Mohamud Weheliye Waqaa,
ambaye alitumikia katika Serikali ya Mpito ya
Shirikisho, alisema mashambulizi ya ndege
zisizokuwa na rubani ni njia nzuri ya
kuunganisha mafanikio ya usalama wa Somalia
na kuiunga mkono serikali ya Somalia.
"Serikali ya Somalia inapaswa kushirikiana
taarifa na [wabia] wanaofanya mashambulizi
hayo ili kuwatoa magaidi,"
Kwa kuzingatia ukweli kwamba jeshi la Somalia
bado halijafanikisha uwezo wa kiufundi kufanya
operesheni hizo, alisema, ni muhimu kwamba
jeshi la Somalia lifanye kazi kwa kushirikiana na
wabia wa kimataifa wakikusanya taarifa katika
maeneo huku wakiomba msaada wa kufanya
aina hizi za mashambulizi inapohitajika.
Hata hivyo, mbunge Mohamed Abdi Yusuf
alisema utawala wa Rais Hassan Sheikh
Mohamud haukupaswa kuidhinisha
mashambulizi hayo bila kushauriana kwanza na
bunge.
"Ubia kama huu unaohusisha ushirikiano kati ya
utawala na nchi za kigeni unapaswa
kuwasilishwa [kwa ajili ya mjadala] bungeni,"
Alisema mapambano yanaweza kusababisha
madhara ambayo hayakukusudiwa kama vile
vifo vya raia, hivyo makubaliano ya wazi
yanapaswa kufikiwa kabla ya kuanza.
Kuimarisha uwezo wa kiintelijensia
Wananchi wa Somalia pia wana maoni
mbalimbali kuhusiana na operesheni hiyo.
Sado Dahir, mwenye umri wa miaka 26
mwanafunzi wa sayansi ya jamii katika Chuo
Kikuu cha Somalia, alisema mashambulizi ya
kutumia ndege zisizokuwa na rubani yalikuwa
ushindi kwa umma wa Somalia.
"Kwanza, hii ni mara ya kwanza kabisa kumsikia
mtu mwenye jina hili, na mwanzo nilidhani
kwamba hakuwa maarufu sana ndani ya al-
Shabaab. Hata hivyo, niliposikia kwamba
alihusika katika kufanya milipuko, nilitambua
jinsi alivyokuwa hatari katika umma," "Hii ni operesheni nzuri sana ambayo
ilifanyika kwa mafanikio na ninaipongeza."
Dahir pia alisema ilikuwa ni muhimu kwa serikali
ya Somalia kuimarisha uwezo wake wa
kiintelijensia.
"Uimarishaji pekee hautafanikisha jambo lolote.
Kila shambulio lililofanyika dhidi ya al-Shabaab
linapaswa kuwa lililopangwa kwa makini ili
lifanikiwe kama hili, na serikali inapaswa
kufanya kazi na serikali zote duniani kuhusu
kuimarisha kitengo chake cha intelijensia,"
alisema.
Lakini Mohamed Jimale, mwenye umri wa miaka
57, alisema ingekuwa afadhali
kumkamata Anta Anta badala ya kumuua.
"Kama serikali ya Somalia na Marekani ilijua
kuhusu anakopatikana mtu huyu anayeitwa Anta
Anta ambaye ni mwanachama wa al-Shabaab,
ninadhani ingekuwa vizuri zaidi kumkamata ili
aweze kuhojiwa na kupata taarifa zaidi, kwani
yeye siye kiongozi hatari peke yake wa al-
Shabaab," alisema. "Hata hivyo, ninaunga
mkono jitihada za kupambana na kila kitu
ambacho kinaleta tishio katika umma."

By Mchimba Riziki

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score