Saturday, May 24, 2014

Tutaongeza Mashambulizi Zaidi Kenya "Ni Faud Mohamed Khalaf" Kiongozi Wa Kundi Haramu La Al-shabab Ameyasema hayo


Kwa mara nyingine kundi la Al Shabaab limeahidi kushambulia Kenya ili kulipiza kisasi kufuatia hatua ya majeshi Kenya kushambulia ngome zake Somalia.
Wapiganaji Wa Kundi La Al-Shabab
Katika kanda ya suati iliyotolewa Alhamisi, mmoja wa viongozi wakuu wa kundi hilo Fuad Mohamed Khalaf alisema magaidi hao wataendesha mashambulizi makali nchini Kenya.

“Tumehamishia vita Kenya, wakiua msichana wa Kisomali tunaua msichana wa Kenya,” alisema Khalaf katika kanda iliyopeperusha na radio ya Andalus.
“Tunatoa wito kwa Waislamu wote nchini Kenya kupigana na serikali ya Kenya ndani ya taifa hilo kwa sababu waliua watu wengi wakiwemo watoto,” alisema.
Majeshi ya Kenya ambayo yaliingia Kusini mwa Somalia 2011 kuzima shughuli za waasi hao, yamejiunga na wanajeshi 22,000 wa Umoja wa Afrika kukomesha oparesheni za kundi hilo la Al-shabab.
Mapema wiki hii majeshi ya Kenya yalishambulia maeneo ya Jilib katika misururu ya mashambulizi yanayoendeshwa na majeshi hayo.
“Wakati maafisa na ndege zao za kivita zinapoua watu wenu, Mungu amewapa idhini ya kulipiza kisasi hivyo tutapigana vikali na Kenya,” alisema Bw Khalaf ambaye anasemekana kuwa na cheo cha pili katika kundi hilo baada ya kiongozi mkuu Ahmed Abdi Godane.
Kundi la Al Shabaab, ambalo lilikiri kuhusika katika shambulizi la Westgate mnamo Septemba 2013 ambapo watu 67 walikufa, limehusika katika misururu ya mashambulizi mengine nchini.
Waasi hao wa Kislamu pia wamekiri kuhusika katika mashambulizi yalioua maafisa kadhaa wa Kenya Jumatatu katika eneo la Mandera.

wengi zaidi wapokea mafunzo ya al-shabab

Kulingana na shirika la AFP Bw Khalaf alisema watu zaidi wamepewa mafunzo na wanachama wa Al Shabaab na kuwa kundi hilo litatuma maafisa zaidi kuendeleza mashambulizi Kenya.

“Tumetoa mafunzo kwa watu ambao ndio walivamia maafisa wa usalama huko Mandera,” alisema na kuongeza kuwa waasi zaidi watatumwa Kenya.
Serikali ya Amerika imetoa tuzo la Dola 5 milioni kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazopelekea kukamatwa kwa Bw Khalaf ambaye ana asili ya Somali na Uswidi na anasemekana kuwa mfadhili mkuu wa kundi hilo.

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score