Wednesday, July 30, 2014

SHUJAA ALIYEAMBUKIZWA UKIMWI KULIPWA KSH MILLIONI 653........

Mwathiriwa mmoja wa bomu la 1998 atapata Sh652.5 milioni kama fidia baada ya kuambukizwa virusi vya HIV akijaribu kuwaokoa manusura katika shambulizi hilo la kigaidi.

William Maina alikuwa akichokoa vifusi vya jengo la Ubalozi wa Amerika, ambalo liliharibiwa kabisa na shambulizi hilo.


Alishuhudia mbele ya mahakama moja ya Amerika kwamba alikuwa akifanya kazi kando na ubalozi huo wakati wa shambulizi, na alikimbia eneo la mkasa kusaidia katika juhudi za uokoaji.
Ni katika shughuli hizo za kuwasaidia wahasiriwa ambapo alipata majeraha na mikwaruzo iliyofanya damu yake kuchanganyika na ya wahasiriwa.
Bw Maina baadaye alipatikana kuwa na virusi vya HIV ambavyo husababisha ugonjwa wa Ukimwi. Alitoa ushahidi mahakamani kuonyesha hakupata ugonjwa huo kwingine.
“Ingawa alikuwa na majeraha madogo tu ya kimwili wakati wa juhudi za uokoaji, HIV ni ugonjwa sugu, hatari na wenye kusababishia mtu fedheha unaohitaji matibabu ya maisha,” Jaji wa Amerika John Bates alisema katika uamuzi wake.
Mwathiriwa mwengine Jael Oyoo pia alifidiwa. Bi Oyoo alitolewa kwenye vifusi na waokoaji na alipata majeraha mabaya ya moto usoni na kichwani. Waokoaji walidhania alikuwa amefariki.
Kadhalika, alipoteza uwezo wa kuona katika jicho lake la kushoto na kuathiri mno kuona katika jicho la kulia. Alikuwa hospitalini kwa miaka miwili.
Wawili hao ni miongoni mwa waathiriwa wa shambulizi hilo la bomu dhidi ya ubalozi wa Amerika mjini Nairobi, waliofidiwa baada ya kupata majeraha mabaya.
Waliopoteza waume au wake zao watapata kiasi cha hadi Sh696 milioni. Wengine watapewa Sh609 milioni.

Katika uamuzi wake, Bw Bates alitoa Sh435 milioni kwa waathiriwa wa majeraha mabaya ya kimwili, kwa mfano kuvunjika sehemu za mwili, maumivu ya nyama na makovu pamoja na waaathiriwa wa kisaikolojia.

Iwapo uchungu wa kimwili na kisaikolojia ni mwingi sana – kama waathiriwa waliopata majeraha mengi na mabaya na waliopoteza uwezo wa kuona na kusikia ama waliodhaniwa kuwa wamefariki – mahakama imetoa hadi dola milioni saba (Sh609 milioni) na zaidi,” Bw Bates alisema katika kesi iliyowasilishwa na Milly Mikali na wengine.
Walikuwa wameshtaki Jamhuri ya Sudan kwa shambulizi hilo la kigaidi.
Lakini kwa waliopoteza wake au waume zao, Jaji alisema watapewa Sh696 milioni kama fidia ya wapenzi wao waliopoteza maisha.
Aidha, kwa waathiriwa waliopata majeraha ya kiakili kuandamana na majeraha madogo ya kimwili, Jaji aliamua watalipwa kati ya Sh130 milioni na Sh261 milioni. Kwa waliokuwa na majeraha kwa saa kadha, watapata fidia ya Sh87 milioni.
Iwapo kipindi cha maumivu ni kidogo atapata pesa kidogo. Kwa mfano, aeleza jaji, waliokuwa na majeraha kwa dakika 10 watapata Sh43 milioni.

Source Taifa Leo

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score