Monday, March 10, 2014

Sheria Yaanza Kufanya Kazi Uganda Wawili Watupwa Gerezani kwa Kosa La......................

Wanawake wawili, mshtakiwa na mlalamishi, waliofika mahakamani wakiwa wamevalia minisketi walifungwa gerezani baada ya jaji kusema mavazi yao yalitatiza mahakama.

Wanawake wakiwa wamevalia minisketi.
Kampala, Uganda

WANAWAKE wawili waliofika mahakamani wakiwa wamevalia minisketi walifungwa gerezani baada ya jaji kusema mavazi yao yalitatiza mahakama.
Bi Prosy Nasuna alikuwa amemshtaki mwanamke mwingine kuhusu deni la Sh103,182.
Stakabadhi za mahakama zinaonyesha Bi Nasuna alimpeleka Bi Jane Nabukenya mahakamani kwa kwenda kinyume na makubaliano yao alipokosa kumlipa deni lake.

Hata hivyo, alipoenda Bukomansimbi kusikiza kesi yake wiki jana, yeye pamoja na mshtakiwa walijikuta wakiishia gerezani.
Awali, kulikuwepo manung’uniko na kelele wakati watu waliposema mavazi yao yalipigwa marufuku kwenye sheria ya kukabiliana na ponografia iliyopitishwa hivi majuzi.
Sheria hiyo inasema ponografia inahusu mbinu yoyote ya kuonyesha sehemu nyeti za binadamu hasa kwa minajili ya kunyegeza.
Hali hii ilimpelekea Hakimu Mkuu Catherine Baguma kuagiza wakamatwe kwa kutoheshimu mahakama.
Alisema mahakama haingeweza kuendelea na kesi hiyo ikiwa wawili hao walikuwa wamevaa minisketi.
Bi Baguma aliwahukumu wawili hao kifungo cha masaa matatu gerezani na kuahirisha kesi yao hadi Machi 13.
Mnamo Desemba mwaka jana, bunge la Uganda lilipitisha sheria ya kuharamisha minisketi ambayo inalenga kuweka wazi kosa la ponografia kwenye sheria za nchi hiyo.
Huku baadhi ya wabunge wakidai mswada huo ulikiuka haki za kibinadamu, wengi waliunga mkono Serikali na kuupitisha.
“Kwa kuidhinishwa kwa mswada huu, ndoto yangu imetimia,” Kasisi Simon Lokodo, aliye Waziri wa maadili alisema.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge walilalamika kuwa maelezo ya mswada huo kuhusu ponografia ni pana mno na yanakiuka tamaduni za Uganda za kudumisha tofauti zilizopo katika jamii.
Mwenyekiti wa kamati ya sheria na masuala ya bunge Steven Tashoboya, ambaye kamati yake ilipigia debe mswada huo, alisema ponografia huongeza ubakaji wa watoto na wanawake.
Mashoga
Sheria hiyo inasema ponografia ni tendo lolote la kitamaduni, tabia au mawasiliano kwa njia ya mazungumzo au maandishi kikamilifu au sehemu yake, au taarifa ya habari, au burudani, au onyesho la sanaa, au picha, au video, au muziki, au densi.

Imepiga marufuku pia mchanganyiko wa hayo yote unaoonyesha sehemu za mwili wa binadamu kama vile matiti, mapaja, makalio, na sehemu za uzazi zikiwa uchi au bila mavazi ya kutosha, mbali na kuonyesha watu wakijamiiana, au kuonyesha tabia zinazolenga kunyegeza, na mienendo mingine yoyote inayolenga kuozesha maadili.

Sheria hiyo imeanza kutekelezwa siku chache baada ya Rais Yoweri Museveni kutia saini sheria inayopiga marufuku uhusiano wa kimapenzi kati ya watu wa jinsia moja.


0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score