Wednesday, December 25, 2013

MSIMU HUU WA SIKUKUU ULINZI WAIMARISHWA MARA DUFU KUEPUKANA NA MATUKIO HATARI ZANZIBAR:

MSIMU HUU WA SIKUKUU ULINZI WAIMARISHWA MARA DUFU KUEPUKANA NA MATUKIO HATARI ZANZIBAR:

 Wakati sikukuu ya krismasi inakaribia, ikitoa nafasi ya kuanza kwa kilele cha msimu wa krismasi, polisi wamewaomba wakaazi kuwa waangalifu na kushirikiana na uongozi ili kuhakikisha usalama kwa wote.

"Hali ya sasa ni nzuri, lakini tumeongeza ulinzi katika maeneo yote ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na maeneo ya makanisa," Kamishna wa Polisi wa Zanzibar Hamdan Omar Makame aliwaambia waandishi wa habari. "Tumewaomba viongozi wa makanisa kuripoti kwa polisi nyendo na matukio yoyote wanayoyatilia shaka."

Makame pia alikutana na viongozi wa Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar katika makao makuu ya polisi siku ya Jumanne (tarehe 24 Desemba) ili kuwahakikishia kuwa polisi wamechukua hatua zote za lazima kuhakikisha usalama wa watalii na raia.

Aliwashukuru kwa kuendeleza ushirikiano wao na viongozi wa usalama na kuomba kwamba wamiliki wa hoteli wote kufunga kamera za usalama katika majengo yao.

"Kila mtu ana jukumu la kutimiza katika kuiweka Zanzibar salama, ikiwa ni pamoja na [kuifanya] mahali salama kwa watalii," alisema.


Matukio ya mashambulizi:
Katika mwaka mmoja na nusu uliopita, mfululizo wa mashambulizi ya tindikali yakiwalenga viongozi wa dini na wageni kutoka nje yaliharibu sifa ya Zanzibar.

Mwezi Novemba 2012, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Suleiman Soraga alijeruhiwa katika shambulizi la tindikali wakati akifanya mazoezi ya kukimbia karibu na nyumbani kwake.

Mwaka jana siku ya Krismasi, mtu mwenye silaha alimpiga risasi na kumjeruhi vibaya Padri Ambrose Mkenda, padri wa kikatoliki katika mji wa Zanzibar. Kisha mwezi Februari 2013, mtu asiyejulikana mwenye silaha alimuua padri wa Kikatoliki Evarist Mushi nje ya kanisa lake Zanzibar.

Mapema mwezi Agosti, washambulizi wasiojulikana waliwamwagia tindikali usoni wanawake wawili wa Uingereza wenye umri wa miaka 18 waliokuwa wakiishi Zanzibar na kufanya kazi kama walimu wa kujitolea.

Tarehe 13 Septemba, padri wa Kikatoliki wa Zanzibari Joseph Anselm Mwangamba aliharibiwa sura na washambulizi wasiojulikana ambao walimmwagia tindikali alipokuwa akitoka kwenye mgahawa wa intaneti Mji Mkongwe. Siku kumi baadaye, kundi la washambuliaji wasiojulikana katika gari la pikapu walitupa guruneti kuelekea kwenye eneo lenye maduka mengi katika Mtaa wa Darajani katika mji wa Zanzibar, lakini lilishindwa kulipuka.

Wakristo na Waislamu wa visiwani walio wengi kihistoria wamekuwa wakiishi kwa amani, Makame alisema, hata hivyo uhalifu huo wa kikatili unauchochea umma na kuipa Zanzibar sifa mbaya nchi za nje.

Ili kusaidia kuhakikisha usalama na kuongeza ushirikiano, Makame alisema ofisi yake imekuwa ikihamasisha mikutano na mijadala baina ya dini mbalimbali ili uhusiano mzuri kati ya Waislamu na Wakristo uimarishwe.

Wakristo wanafikia asilimia 3 ya watu milioni 1.2 wa Zanzibar, walio wengi kati ya hao ni Waislamu.


Wajibu wa Uamsho wachunguzwa:
Bado haieleweki kama mashambulizi ya tindikali na matukio mengine yanachochewa kidini, lakini vurugu za hapa na pale zilianza baada ya kukamatwa kwa kiongozi wa Uamsho Sheikh Farid Hadi Ahmed mwezi Oktoba 2012.

Uamsho, ulitokana na shirika la hisani la dini kuwa chama cha waliojitenga wakidai uhuru kutoka Tanzania.

Ahmed ana viongozi wengine tisa wa Uamsho bado wanashikiliwa, wakishtakiwa Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa kuchochea vurugu na fujo, na njama za kuhatarisha amani na utulivu, miongoni mwa makosa mengine. Walikuwa hawajashitakiwa na walikataliwa dhamana chini ya Sheria ya Usalama wa Taifa. Walikuwa wanasubiri rufaa katika Mhakama Kuu ili kubatilisha uamuzi wa dhamana.

Viongozi wa Uamsho na wafuasi mara kwa mara wamekuwa wakileta wasiwasi wa kidini katika visiwa, lakini taasisi wakati wote imekuwa ikikanusha kuhusika.

