Saturday, January 11, 2014

Seneta Wetangula Ashambuliwa Jijini Nairobi.

Moses Wetangula, seneta mteule wa Kaunti ya Bungoma, alinusurika kuuwawa siku ya Alhamisi (tarehe 9
Januari) pale watu wenye bunduki wasiojulikana walipomfyatulia risasi kwa gari lake jijini Nairobi.

Wetangula alikuwa akiendesha gari kurudi nyumbani kwake Karen kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA),ndipo pale risasi alipovurumishiwa risasi kadhaa kutoka kwenye gari iliyokuwa imeegeshwa ng'ambo ya barabara ya Mbagathi Way.

Aliandika maelezo kwenye kituo cha polisi cha Kilimani baada ya mkasa huo, akisindikizwa na waziri mkuu wa zamani, Raila Odinga, na
msemaji wake, Maseme Machuka.

"Nachukulia hili kuwa ni jaribio la mauaji. Polisi wanapaswa kufanya haraka kufanya uchunguzi
juu ya jambo hili," alisema Wetangula.

Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Nairobi, Benson Kibue, alikiambia kituo cha Capital FM kwamba
polisi watachunguza tukio hilo.

"Hatulichukulii jambo hili kirahisi, maafisa wetu wanafanya kila liwezekanalo kuwakamata washambuliaji," alisema.

Mchimba Riziki

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score