Thursday, May 8, 2014

Abdulfatah al Sisi mwanajeshi Anayetaka Urais Misri.

Abdulfatah al Sisi mwanajeshi anayegombea katika uchaguzi wa rais wa Misri na ambaye siku hizi ndio gumzo la siku katika vyombo vya habari, amesema katika mahojiano na kanali ya CBC kwamba nchini Misri hakuna tena kitu kinachojulikana kama Ikhwanul Muslimin.

Al Sisi pia amejiarifisha kuwa ndiye mwakilishi wa wananchi wa Misri, na kwamba yeye si mgombea wa jeshi.

Wakati huo huo amesisitiza kuwa iwapo atashinda urais, Misri itashuhudia matukio mazuri.

Ingawa matamshi hayo yanaweza kutafsiriwa kuwa ya kampeni, lakini kutamka wazi jenerali huyo wa zamani wa jeshi kwamba harakati ya Ikhwanul Muslimin haina tena nafasi nchini Misri, kunaonesha kuwa atakabiliana vikali na wapinzani, suala linalokinzana na misingi ya demokrasia na uhuru wa kujieleza.

Wakati huo huo, makundi ya kutetea haki za binadamu nchini humou sambamba na kusema kuwa al Sisi anaungwa mkono na wanajeshi, yamesisitiza kuwa jeshi linazuia uhuru wa vyombo vya habari na wapinzani wa kisiasa.

Wananchi wa Misri bado hawajasahau kipindi cha miaka 30 ya kutekelezwa sheria ya hali ya hatari, iliyouwezesha utawala wa dikteta Hosni Mubarak kuwanyanyasa na kuwatia mbaroni wapinzani.

Pia tangu jeshi lilipompindua Rais Muhammad Mursi aliyechaguliwa na wananchi,

serikali ya mpito inayoungwa mkono kwa kiasi kikubwa na jeshi nayo pia inaendeleza mwenendo huo huo.  Serikali ya Misri kwa kuitangaza harakati ya Ikhwanul Muslim kuwa ni kundi la kigaidi,

harakati ambayo kwa muda wa mwaka mmoja ilitawala Misri, kivitendo imeonesha kuwa siasa zake ni kama za  utawala wa kijeshi wa Hosni Mubarak.

Moja ya sifa za watawala wa kijeshi wa Misri zilikuwa ni ukandamizaji na hivi sasa pia serikali ya mpito ya Cairo inaendeleza mwendo huo.

Jambo la kuzingatia hapa ni kuwa, al Sisi anajiona kuwa mwakilishi wa wananchi na sio jeshi.

Lakini kwa karibu miezi 10 iliyopita jeshi ndilo limekuwa likisimamia masuala ya Misri.

Kwa maelezo hayo ni wazi kuwa, hata kama Adil Mansour ndiye rais wa serikali ya mpito  lakini kivitendo nchi imekuwa ikiongozwa na jeshi.

Jenerali Abdulfatah al Sisi aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Misri ameingia katika kinyang'anyiro cha kugombea urais kwa kujivika vazi la kiraia, ili kwa mara nyingine aweze kuihusisha utawala wa kijeshi katika muundo wa kisiasa wa nchi hiyo.

Mwaka mmoja ambao Muhammad Musri aliongoza serikali ya Misri, ulikuwa ni wakati mgumu mno kwa wanajeshi waliokuwa wamezoea kudhibiti nguzo zote za kisiasa, kiuchumi na kiusalama.

Hata utawala wa Kizayuni, Marekani na madola ya Kiarabu ya pembezoni mwa Ghuba ya Uajemi pia yalionesha wasiwasi kutokana na Misri kuongozwa na utawala wa kiraia ulioletwa na kundi la Ikhwanul Muslimin.

Lakini baada ya jeshi kuipindua serikali ya Misri, wimbi la misaada ya kifedha na kisiasa ya Wamagharibi na serikali za Kiarabu lilianza kumiminika kwa serikali ya mpito ya wanajeshi.

Suala hilo linabainisha wazi kuwa, ushindi wa wanajeshi nchini Misri una umuhimu mkubwa  kwa nchi hizo za Magharibi na Kiarabu.

Lakini jambo lililo wazi ni kuwa, nchini Misri kila siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo malengo ya wanapambinduzi yanavyozidi kupewa mgongo huku jeshi likipiga hatua za kushika madaraka.

Hali hiyo ina maana kuwa, utawala wa kijeshi unakaribia tena kuasisiwa nchini humo suala linaloashiria uwezekano wa kuanza tena uasi, upinzani na machafuko mapya katika nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score