Sunday, March 16, 2014

Ukristo Wetu ni kama Safari ya Imani

Jumapili ya Pili ya Kwaresima

Dhamira: Ukristo Wetu ni kama Safari ya Imani
Masomo: Mwanzo 2:1-4; 2 Tim. 1:8-10; Mathayo 17:1-9


"Toka wewe katika nchi yako na jamaa zako, uende mpaka inchi nitakoyokuonyesha". Maneno hayo kutoka Somo la kwanza la Jumapili ya Pili ya Kwaresima, yatupatia kiini cha ujumbe wa Jumapili hii, yaani kama Wakristo tunaitwa tuache nchi yetu na utamaduni wetu na tutoke tuingie safarini ya imani kuelekea mahali Bwana atakapotuonyesha. Huo pia ulikuwa wito wa Mungu kwa Abrahamu. Kwa kawaida sisi wanadamu hupendelea kukaa mahali tulipo na kuwa starehe. Lakini kama Abrahamu, Mungu anatuita tutoke katika nchi yetu twende mahali atakapotuonyesha. Hivyo Ukristo wetu ni kama maisha ya safari ya imani na matumaini katika Mungu. 

Nchi ya Abrahamu wakati ule kabla ya kuitwa ilikuwa nchi yenye uchumi wa hali ya juu. Lakini dini yao ilikuwa ya kuabudu miungu ya kuwaongeza watu nguvu za kimwili. Hivyo ibada yao ilifanyika mahali paliokuwa na mtindo wa kufanya umalaya wa kiume na wa kike. Pia ibada yao ilikuwa kuwatoa watoto wachanga kama sadaka, kwa sababu miungu yao ilidai damu ya watoto.  Basi twaweza kuelewa sababu ya Mungu kumwita Abrahamu aondoke kutoka mazingira ya haina hiyo. Nasi pia twaitwa tuondoke tutoke kwenye vitendo vibofu vya utamaduni wetu tuingie mahali pa neema ya Mungu. Twakumbushwa kwamba, hata ingawa huenda tukapata shida na majaribio njiani, hapo mwisho tutapata ule utukufu tulioahidiwa. Ndiyo sababu Mtk. Paulo anatukumbusha kwamba kwenye safari yetu ya imani tunaelekea mahali tusiopajua, na hivyo tuwe tayari kukabiliwa na shida na mateso. Wakati huu wa Kwaresima, tunaitwa tuvumilie mabaya kwa ajili ya Injili, kwa kadiri  ya nguvu ya Mungu.


Injili ya Jumapili hii ni juu ya Yesu akigeuka sura huko mlimani na umaana wa kitendo hicho maishani mwetu. Mara kwa mara, sisi wanadamu hujaribiwa kuepuka shida zinazoambatana na wito wetu wa Kikristo. Badala ya kuzikabili twapendelea kuziepuka, ili tuwe na utulivu. Kama Mtk. Petro kwenye Injili, mara kwa mara tunaoja utukufu wa Mungu; wakati ambao tungetaka kujenga hema ili tukae starehe katika hali hiyo ya furaha; maisha ambayo hayana shida hata kidogo. Nyakati kama hizi hupita haraka, kama vile kugeuka sura kwa Yesu mlimani kuliwa kwa mda tu, na punde Mitume wakajikuta tena katika hali ya kawaida. Basi nasi pia tuwe tayari siku zote kukabiliwa na shida na majaribio kwenye safari yetu ya imani hapa duniani. Nyakati kama hizo, tukumbuke kwamba hapo mwisho taji ya utukufu yatungojea. Wale wanaomwamini Mungu na kumtumaini daima, siku moja hata wao watageuzwa sura na kuingia katika maisha ya milele mbinguni.

 Ujumbe wa masomo ya Jumapili hii hasa ni mambo matatu. 1) Tunaitwa tuache usalama wetu na utamaduni wetu tukimtumainia Bwana, ili atugeuze tuishi maisha mapya katika Kristo; 2) Katika dunia ya leo hasa sio sahisi kuishi ukristo wetu kwa sababu huenda marafiki wetu wakatuchekelea hasa tukiishi kulingana na amri za Mungu au za Kanisa, lakini tunaweza kwa neema ya Mungu; 3) Kwa sababu Yesu atupatia nguvu zake, tunaweza pia kuvumilia kuchukua msalaba wetu na kumfuata wakati huu wa Kwaresima, ili tuadhimishe vyema Pasaka Ya Bwana.


Shukrani Kwa Mtumishi Wa Bwana 
Mr.John M. Mbinda

Mchimba Riziki

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score