Monday, March 10, 2014

Mishahara Yapunguzwa Kwa Wafanyakazi Wa Umma Kenya

Rais Uhuru Kenyatta ameagiza mishahara ya wakuu wa mashirika ya serikali ipunguzwe kwa asilimia 20 na kuonya kuwa watakaokaidi agizo hilo watatimuliwa.
Rais Uhuru na Makamu Wake Ruto Wakijadili jambo 


RAIS Uhuru Kenyatta Jumatatu aliagiza mishahara ya wakuu wa mashirika ya serikali ipunguzwe kwa asilimia 20 na kuonya kuwa watakaokaidi agizo hilo watatimuliwa.
Rais Kenyatta alisema wakuu wa mashirika ya umma wanafaa kufuata nyayo za maafisa wa ngazi za juu serikalini kwa kukubali mishahara yao ipunguzwe kwa hiari.

“Maafisa ambao hawataridhishwa na agizo hilo waende mahakamani, ikiwa mahakama itaamua kuwa wafidiwe tutawalipa na kazi zao tupatie watu wengine. Kuna Wakenya wengi ambao wanataka kazi hizo,” akaonya Rais Kenyatta.

Rais Kenyatta alisema hayo wakati wa uzinduzi rasmi wa kongamano lililoandaliwa na Tume ya Mishahara (SRC) kujadili jinsi ya kupunguza kiasi kikubwa cha fedha zinazotumika kulipa watumishi wa umma, chini ya kauli mbiu: 'Mshahara wako mzigo Wangu’  katika jumba la KICC, Nairobi

Tangazo hilo linafuatia siku chache baada ya rais na naibu wake Bw William Ruto, mawaziri na makatibu wa wizara kutangaza kupunguzwa kwa mishahara yao kwa asilimia 20.
Tayari baadhi ya viongozi  wamekubali kukatwa mishahara yao huku wa hivi karibuni akiwa mwenyekiti wa Tume ya Mishahara (SRC) Bi Sarah Serem, ambaye jana alisema kuwa marupurupu yake yapunguzwe kwa asilimia 10.
Rais Kenyatta alidokeza kuwa tayari zoezi la kuleta mageuzi katika mashirika ya serikali limeanza ili kuhakikisha kuwa wafanyakazi wazembe wanatimuliwa.
Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka huu wa fedha wa 2013/2014, asilimia 56 ya bajeti ilitumiwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wa umma na matumizi mengine ya afisini.
Hiyo inamaanisha kuwa ni asilimia 44 ya fedha ambazo zilitumika kuendeleza miradi ya maendeleo.
Asilimia saba
“Asilimia 13 ya mapato ya nchi ilitumika kuwalipa mishahara watuishi wa serikali tofauti na kiwango cha kimatifa cha asilimia saba. Serikali haiwezi kutumia kiasi hicho kikubwa cha fedha kulipa watumishi wa umma mishahara badala ya kuendeleza miradi ya maendeleo,” akasema huku akiongeza kuwa serikali itasawazisha upya mishahara ya watumishi wa umma baada ya kubainika kuwa wafanyakazi wenye ujuzi sawa wanalipwa mishahara tofauti.
Kulingana na ripoti iliyotolewa na Kituo cha Kutafiti masula ya Sera (KIPPRA),  mawaziri ni miongoni mwa watumishi wa umma wanaolipwa mishahara minono zaidi isiyopungua Ksh 737,332 huku mtumishi wa serikali anayepata mishahara ya chini zaidi akipokea mshahara wa Sh 7,701.
Rais alipuuza mapendekezo ya kutaka kuongezwa kwa ushuru kuimarisha mapato ya nchi huku akisema kuwa hatua hiyo itakuwa hatari katika ukuaji wa uchumi.
“Pendekezo la kutaka tuongeze ushuru halifai kwani tutakuwa tunawafukuza wawekezaji ambao ni muhimu katika ustawi wa uchumi,” akasema.
Maafisa wa ngazi za juu serikalini wanapata marupurupu 16 ya aina mbalimbali jambo ambalo tume ya SRC inasema kuwa ni uharibifu wa fedha za umma.

Mchimba Riziki

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score