Thursday, August 29, 2013

WATU WALIOFARIKI DUNIA KWA AJALI YA NAROK WAFIKA 41

WATU 41 wamefariki na wengine wengi kujeruhiwa baada ya basi lililokuwa likielekea Homabay kutoka Nairobi kuanguka na kubingiria mara kadha karibu na mji wa Narok. Kwa mujibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu watu wengine 33 walijeruhiwa na wakakimbizwa hospitali ya wilaya ya Narok. Ajali hiyo ilitokea eneo la Ntulele mwendo wa saa saba usiku. Miongoni mwa waliofariki ni watoto wanne. Kamanda wa Polisi wa Trafiki Samuel Kimaru alisema eneo hilo ni hatari na ajali hutokea mara kwa mara. Alisema serikali imekuwa ikiweka alama za kutahadharisha watu lakini alama hizo huibiwa na watu na kuuzwa kama vyuma vikuu kuu. Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga ameeleza kuhuzunishwa kwake na habari za ajali hiyo na kutuma rambirambi kwa jamaa za waliopoteza maisha. “Nawapa heko polisi na maafisa wa kutoa huduma za dharura kwa kasi yao katika kufika na kusaidia walionusurika, ” alisema kupitia akaunti yake kwenye Twitter. Katibu wa Baraza la Mawaziri Francis Kimemia pia alituma rambirambi zake na kusema “sheria lazima itekelezwe kikamilifu.” Mungu azilaze mahali pema peponi marehemu wote Na awaponye haraka majeruhi. Amen. Endelea kufuatilia muda baada ya muda tutaripoti kila tukipata taarifa zaidi.

Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score