Friday, November 29, 2013

Dini Isiyoamini Dawa Yeyote Iliyotengenezwa Na Mwanadamu, wanaamini Maombi Ya Dini Yao, Fuatili Hapa Ndani

TANGU 1977, Mzee Kavulu Musembi hajawahi
kutumia dawa ama hata kushika dawa na
mikono yake japo amekuwa akiugua mara kwa
mara.
Hii ni kwa sababu ya imani yake kuwa
Mungu ndiye mponyaji pekee na hana imani na
vitu vilivyotengenezwa na binadamu kama vile
dawa.

Mzee Kavulu ni mmoja wa waumini wenye imani
kali wa dhehebu la Kavonokya katika eneo la
Mwingi, Kaunti ya Kitui.
Bw Kavulu, ambaye
alijiunga na Kavonokya
akiwa kijana wa umri
mdogo mnamo 1976,
anasema kulemewa na
ugojwa ndio kulimfanya
ajiunge na dhehebu hilo.

“Nilipatwa na ugonjwa
mbaya na nikapelekwa na ndugu yangu Nairobi
kupata matibabu.
Nililazwa hospitalini kwa wiki
kadha bila nafuu yoyote na wakati mmoja
nikaona maisha yangu yamefika mwisho.

Baada
ya kurudi nyumbani nilifanyiwa maombi na
waumini wa Kavonokya na nikapona kabisa,”
alieleza Mzee Musembi.

Wazazi wa Mzee Musembi walikuwa wanaamini
tamaduni za jamii ya Wakamba hivyo alikuwa
wa kwanza katika familia yao kujiunga na
dhehebu hilo.

“Sijawahi kupeleka watoto wangu sita hospitalini
tangu wazaliwe na sasa ni watu wazima na
baadhi yao wana shahada za digrii kutoka vyuo
vikuu,” alisema.

Alisema watoto wake wote walizaliwa nyumbani
na hawajawahi kupata chanjo hata moja hata
baada ya kuugua ukambi.

Kwa miaka mingi wafuasi wa dhehebu la
Kavonokya wamekuwa wakikabiliwa na utata
kuhusu imani yao ya kususia matibabu kwa
madai kuwa wanaamini uponyaji hutoka kwa
Mungu pekee na wala si kutokana na matibabu
ya hospitalini.

Baadhi ya vijiji katika wilaya ya Mwingi Mashariki
vimedhibitiwa na waumini wa Kavonokya ambao
wanakutana kila siku ya Jumapili sawa tu na
Wakristo wengine kwa ibada.

Waumini wa dhehebu la Kavonokya mara kadha
wamegonga vichwa vya habari katika mzozo wao
na maafisa wa afya wakitakiwa kupeleka watoto
wao kupata chanjo.

Bw John Kasembei ambaye ni mfuasi wa
dhehebu hilo kutoka eneo la Mwingi anaeleza
kuwa walioanzisha vuguvugu hilo miaka ya
hamsini walikuwa na ushuhuda wa pamoja wa
jinsi Mungu alivyowaponya kutokana na maradhi
tofauti tofauti ambavyo binadamu hangeweza.

“Ni kutokana na neno la Kikamba 'vonokya’
kumaanisha kuokolewa ambapo walitoa jina
'kavonokya’,” anasema Bw Kasembei.

Wafuasi wa dhehebu hili hutambulika kwa imani
yao kali ambayo wanasema inawatofautisha na
waumini wa madhehebu mengine.

“Mimi
nimejaribu kuwa muumini wa makanisa
mengine lakini ni katika dhehebu la Kavonokya
ambapo kuna imani ya kweli.

Hautawahi kusikia
waumini wetu wakiwa na mizozo kama
makanisa haya mengine,” alielezea Bw
Musembi.

Waumini wanawake wa Kavonokya hutambulika
kwa marinda yao marefu na kujifunga vitambaa
kichwani.
Mavazi yao yanafanana na yale ya wafuasi wa
dhehebu la Akorino lakini wanaume hawajifungi
vitambaa kichwani.

