Jalala Kubwa La Taka Dandora Jijini Nairobi |
Mtambo huo mpya unatarajiwa kuchukua miaka miwili kujengwa na utatoa ajira za moja kwa moja 250 na nyingine 1,000 kwa ajili ya kukusanya, kuchambua na kuweka alama takataka kabla ya uzalishaji wake.
"Udhibiti wa takataka umekuwa ukiumiza vichwa kwa watunga sheria pamoja na wakaazi wa jiji hili kwa muda mrefu," Gavana wa Kaunti ya Nairobi Evans Kidero aliiambia Sabahi. "Kwa kuwa na mradi huu, matarajio yetu yanaonyesha kwamba tunaweza kuzalisha megawati 70 za umeme kwa saa kutokana na takataka zinazozalishwa na jiji hili."
Kidero alisema umeme utakaozalishwa utauzwa kwenye Kampuni ya Umeme ya Kenya kuunganisha na mfumo wa taifa. Utasaidia kushughulikia tatizo la kukatika mara kwa mara kwa umeme na mgao unaotokea wakati wa saa za kuhitajika sana na wakati mabwawa ya kuzalisha umeme yanapokarabatiwa.
Wakaazi wa Nairobi milioni 3.2 wanazalisha tani za takataka 2,000 kwa siku, lakini serikali ya jiji inakusanya kati ya tani 850 na 1,100 tu kila siku, kwa mujibu wa gavana.
"Kiasi kinachobakia kinatupwa katika majalala yasiyoruhusiwa kisheria au hazikusanywi katika maeneo zilipo, Kidero alisema. "Mradi huu utaboresha uwezo wetu wa kukusanya kwa sababu jinsi tutakavyokusanya takataka nyingi, ndivyo hivyo hivyo mtambo huu utazalisha umeme mwingi."
Alisema kaunti itaongeza magari yake ya kusafirisha takataka kukusanya taka katika maeneo ya jiji na kuunda vituo vya kukusanya takataka huko Nairobi pamoja na lengo la ukusanyaji wa tani za ziada 800 kila siku.
Nairobi safi na yenye afya zaidi
Kidero alisema mradi huo ni wa aina yake pekee katika nchi. "Utatufanya tufikia ndoto yetu ya muda mrefu ya kusaficha jiji ambayo imekuwa changamoto kwa sababu ya ukosefu wa utaalamu wa kiufundi wa kudhibiti takataka," alisema.
"Takataka zinazotokana na mabaki zinafikia asilimia 60 ya taka ngumu katika jiji hili. Machinjio mengi hayawezi kwa ufanisi kutupa takataka zake katika hali ya usafi unaotakiwa au kiwango cha usalama, lakini nina hakika [hawa] watafarijika na kuwa tayari kupeleka taka zao kwenye mradi huu," alisema.
Mtambo wa umeme utajengwa kwenye eneo la jalala la Dandora kwenye vitongoji vya mashariki mwa Nairobi. Ni mojawapo wa jalala kubwa Afrika lenye ekari 30 na maeneo ya kusafisha, na wakaazi wanaoishi karibu wataunga mkono mradi huu kama suluhisho la muda mrefu kwa tishio la afya ambalo linaathiri maisha yao mara kwa mara.
"Imekuwa ikichukiza machoni kwa miaka mingi," alisema Sarah Njoroge, mama wa nyumbani mwenye umri wa miaka 45 ambaye anapanga nyumba karibu na eneo la jalala. "Kunapokuwa na joto, harufu mbaya inachefua na hatuwezi kula kwa amani kwa sababu ya nzi wanaozagaa. Sasa nimepata faraja mtambo unaokuja utakuwa ni suluhisho la kudumu."
Njoroge alisema anaogopa hatari ya afya inayohusiana na maeneo ya jalala kwa sababu inavutia panya, ambao wanaingia majumbani na ndege wanaokula mizoga, ambao wanakula takataka katika makazi ya wakaazi.
"Kuna hatari ya kupata magonjwa kwa sababu kile kinachotupwa hapa hakijapunguzwa makali na kinatokana na taka za viwandani, kilimo, majumbani na hospitali," aliiambia Sabahi.
Kaberia Lula, mhandisi makenika mwenye umri wa miaka 32 ambaye anaishi Nairobi, alitarajia mradi huo kuwa utazidi mategemeo.
"Utekelezaji wa taka kuwa nishati na kuchoma utakuwa mfano kwa kaunti nyingine," aliiambia Sabahi. "Nairobi kutumia utaratibu wa kukusanya taka kutoka katika kaunti nyingine kutahitaji njia ya usambazaji mara mradi huu utakapoanza."
Mradi wa taka kuzalisha nishati 'mfano unaoshamiri'
Ayub Macharia, mkurugenzi wa elimu ya mazingira, ushiriki usio rasmi na wa Umma katika Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira, alisema mradi huo utaonyesha njia kwa ajili ya ukarabati wa eneo la jalala Dandora, ambao utawanusuru watu na mazingira pia.
Kenya inazalisha megawati 1,600 za umeme kila siku dhidi ya mahitaji makubwa ya megawati 1,500, mahitaji yakiwa yanaongezeka kwa wastani wa asilimia 8 kwa mwaka, kwa mujibu wa takwimu kutoka Shirika la Uzalishaji wa Umeme la Kenya (KenGen).
KenGen inazalisha zaidi ya megawati 1,200, wakati kampuni nyingine binafsi zinazalisha kiasi kinachobaki.
"Huu utazalisha megawati 70 zitakazojazia usambazaji wa umeme kwa sababu kwa kuwa na maendeleo ya majengo yanayoibuka, umeme zaidi utahitajika jijini na katika nchi kwa ujumla," Macharia alisema.
Alisema maeneo mengine ya Kenya, hususan majiji makubwa yanapaswa kutumia mkakati wa taka kuwa nishati kwa sababu nishati jadidifu inapunguza matumizi ya nishati asilia na kwa hiyo kuwa suluhisho la kuongezeka kwa joto duniani.
Sehemu ya kitengo cha mtambo mpya itatumika kubainisha vioo, plastiki, chuma, kadibodi na vifaa vingine vinavyoweza kurejelezwa. Kwa sasa urejelezaji unafanywa na kampuni ndogo na watu binafsi katika kiwango cha chini.
"Kimsingi, imetatua mahitaji ya kuhamisha eneo la jalala kama mamlaka ya jiji inavyopendekeza," Macharia aliiambia Sabahi. "Mradi huu utafanya kazi kama mfano unaoshamiri kwa kampuni nyingine za kaunti za Kenya. Ni hatua kubwa kuelekea mwanzo wa upunguzaji, utumiaji tena na urejelezaji wa taka."
Mchimba Riziki
0 maoni:
Post a Comment