Dar es Salaam.
John Heche Mwenyekiti Bavicha Taifa |
Viongozi wote wa juu wa sasa wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) hawatagombea nafasi yoyote katika baraza hilo kutokana na umri wao kuzidi miaka 30.
Kwa mujibu wa katiba ya Bavicha, mgombea wa nafasi yoyote anatakiwa asiwe na umri wa zaidi ya miaka 30.
Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche alisema jana kuwa yeye, Katibu Mkuu wake, Deogratius Munishi na Naibu Katibu Mkuu, Ester Daffi hawatagombea nafasi yoyote kutokana na umri walionao... “Hii ina maana kuwa baada ya uchaguzi, tutaachia madaraka na kuendelea na shughuli nyingine za chama.”
Alisema ili kuepuka udanganyifu hususan wa umri miongoni mwa wagombea wengine katika nafasi mbalimbali za baraza hilo, watahakikisha wanasimamia suala hilo kwa umakini mkubwa.
Heche alisema uchaguzi wa Bavicha katika ngazi ya taifa utafanyika Septemba 10, mwaka huu na fomu zitaanza kutolewa kuanzia Agosti 10 hadi 25 mwaka huu.
Alisema nafasi zitakazogombewa katika uchaguzi huo ni mwenyekiti, makamu mwenyekiti bara na Zanzibar na katibu mkuu.
Nyingine ni naibu katibu mkuu bara na Zanzibar, mratibu mhamasishaji taifa, mweka hazina na wajumbe watano wa kuwakilisha kwenye baraza kuu la chama na wajumbe 20 wa kuwakilisha vijana kwenye mkutano kuu wa chama hicho.
Rushwa
Akizungumzia suala la rushwa katika uchaguzi, Heche alisema uongozi unaomaliza muda wake umejipanga kudhibiti vitendo hivyo ili kuzuia wasaliti kujipenyeza.
Alisema kuna baadhi ya watu wamejipanga kutoa rushwa ndani ya baraza hilo ili kushinda nafasi mbalimbali kwa lengo la kuivuruga Chadema baadaye na kuidhoofisha.
Alisema chama hicho kitawawinda wagombea hao na kuwafisha katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ili wachukuliwe hatua za kisheria na baadaye kufutwa uanachama.
Mwaka 2011, Bavicha ilifanya uchaguzi ambao ulitawaliwa na mizengwe na vurugu hadi kusababisha kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea.
Mwananchi Source
0 maoni:
Post a Comment