Tuesday, July 22, 2014

Saratani Ya Koo Na Tumbo Husababishwa Na Pombe Za Kienyeji Kama Busaa.

Wazee wakifurahia Busaa Picha kwa Hisani Ya Nation Mediu Group
Wanasayansi wameitaka kuangazia unywaji busaa wakisema unachangia pakubwa ongezeko la visa vya saratani ya koo.
Ripoti hiyo inasema ingawa kinywaji hicho ni maarufu sana hapa nchini katika jamii mbalimbali utumiaji wa mahindi, mawele na mtama au mhogo ulioharibika kutengeneza busaa unachangia pakubwa katika kuwapa sumu wanywaji ambao mwishowe hupata magonjwa mbalimbali ukiwemo saratani ya tumbo na koo.

Wanasayasi watatu kutoka Chuo Kikuu cha Kiteknolojia cha Jomo Kenyatta(JKUAT), mmoja kutoka Chuo Kikuu cha Chiba kule Japan na mwingine kutoka Kituo cha Utafiti wa Maswala ya Afya (KEMRI) wanasema udadisi umeonyesha kemikali zinazochangia usambazaji wa saratani zinapatikana katika pombe iliyonunuliwa katika vituo mbali mbali vya vileo kule Bomet.
Wadadisi waligundua kuwa wagema wana mazoea ya kutumia mahindi yaliyooza ambayo huuzwa kwa bei ya chini na wauzaji na hivyo kufanya wanywaji pombe kupata sumu iliyo ya hali ya juu.
“Kuna haja ya kutumia mahindi masafi na bidhaa nyingine katika kutengeneza pombe lakini mambo yalivyo, tunaona wagema wakipendelea kutumia mahindi yaliyooza na kutengeneza busaa ambayo baadaye hupewa wanywaji katika sherehe za mazishi, harusi, ulipaji mahari na wakati wa kutahiriwa kwa wavulana,” ikasema ripoti hiyo.
“Kemikali hizi humfanya mnywaji kupoteza uzito, kutapika mara kwa mara na pia kuhara. Lakini baada ya muda mrefu, mwili hupoteza uwezo wake wa kuzuia magonjwa na mtu akapata saratani ya koo au matumbo,” ikasema ripoti hiyo.

Hali ya wabugiaji pombe huwa mbaya zaidi kwani wao hunywa hapa na kisha kunywa pale na hii inawafanya kuwa hatarini ya kunywa sumu aina mbalimbali na hivyo kuhatarisha maisha yao zaidi.
Inaonya kuwa wagema wengine sasa wameanza kutumia chakula ya mifugo ambacho kina sumu kali na hivyo kufanya wanywaji kunywa mvinyo wenye sumu aina mbali mbali.
Wanasayansi hao, Mary Kirui, Amos Alakonya na Keith Talam-wote kutoka Chuo cha JKUAT ,Bi Christine Bii(KEMRI) na Gonoi Tohru wa Chiba wanaamini kuna haja ya serikali kuangalia ubora wa Busaa mara kwa mara ili kuinua hali ya wabobeaji pombe.

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score