Thursday, May 8, 2014

Watu Waliofariki Wazidi Kuongezeka Wafikia Watu 78 Ni kutokana na kunywa pombe yenye sumu

IDADI ya watu waliokufa
kutokana na pombe
haramu katika mtaa wa
mabanda wa Shauri Yako,
Embu mjini imepanda na
kufikia watu 39 baada ya
waathiriwa zaidi ambao
walikuwa wamelazwa
katika Hospitali ya Embu
Level Five kuaga dunia.

Meneja wa mawasiliano wa St John Ambulance Bw
Fred Majiwa alisema kuwa miili miwili bado
haijatambuliwa, na kwamba wakazi wa Embu
wamehimizwa kuwaripoti watu wote waliotoweka
katika dawati la St John Ambulance hospitalini
humo ambalo liliwekwa mahususi kushughulikia
mkasa huo.

Wagonjwa 73 wametengwa katika hospitali hiyo hadi
sumu iliyokuwa ndani ya pombe waliyokunywa
itakapojulikana.

“St John Ambulance ikishirikiana na Idara ya
Huduma za Jamii wameunda dawati la kutoa
msaada kuwatafuta watu waliotoweka na ule wa
kisaikolojia wa kuzipatia familia na manusura
ushauri nasaha,” alisema Bw Majiwa.

Sampuli za
pombe hiyo pamoja na mkojo na damu ya
waathiriwa imepelekwa maabara ya serikali
kwa ukaguzi.

Afisa mkuu wa matibabu hospitalini humo Dkt
Gerald Ndiritu alisema kwamba wanatarajia
kupokea matokeo kamili katika muda wa siku mbili.

Kufikia sasa, pombe hiyo haramu imepelekea vifo
vya angalau watu 78 katika kaunti tano.

Kaunti ya Embu ambapo watu 39 wamepoteza
maisha yao, ndiyo yenye idadi kubwa ya vifo.

Katika kaunti ya Makueni, takriban watu 18
wamekufa, ilihali wengine 10 wamethibitishwa kufa
mjini Limuru, kaunti ya Kiambu.

Kaunti za Kitui na
Murang’a zimerekodi vifo tisa na viwili mtawalia.

MURANG’A
WATU watano zaidi walifariki Jumatano baada ya
kubugia pombe yenye sumu katika kaunti ya
Murang’a, hivyo kufanya idadi ya walioangamia
katika eneo hilo kufika watu saba.

Wawili walifariki katika soko la Kirere, eneo bunge
la Kigumo baada ya kunywa pombe inayofahamika
kama 'Sacramento’.

Pombe hiyo ambayo imekuwa
maarufu miongoni mwa watumiaji wake kimetiwa
kwenye chupa za milimita 500.

Watu Wengine watatu
walifariki eneo la Kamucii.

Madaktari walikuwa na kibarua kigumu cha kutibu
idadi kubwa ya waathiriwa ambao walikuwa
wakisombwa na ambulansi huku wengine wakiletwa
na jamaa zao.

Magari ya ambulensi yalikuwa yakizuru kila kijiji
kubeba waathiriwa wa pombe hiyo.

Kamishna wa kaunti hiyo Bi Kula Hache alisema
maafisa wa polisi tayari wamekusanya sampuli za
pombe hiyo katika baa mbalimbali za Kigumo na
Maragua na kupelekwa katika kituo cha polisi cha
Kigumo ambapo inafanyiwa uchunguzi na maafisa
wa Shirika la Takwimu nchini na Mamlaka ya
Ukusanyaji Ushuru (KRA).

MAKUENI
Idadi ya watu waliofariki kutokana na pombe
haramu katika kata ya Kitise, Kaunti ya Makueni
imeongezeka kutoka 12 hadi 16 na waliolazwa
hospitalini kutoka 67 hadi 75.
Akizungumza na mwandishi wa Taifa Leo
Mkurungezi Mkuu wa afya Kaunti ya Makueni Dkt
David Kiuluku alisema kuwa idadi hiyo iliongezeka
baada ya maiti zao kupatika katika kijiji cha Kitise.

Kiuluku alisema kuwa waathiriwa wanane walifariki
wakitibiwa katika hospitali ya Makueni ilhali wengine
wanane walipatikana wamefariki katika vijiji vya
Kitise na Kanzokea.

Kiuluku alisema kuwa hospitali ya Makueni ilikuwa
na waathiriwa 75 na mmoja katika hali maututi na
watatu wakiwa vipofu.

Mmoja wa waliolazwa alikuwa mhudumu katika baa
ya Kasovo iliyo eneo la Kitise.

Mbithe Muthoka ambaye ndugu zake walikuwa
miongoni mwa waathiriwa alisema kuwa mamake
alikuwa amempigia simu baada ya watatu hao
kutoamka Jumatatu asubuhi.

Mmoja wa ndugu zake Munyao Muthoka alifariki
na wengine watatu wanapokea matibabu katika
hospitali ya Makueni.

Haya ndio madhara makubwa yaliyotokana na pombe yenye sumu iliyotengenezwa Nairobi katika mtaa wa Kariobangi North.

Swali ni jee kilipata wapi kibali cha kuingia sokoni? Je KRA hawakudhibitisha ubora ama kulikuwa na Ukora?

Mchimba Riziki itaendelea kuchunguza hayo yote na utayapata hapa hapa.

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score