Friday, January 3, 2014

AMRI JESHI MKUU AMWAPISHA IGP MANGU IKULU

Kamishna wa Polisi, Ernest Mangu,

Juzi, Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete,
alimwapisha Ernest Mangu kuwa Inspekta
Jenerali wa Polisi (IGP) akichukua nafasi
iliyoachwa na Said Mwema ambaye amestaafu
kwa mujibu wa sheria.

Mbali na Mangu, Rais pia alimwapisha
Abdulrahman Kaniki kuwa Naibu Inspekta
Jenerali wa Polisi, cheo kipya katika mfumo
wa jeshi hilo.

Tunapenda kuwapongeza
makamanda hao wawili kwa uteuzi huo, pia
kumtakia heri ya kustaafu, Mwema.

Hata hivyo, pamoja na pongezi hizo,
tunaamini kwamba wanazifahamu vyema
changamoto zinazowakabili katika kutimiza
majukumu yao hasa ikizingatiwa kwamba
‘wamekulia’ ndani ya jeshi hilo.

Mara baada ya kuapishwa, Mangu alikaririwa
na vyombo vya habari akisema kwamba
ataanza kazi kwa kupambana na uhalifu wa
aina zote pamoja na ajali za barabarani.

Kimsingi hayo ndiyo masuala makubwa
ambayo jeshi hilo lililo na wajibu wa kulinda
raia na mali zao linapaswa kuyasimamia.

Akilihutubia Taifa juzi usiku, Rais Kikwete
alisema Jeshi la Polisi limeendelea kupambana
na ujambazi wa kutumia silaha na mafanikio
yameendelea kupatikana na kusema kwamba
matukio ya ujambazi yalipungua mwaka 2013
ikilinganishwa na mwaka 2012.

Alisema mwaka 2012 matukio ya ujambazi
yaliyoripotiwa yalikuwa 6,872 na kwa mwaka
2013 yalikuwa 6,409. Tunasema upungufu huo
ni mdogo na tunaamini kwamba hiyo ndiyo
changamoto kubwa inayomkabili Mangu na
Kaniki katika kuwahakikishia wananchi
usalama wao.

Tunasema hivyo kwa kurejea kauli ya Rais
katika hotuba yake hiyo kwa Taifa juzi
kwamba Julai mwaka jana, aliamua
kulihusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), katika kupambana na
ujambazi wa kutumia silaha na utekaji wa
magari katika Mikoa ya Geita, Kagera na
Kigoma.

Tunadhani kwamba ipo haja sasa kwa Serikali
kuliwezesha jeshi hilo kushika hatamu za
usalama wa ndani ya nchi na kuwafanya
wananchi watekeleze majukumu yao ya kila
siku.

IGP Mangu pia aligusia suala la usalama
barabarani. Hakuna ubishi kwamba ajali za
barabarani zimekuwa na mchango mkubwa
katika kuongeza idadi ya vifo na ulemavu
kwa wananchi.

Katika hili, moja ya sababu kubwa za
kuendelea kutokea kwa ajali katika mtindo
unaofanana ni kutozingatiwa kwa Sheria za
Usalama Barabarani, pia kutosimamiwa vyema
na waliopewa dhamana.
Tunaamini kwamba kwa kuwa IGP Mangu
ameliona hilo, tutaona jitihada zaidi
zikiwekwa katika kuzuia ajali badala ya
kusubiri zitokee ndipo hatua za zimamoto
zichukuliwe.

Katika hilo la ajali za
barabarani, IGP Mangu anapaswa kutafuta
mwarobaini wa kudhibiti ajali zinatokana na
uendeshaji wa pikipiki za biashara maarufu
kama bodaboda.

Licha usafiri huu kuwa mkombozi kwa
wananchi hasa wa kipato cha chini,
umekuwa janga kubwa kutokana na kuongeza
idadi ya vifo vinavyotokana na ajali za
barabarani na ulemavu.

Source Mwananchi

Share by Mchimba Riziki

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score