Thursday, August 29, 2013

Podolski Atia Dosari Sherehe Za Arsenal Kufuzu Kuingia Hatua ya Makundi

LONDON, Uingereza
SHEREHE za Arsenal baada ya kufuzu kwa kabumbu ya Ulaya, Uefa zilitiwa dosari kufuatia jeraha la straika wao, Lukas Podolski. Mjerumani huyo alitolewa nje katika mechi ya mkondo wa pili ya raundi ya kufuzu kwa dimba hilo dhidi ya Fenerbahce ambapo walishinda 2-0. Podolski alifunga bao katika mkondo wa kwanza wiki jana ambapo walishinda 3-0 na sasa vijana hao wameingia hatua ya makundi kwa jumla ya mabao 5-0. Alitolewa nje kwa machela katika dakika za mwanzo za kipindi cha pili na atakosa mechi zijazo katika Ligi Kuu ya Uingereza. Kushinda mechi hiyo na kujikatia tiketi ya kabumbu ya Uefa kunapunguzia presha kocha wa Arsenal, Arsene Wenger ambaye amekuwa akishurutishwa na mashabiki kuwanunua wanasoka wapya. Kocha huyo alieleza wasiwasi wake kuhusu mfungaji wa bao katika mechi hiyo, Aaron Ramsey ambaye alimaliza akihisi maumivu kwenye kiuno huku kiungo matata, Jack Wilshere akigongwa kwenye mguu wake katika dakika za mwisho za mechi. “Hizo ndizo habari za kusikitisha usiku huu kwani licha ya kushinda, tumegharamia kwa kumpoteza Podolski kwa jeraha. Sijui kiwango cha jeraha la Ramsey na jinsi Wilshere atakavyopata nafuu na itabidi kuwachunguze zaidi,” Wenger alisema. Zimwi hili la majeruhi limewaandama wanasoka wa Arsenal mara nyingi, pia katika msimu uliopita majeruhi walikuwa wengi katika mwanzo wa Ligi kilichopelekea Arsenal kufungwa magoli mengi katika mzunguko wa kwanza..

Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score