Bw Kasembei anaeleza kuwa mavazi yao
yanatokana na mafunzo ya Biblia kuwa
mwanamke afunike kichwa chake haswa wakati
wa ibada.
“Kulingana na kitabu cha Wakorintho
wa kwanza katika mlango wa 11, Biblia imeeleza
mwanaume ndiye kichwa cha jamii na hivyo
kutaja jinsi kichwa cha mke kinafaa kunyolewa
au kufunikwa kama ishara ya unyenyekevu,”
alielezea.

Marinda yao marefu yaliyo na mikunjo ni
kuhakikisha kuwa mwanamke anaficha uchi
wake na havai rinda linaloonyesha umbo lake
hata wakati wa upepo, rinda hilo linamsitiri
vilivyo.

Wakati kunapozuka maradhi ya watoto haswa
ugonjwa wa kupooza na ukambi inawalazimu
maafisa wa afya kwa ushirikiano na maafisa wa
usalama na viongozi wa eneo hilo kuwashinikiza
kwa lazima waumini wa dhehebu hilo
kuwapeleka watoto chanjoni.

Chifu wa wa eneo hilo la Endui katika wilaya ya
Mwingi ya Kati, Bw Samuel Maithya anasema
mara nyingi inambidi kuwachukua watoto
wanaougua kwa lazima na kuwapeleka kupata
matibabu.

“Mwaka jana watoto kadhaa ambao wazazi wao
ni wafuasi wa kavonokya walipoteza maisha yao
wakati ugonjwa wa ukambi ulipochipuka katika
eneo hili,” asema Bw Maithya.

Waumini hao huamini kuwa imani yao huponya
hata magonjwa yasiyokuwa na tiba ya
kimatibabu.

“Hakuna pahali katika Biblia ambapo Wakristo
walienda hospitalini. Walikuwa wakiponywa na
Yesu mwenyewe au katika maziwa kama lile la
Bethsaida ambapo malaika alikuwa akishuka na
kukoroga maji ili mgonjwa wa kwanza kuingia
majini apone,” alielezea Bw Musembi.

Kulingana na mafunzo ya dhehebu hili, watu
hupata magonjwa kwa sababu ya mambo
matatu:
Majaribu ya kupima imani ya Mkristo,
njia ya Mungu kuadhibu Mkristo kwa maovu
yake au njia moja ya Mungu kumpumzisha mtu
kama siku zake za kuishi zimeisha duniani.

Waumini hawa huamini kuwa dawa si mwisho
wa magonjwa duniani na kuwa cha muhimu ni
mtu kuwa na imani na kupata uponyaji wa bure
kutoka kwa Mungu.

“Iwapo ni kweli matibabu
ya dawa yanaweza kuponya magonjwa, ni kwa
nini hospitali huwa na vyumba vya kuhifadhi
maiti?,” alishangaa muumini mmoja.

Wafuasi hawa wanasema watashikilia imani yao
hata serikali ikiamuru watoto wapewe chanjo.

Wanaamini kuwa siku ya mtu kufariki ifikapo,
hata dawa zinazoaminika kuwa bora zaidi
haziwezi kuzuia kifo.

Bw Kasembei anasema kuwa ugonjwa wa
Ukimwi ni dhibitisho kamili kuwa mwanadamu
hawezi kutengeneza dawa za kuponya magonjwa
yote.

“Wagonjwa wa Ukimwi humlilia Mungu
awaponye kwani hata dawa za kupunguza
makali yake haziwezi kuponya ugonjwa huo,”
akasema.

Anasema wao hutambua magonjwa kama pepo
mbaya inayowajia wanadamu na kuwa dawa ni
vitu vilivyotengenezwa na wanadamu kutumia
akili yao na si kitu kitakatifu mbele ya Mwenyezi
Mungu.

Waumiwa hao walisema kuwa idadi
ya watoto wao wanaofariki kutokana na
michipuko ya maradhi kama ukambi ni ndogo
mno ikilinganishwa na ile ya watoto wanaopona
baada ya kufanyiwa maombi katika dhehebu
hilo.

Bw Kasembei amekuwa katika kazi hii ya
kuhubiri sehemu mbalimbali na anasema kuna
wafuasi katika maeneo mengine nchini.

“Nimehubiri na kubatiza watu katika mji wa
Eldoret, Nairobi, Kati, Eldama Ravine, Busia,
Marachi, Ahero na Kisii ambapo wote huamini
Kavonokya.”

