Wednesday, January 8, 2014

Zitto ashinda kesi yake ya kutojadiliwa

Mh. Mbunge Z.Z.Kabwe

Aliyekuwa Naibu Katibu
Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ameshinda
maombi yake dhidi ya chama hicho
mahakamani.
Katika maombi hayo namba 1 ya mwaka 2014,
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, aliiomba Mahakama Kuu, Kanda ya
Dar es Salaam kuizua Kamati Kuu (CC) ya
Chadema kumjadili au kuchukua uamuzi
wowote kuhusu uanachama wake.

Zitto kupitia kwa Wakili Albert Msando
alikuwa akiiomba Mahakama itoe zuio hilo la
muda hadi kesi yake ya msingi
itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Katika uamuzi wake jana, Mahakama Kuu
ilikubaliana na maombi na hoja za Zitto na
kutoa zuio kwa Kamati Kuu ya Chadema na au
chombo chake chochote cha uamuzi kumjadili
na kutoa uamuzi wowote kuhusiana na
uanachama wake, hadi kesi yake ya msingi
itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Awali, Mawakili wa Chadema wakiongozwa na
Mwanasheria Mkuu, Tundu Lissu na
Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za
Binadamu, Peter Kibatala walipinga maombi
hayo wakidai kuwa hayajakidhi matakwa ya
kupewa zuio la muda.

Katika uamuzi wake, Jaji John Utamwa
alikubaliana na hoja za Wakili Msando kuwa
maombi hayo yametimiza matakwa yote ya
kupewa zuio hilo.

Matakwa hayo ni pamoja na kuwapo kwa
mgogoro baina ya pande mbili, hasara au
madhara yasiyoweza kufidiwa na usawa
katika athari kwa pande zote.

Jaji Utamwa alikubaliana na hoja za Wakili
Msando kuwa iwapo Mahakama haitaingilia
kati na kutoa zuio hilo, mtoa maombi
ataathirika zaidi kuliko wajibu maombi.

Akijibu hoja ya Wakili Lissu aliyepinga hoja
ya mtoa maombi kuathirika pamoja na
wananchi wa jimbo lake kwa kukosa
uwakilishi bungeni, kuwa hata akipoteza
ubunge kwa kuvuliwa uanachama utaitishwa
uchaguzi mdogo, Jaji Utamwa alisema
uchaguzi mdogo huwa unachukua mchakato
mrefu.

Baada ya kurejea vifungu mbalimbali vya
sheria, kanuni, amri na uamuzi wa kesi
mbalimbali za Mahakama Kuu, Mahakama ya
Rufani na za nje, Jaji Utamwa alisema
anakubaliana mtoa maombi.

“Kwa hiyo ninatoa zuio la muda kwa Kamati
Kuu ya Chadema na au chombo chake
chochote cha uamuzi kwamba kisimjadili na
kutoa uamuzi wowote dhidi ya mleta maombi
kuhusiana na uanachama wake kusubiri
kusikilizwa na kuamuriwa kwa kesi yake ya
msingi,” alisema Jaji Utamwa.

Kabla ya kufikia uamuzi huo, Jaji Utamwa
alitupilia mbali hati ya kiapo kinzani ya
Chadema iliyotolewa na Wakili Kibatala baada
ya kuwekewa pingamizi na Wakili Msando
ambaye alidai kuwa katika hati hiyo, kuna
taarifa za kusikia ambazo hakueleza
alipozitoa.

Mchimba Riziki

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score