Katika mikusanyiko kadhaa mwaka jana, viongozi wa Uamsho walitetea uhuru wa Zanzibar kutoka katika muungano wa sasa na Tanzania ili kutekeleza sheria za Kiislamu.

"Viongozi wa Uamsho wanaamini kwamba uhuru wa Zanzibar utasaidia kutunza utamaduni wa Kiislamu ambao umeharibiwa na mwingiliano wa mtindo wa maisha wa kigeni unaoletwa na wageni na kuigwa na vijana wa nchini," Ahmed aliwaambia waliohudhuria katika mkusanyiko kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Lumumba mwezi Mei 2012.

Hassan Khatib, mwenye umro wa miaka 32, mwalimu katika shule ya dini na mfuasi wa Uamsho anayeishi Zanzibar, alisisitiza kusema kauli yake na kupuuza tuhuma kwamba kikundi kinachochea vurugu.

"Tunataka nguo za heshima hatutaki sketi fupi," Khatib aliwambia waandishi wa habari. "Tunapinga kuongezeka kwa baa, na tunadai uhuru wa Zanzibar ili tuweze kujenga uchumi wetu na kulinda utamaduni wetu."


Vurugu zatishia tasnia muhimu ya utalii:
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar Saidi Ali Mbarouk alisema kwamba mwaka jana tasnia ya utalii, ambayo inachangia asilimia 27 ya pato ghafi la ndani la Zanzibar, iliathiriwa vibaya sana na vurugu.

Tasnia inaajiri moja kwa moja watu 15,000, wakati zaidi ya kazi nyingine 35,000 zinatokana moja kwa moja na utalii, alisema.

"Machafuko yaliyochochewa na kikundi cha Uamsho cha Waislamu mwezi Oktoba mwaka jana, yakifuatiwa na mashambulizi ya viongozi wa dini yameharibu sifa ya Zanzibar," aliiambia Sabahi, akiongeza kwamba kutokuwa na utulivu kumesababisha kushuka kwa utalii, ambako serikali inajaribu kuzuia katika msimu mkuu wa mwaka huu.

Kipindi cha watalii wengi Zanzibar ni kuanzia katikati ya mwezi Juni hadi Septemba na katikati ya Desemba na Februari.

Kutokana na hatua za kukinga zilizochukuliwa kuhakikisha usalama, Mbarouk alisema mamlaka zilikuwa zikitarajia kila kitu kuendeshwa kwa amani kuzunguka katika maeneo ya utalii wakati wa sikukuu.

"Hatutarajii tukio lolote wakati wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya," alisema. "Tunawaomba wananchi kuwakaribisha wageni."

Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar Abdulsamad Ahmed Saidi alikiri kwamba hadi sasa mambo yanaonekana kuwa mazuri.

"Utafiti tulioufanya wiki iliyopita unaonyesha kwamba kuna uthabiti wa biashara katika utalii na ushikaji mzuri wa nafasi kwani katika baadhi ya hoteli nafasi zimejaa," aliwaambia waandishi wa habari.

"Tumelalamika kuhusu usalama, lakini serikali ilijibu vizuri kwa kuongeza maofisa usalama zaidi na pia kuhamasisha polisi jamii, hususani kuzunguka maeneo ya vivutio vya utalii kama vile Mji Mkongwe wa Zanzibar," alisema Saidi.


Hofu inaendelea kuwa kubwa:
Pamoja na uhakika kutoka kwa viongozi wa serikali, hofu inaendelea kuwa kubwa miongoni mwa jamii ya Kikristo.

"Tuko imara na tunaamini yote yataendelea vizuri, lakini jamii ya Kikristo ina wasiwasi," alisema Michael Hafidh, mhubiri katika Kanisa la Anglikani la Zanzibar. "Tumekuwa tukiishi [pamoja] kwa amani kwa miaka mingi, lakini baadhi ya watu wanatugawanya."

Aliwaomba polisi kuendelea kufanya jitihada za kuwasaka watu wanaosababisha hofu na wasiwasi wa kidini visiwani hapo.

Dickson Kaganga, askofu wa Kanisa la Assemblies of God huko Zanzibar, mojawapo kati ya makanisa yaliyolengwa wakati wa maandamano mwaka jana, alisema waumini wake walikuwa na wasiwasi lakini wana matumaini.

"Wote tuna haki ya kushiriki katika dini zetu huko Zanzibar," aliwaaambia waandishi wa habari, akitoa wito kwa polisi kuhakikisha kila mmoja anakuwa salama.

Sheikh Soraga pia alitoa wito wa waamini kuwa na uvumilivu na kushirikiana kwa amani huko Zanzibar, akisema kisiwa hakiwezi kuendelea kama hali ya wasiwasi wa kidini na kisiasa iliopo sasa itaendelea.

"Tuepuke migogoro isiyo ya lazima. Kuna baadhi ya watu wenye ndoto za kisiasa, wanatumia dini kuligawa taifa.

Mchimba Riziki
Tunakutakia X-Mass Njema Na Heri Kwa Mwaka Mpya.

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score