Ibada

Kavonokya hukutana siku ya Jumapili kwa ibada
yao sawa tu na Wakristo wengine duniani.

Wafuasi hawa hutumia Biblia ya kawaida
inayosomwa na Wakristo wengine.

Maombi
hufanywa kwa pamoja huku kila mmoja akiwa
amepiga magoti.

Cha kushangaza ni kuwa waumini hawa
hawafanyii ibada zao katika makanisa. Wao
hukutana katika boma za washirika wao.

Waumini hawa wanasema hatua ya kutokuwa na
makanisa ni kwa sababu hawataki washirika
wake kutumia pesa zao kwa ujenzi wa makanisa.
Wanaamini kwamba kanisa ni roho ya mtu.

Wakati wa ibada wanawake na wanaume
hawatangamani kwani kila jinsia inakaa upande
wake. Vilevile wanawake hawakubaliwi kuongea
au kutoa mafunzo yoyote wakati wa ibada.

Masomo yote ya Biblia pamoja na mahubiri
hufanywa na wanaume pekee. Wakati wa
kuimba pekee ndio wanawake wanakubaliwa
kusimama na kuimba kwa pamoja na pia wakati
wa maombi.

Jambo hili la wanawake kukaa kimya wanasema
ni kulingana na kitabu cha Wakorintho wa pili
mlango wa 14 ambapo wanawake wanatakiwa
kukaa kimya na kuacha wanaume kuongoza
ibada.

Dhehebu hili halina wahubiri au kiongozi yeyote,
kila mfuasi wa kiume ana uhuru wa kuhubiri
neno alilopewa na Mungu.

Sherehe za ndoa huongozwa na mwanaume
yeyote aliyekomaa miongoni mwa waumini hao.
Kinyume na Wakristo wengine duniani , waumini
wa Kavonokya hawavalishani pete wakati wa
harusi na vilevile hakuna cheti chochote cha
harusi kwa wanaooana.

Wanasema pete na vyeti hivyo hutolewa na
madhehebu yale ambao yamejaa unafiki wa
kukubali talaka miongoni mwa waliooana.

“Hatuhitaji pete au cheti chochote kwani Mungu
ndiye shahidi mkuu wala hatuna hofu ya watu
kutengana baada ya kuoana,” akasema muumini
mmoja.

Waumini hawa pia hawatumii vitabu vya nyimbo
wakati wa ibada na huimba kwa pamoja bila
mtu yeyote kuongoza.
Vilevile wafuasi hawa huimba bila ala za muziki
zozote na hucheza kwa kuruka juu huku
wakipiga makofi.

Hawatoi sadaka yoyote wakati wa ibada au hata
kutoa fungu la kumi. Wanaamini kuwa hakuna
haja ya kumtolea Mungu asilimia kumi huku
mtu akibaki na asilimia tisini kwa matumizi yake
binafsi. Badala yake wao hutumia asilimia
kumi na kutenga asilimia tisini kwa kazi ya
kuhubiri neno la Mungu, kusaidia maskini na
watoto yatima.

Bi Nzakya Mutava ni muumini wa Kavonokya
anayeishi katika eneo la Mwingi. Anasema
alikuwa na shida ya kuzaa watoto na kufariki
wakiwa na umri mdogo bila kuugua.

Bi Nzakya
anasema alipoteza watoto wanne katika hali hiyo
na kuamua kuomba na wafuasi wenzake kabla
ya kupata mimba ya mtoto wa tano.
“Tuliomba kwa muda mrefu hata wakati
nilipokuwa na mimba ya mwanangu wa tano na
alipozaliwa tukazidi kuomba, hivi sasa nina
watoto wanane na wote wana afya njema,”
akasema.

Bi Mwalale Ngui anasema hapo mwanzoni
hakutaka kuhusishwa na dhehebu la Kavonokya
kwani hakuamini mwanadamu angeishi bila
kupata matibabu hospitalini.

Mambo yalimgeukia alipougua maradhi ambayo
hayakuweza kutambuliwa na madaktari.

“Nilitumia mali yangu yote nikijaribu kupata
uponyaji hadi nilipoishiwa ndipo niliamua
kujiunga na Kavonokya,” akasema.

Mchimba Riziki

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score