Sunday, December 22, 2013

HAWAJALI GHARAMA KUBWA ZA SMARTPHONE BALI WANACHOJALI NI MAWASILIANO

Licha ya gharama kubwa za awali za kununua smartphone, Wasomali wanaongezeka katika kulipia kutokana na faida za kuunganishwa papo hapo na intaneti, kunakorahisisha mawasiliano na wanafamilia walio nje ya nchi na kupata habari na taarifa kwa urahisi na kwa gharama nafuu kuliko njia iliyokuwa imezoeleka ya kupata intaneti.

"iPhones ya gharama kubwa kabisa ni dola 800, wakati [simu] Samsung ziliuzwa kwa dola 500, ingawaje zipo baadhi ambazo zinagharimu zaidi," alisema Faisal Abdullahi mwenye umri wa miaka 34 ambaye anamiliki duka la kuuza simu za mkononi katika soko la Hamar Weyne huko Mogadishu. Smartphone ya gharama ndogo kabisa iliuzwa kwa dola 250, alisema.

Uuzaji wa smartphone umeongezeka kwa haraka, Abdullahi alisema, akinukuu kwamba duka lake liliuza smartphone 12 mwaka 2012, na takriban 100 mwaka huu.

Abdullahi alisema wateja wake wengi wanaulizia smartphone, hususani simu za mkono za Samsung, ambazo zinafahamika sana kwa sababu ni bei rahisi kuliko iPhone na zina programu za bure zaidi.

"Baadhi ya simu hizi ni ghali sana ingawaje kwa sasa zinauzwa kwa gharama nafuu kidogo kuliko zilipokuja kwa mara ya kwanza ," alisema. "Unaweza kuona nyingine ni ghali sana, lakini tunaziuza kila mara."

Gharama ndogo za matumizi ya data:

Abdisalam Warsame, mwenye miaka 20 mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Djibouti katika wilaya ya Wadajir, alisema alimshukuru dada yake aliyeko Saudi Arabia ambaye alimtumia fedha kununua smartphone miezi nne iliyopita.

"Nilizoea kwenda katika mgahawa wa intaneti ambao unatoza shilingi 18,000 za Somalia kwa saa wakati nilipohitaji kutumia intaneti, na inawezekana kuihitaji mara kadhaa kwa siku,. "Sasa ninalipa dola 1 (shilingi 20,000) kwa zaidi ya saa 24 katika smartphone yangu."

Kwa upatikanaji wa intaneti katika simu yake ya mkononi, Warsame alisema sasa anaweza kuwasiliana na nchi nyingine duniani wakati wote.

Vivyo hivyo, mkaazi wa Mogadishu mwenye miaka 32 Yusuf Ibrahim alisema amekuwa mtumiaji wa mara kwa mara wa intaneti katika simu ya mkononi kwa miezi mitano iliyopita.

Alisema huduma hii imefanya iwe rahisi kwake kuendelea kuwasiliana na wanafamilia wake wanaoishi Finland.

"Ninawasiliana na mke wangu na watoto katika WhatsApp kila siku," Ibrahim alisema . "[Ninahisi] kama vile niko pamoja na wao, na ni nafuu kuliko kuongea nao moja kwa moja. Nilikuwa nalipa zaidi ya dola 50 hapo kabla kuongea nao tu, lakini sasa ninatumia chini ya dola 10 kwa mwezi, ingawa nawasiliana nao kila saa."

Abdirashid Hussein mwenye umri wa miaka 35, mfanyakazi wa kampuni ya intaneti na simu za mkononi ya Hormuud Telecom, alisema 1 gigabyte (GB) ya data ya intaneti inagharimu dola 25, na muda itakayodumu inategemea matumizi ya mtu.

Licha ya Hormuud, Somtel iliyoko Hargeisa ni kampuni nyingine pekee inayotoa huduma ya intaneti kupitia simu za mkononi huko kusini mwa Somalia.

Aweys Abdirahman, mwenye umri wa miaka 23 mwanafunzi katika Shule ya al-Imra katika wilaya ya Hodan Mogadishu, alisema simu za kisasa zinarahisisha kwa Wasomali kuwa wameunganishwa, ingawaje wakosoaji wanasema kwamba vijana wanatumia muda wao mwingi kwenye smartphone zao.

Somalia iko nyuma sana katika suala la upatikanaji wa intaneti, hata hivyo, ongezeko la matumizi ya intaneti ya simu ya mkononi ya gharama nafuu inasaidia kuziba pengo mwaka baada ya mwaka, alisema.

"Kwa upande mmoja sio ghali sana kwa sababu kiasi cha fedha ninachotumia kupata intaneti sasa ni [chini ya] kile nilichokuwa nikitumia kwa kupiga simu [pekee yake]," alisema Abdirahman, akiongeza kwamba anahifadhi fedha kwa kutuma ujumbe mfupi kwa marafiki zake na familia badala ya kupiga simu.

Faisal Muse Mohamed, mwandishi wa habari mwenye umri wa miaka 24 anayefanya kazi katika Redio Mogadishu, amekuwa akipata intaneti kupitia smartphone yake kwa mwaka sasa.

Hususan, anasema anatumia simu yake ya aina ya Samsung Galaxy kupata mitandao ya kijamii kama vile Facebook, ambako huingia kuwasiliana na kupata habari.

"Ninatumia Facebook zaidi kwa sababu unaweza kuwasiliana na marafiki na kupata taarifa na picha zinazokwenda na wakati ambazo zimetumwa," . Alisema anatumia pia Whatsapp kuwasiliana na marafiki kwa sababu sio gharama kubwa na haihitaji matumizi makubwa ya data.
Kuchukua nafasi ya mikahawa ya intaneti
Hassan Mohamed, mkazi wa Mogadishu mwenye umri wa miaka 30 ambaye anasoma sosholojia katika Chuo Kikuu cha Somalia, alisema smartphone ni njia binafsi zaidi ya kupata intaneti, kuunganishwa na watu na kuwa na taarifa wakati wote.

"Sasa ninajisikia kwamba nina uwezo wa kupata intaneti wakati wote ninapoihitaji badala ya kuwategemea [watoa huduma wengine] wa intaneti kama zamani," alisema Mohamed, ambaye amekuwa akitumia simu aina ya Samsung Galaxy kwa karibia miezi saba sasa.

"Ninaitumia kutuma baruapepe, kupata taarifa kuhusu habari, na pia ninatumia kupata tarifa zinazohusiana na masomo na taarifa kutoka katika Google na kupata mitandao ya kijamii," .
"Ninaweza pia kusoma au kutazama chochote ambacho ni faragha kivyangu. Kwa kuwa maeneo ya huduma za intaneti ni maeneo ya umma, huwezi kupata au kutazama kila kitu unachokitaka," alisema.


Mchimba Riziki

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score