Thursday, April 24, 2014

Ukabila Huu Utaisha Lini Afrika? Cheki Kiongozi Mkubwa AliyeKataa Kujibu Swali La Mwanahabari kisa Ukabila...

Kiongozi wa chama cha Wiper aliye pia mmoja wa vinara wa Cord Kalonzo Musyoka alichemka na kukataa kujibu swali la mwanahabari kwa misingi ya jina lake la ukoo.
Kalonzo Musyoka Akimwomba Murethi Mwaandishi Wa
 Habari Msamaha baada ya kukataa kulijibu swali lake
Bw Musyoka alilazimika kutuma taarifa baadaye kuomba msamaha kwa kutoa matamshi hayo.

“Ilikuwa utani lakini nigependa kumwomba msamaha, pamoja na wanahabari wengine wote na mtu yeyote yule aliyeudhika na matamshi hayo,” taarifa hiyo iliyotumwa na msaidizi wake Dennis Kavisu ilisema.
Tukio hilo lililoshangaza wengi wakati wa kikao cha wanahabari kilichoandaliwa na muungano huo Nairobi kilipelekea Wakenya wa tabaka mbalimbali kueleza hasira yao katika mtandao wa kijamii wa Twitter.
Wakati wa mahojiano baada ya Cord kutoa ripoti yake kuhusu utawala wa mwaka mmoja wa Serikali ya Jubilee, mwanahabari wa runinga ya Q TV inayomilikiwa na Nation Media Group, Bw Kennedy Mureithi aliuliza ni kipi ambacho upande wa upinzani umefanya hadi sasa kushauri Serikali.
Mureithi: Yale ambayo mumekuwa mkisema ni kuhusu makosa ya Serikali ingawa hamjatoa mwongozo mbadala kama Cord. Hamsemi ‘hili ni baya, hili ndilo linafaa kufanywa’.  

Video Ndio Hii Hapa Chini


Musyoka: Kwanza sikupata jina lako.
Mureithi: Jina langu ni Kennedy Mureithi kutoka Nation Media, QTV.
Musyoka: Asante Kennedy…hilo jina limekusaliti kabisa…
Ingawa aliendelea kuongea, matamshi yake hayakusikika kutokana na kicheko cha baadhi ya waliokuwepo, pamoja na jinsi kaimu kiongozi wa ODM Anyang’ Nyong’o na mbunge wa Budalangi Ababu Namwamba walivyoingilia kati kwa haraka na kueleza swali hilo lilikuwa limeangaziwa tayari.
Hisia tofauti zilitolewa na Wakenya wa tabaka mbalimbali katika Twitter, ambapo wengi walimshutumu Bw Musyoka huku wengine wakionekana kutetea matamshi yake.
“Kwa kweli sina la kusema. Sijui hata nianzie wapi,” alisema mwanahabari mashuhuri wa runinga ya Citizen, Bi Julie Gichuru.
Mwanahabari mwingine, Bi Isha Chidzuga wa runinga KTN alisema, “Kuna sababu ya kuwepo kwa msemo ‘No comment’. Imenuiwa kukuokoa. Jikwae dole wala sio ulimi.”


Waliomtetea walisema Wakenya hujifanya tu kukemea ukabila ilhali wao wenyewe ni wakabila.
“Amen. Wanahabari pia walihusika kugawanya Kenya kikabila mbali na kuwa walituuza kwa chai na mandazi,” alisema Bi Noreen Auma kwenye Twitter.
Kwa upande wake, Geoffrey Nyambane alitaja yaliyokuwa yakiendelea mtandaoni kama kutotaka kutambua ukweli na akasema cha muhimu ni “kukabiliana na tatizo halisi ambalo ni ukabila Kenya.”
Kwenye kikao hicho, Bw Musyoka alitoa wito kwa Serikali ikabiliane na ukabila ambao ni tishio kwa umoja wa kitaifa.


0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score