Gaza On Fire |
Familia nyingi za Kipalestina zimekimbilia katika shule hizo za Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kulinda maisha yao mbele ya mashambulizi ya kinyama yanayofanywa na jeshi la Israel dhidi ya watu wa Ghaza. Shule hiyo ni ya tatu ya Umoja wa Mataifa kushambuliwa na jeshi la Israel katika mashambulizi ya sasa ya utawala huo haramu katika Ukanda wa Ghaza. Makumi ya wengine wamejeruhiwa.
Habari zinasema kuwa zaidi ya Wapalestina 150 wameuawa shahidi katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Ghaza katika mashambulizi ya jana ya jeshi za Israel. Jeshi la Israel linashambulia kwa makombora taasisi za kiraia na kijamii kama shule na vituo vya elimu, misikiti na makanisa, hospitali, vituo vya umeme na maji na kadhalika.
Gaza On Fire |
Ni wiki tatu sasa ambapo wakazi wa Ghaza wanakabiliwa na mashambulizi makali ya nchi kavu, baharini na angani ya jeshi la Israel ambalo halikuwaonea huruma hata watoto wadogo, wanawake wajawazito, wazee na vikongwe.
Ndege za kivita za Israel na walenga shabaha wa utawala huo ghasibu wamekuwa wakiwashambulia watoto wadogo wa Palestina wanaoonekana wakicheza mitaani. Matukio haya, kama yanavyosisitisza mashirika ya kutetea haki za binadamu, ni kielelezo cha jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu.
Hadi kufikia leo Wapalestina karibu 1290 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 7115 wamejeruhiwa katika siku 23 za mashambulizi ya kinyama ya utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Ghaza.
Raia wa Ghaza ambao wako katika mzingiro wa pande zote wa Israel kwa kipindi cha miaka saba sasa wanakabiliana na utawala huo katili kwa kila walichonacho huku silaha ya watoto wadogo na wanawake ikiwa ni machozi na mayowe. Maeneo yote ya Ghaza yamejaa damu za mashahidi wanaouawa huku karibu kila nyumba ikiwa katika maombolezo ya ndugu, jamaa au rafiki.
Jambo la kusikitisha zaidi kuhusu matukio ya sasa ya Ghaza ni kimya cha jamii ya kimataifa hususan nchi za Ulaya na Marekani ambazo zimekuwa zikijigamba kuwa wabeba bendera ya kutetea haki za binadamu. Nchi za Magharibi hazikuishia katika kunyamaza kimya mbele ya mauaji hayo ya kutisha yanayofanywa na utawala katili wa Israel huko katika Ukanda wa Ghaza, bali zinausaidia utawala huo wa kigaidi kwa silaha zaidi. Kwa kweli yanayotokea Ghaza ni maafa makubwa ya binadamu ambayo doa lake jeusi litabakia milele katika uso wa historia ya mwanadamu.
Ghaza ya leo ni mtihani mgumu kwa Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama, taasisi za kimataifa na nchi zote zinazodai kutetea haki za binadamu zinazoendelea kunyamaza kimya na kushuhudia kwa macho tu jinsi watu wa Ghaza wanavyochinjwa na mashine ya vita ya Israel.
Katika mazingira hayo linajitokeza swali kwamba je, raia wa Ghaza si wanadamu kama wengine wanaopaswa kudhaminiwa usalama na amani? Je, ni jumuiya na taasisi gani zinazopaswa kuwadhaminia usalama na amani? Ni nini majukumu ya wajibu wa Umoja wa Mataifa la Baraza lake la Usalama katika hali ya sasa ambapo watoto wadogo wasio na dhambi na wanawake wa Ghaza wanaendelea kuchinjwa na kuuawa kama wadudu wasio na thamani?
0 maoni:
Post a Comment