Friday, February 7, 2014

Chadema walia hujuma kukamatwa wabunge

Iringa. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimedai kufanyiwa hujuma, Mbunge wa Iringa Mjini kupitia chama hicho, Mchungaji Peter Msigwa amekuwa mbunge wa pili kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kujeruhi.

Msigwa alifikishwa jana katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa akidaiwa kutenda kosa hilo juzi kwa kumjeruhi kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salum Kaita kwenye mikutano ya kampeni ya kumnadi mgombea wa udiwani wa Chadema katika Kata ya Nduli, Ayub Mwenda.

Juzi, katika Mahakama ya Wilaya ya Kahama, Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbayi na wenzake 15, walipandishwa kizimbani kwa tuhuma za kuwajeruhi wafuasi watano wa CCM katika kampeni za udiwani na kulazwa rumande. Wakati hayo yakiendelea, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alijisalimisha polisi kutokana na taarifa za kutafutwa kwake kutokana na tuhuma zinazohusiana na uharibifu wa mali katika kampeni za udiwani. Aliachiwa baadae.

Mashtaka ya Msigwa

Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo Godfrey Isaya, Wakili wa Serikali, Elizaberth Swai alidai kuwa mnamo Februari 5 mwaka huu katika Kata ya Nduli, Msigwa alimjeruhi Kaita kinyume cha sheria sura ya 12 ya mwaka 2002 kifungu cha 225 cha kanuni ya adhabu.

Mchungaji Msigwa alikana mashtaka hayo na kuachiwa kwa dhamana ya Sh2 milioni iliyowekwa na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Chiku Abwao na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Lilian Msomba.

Chadema walia na polisi

Kutokana na matukio hayo, Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa Chadema, Kigaila Benson aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa Jeshi la Polisi linatakiwa kuwatia nguvuni wale wote ambao wanahusika na vitendo kuwajeruhi wanachama wao badala ya kupindisha ukweli.

Akizungumzia vurugu zinazoendelea katika kampeni za kuwania udiwani kwenye kata 27, Kigaila alisema uongozi wa CCM na Polisi kwa pamoja wanajua kinachotokea lakini wanakifumbia macho.

“Watu wetu wanajeruhiwa, wanakamatwa wanawekwa mahabusu na tunapotoa taarifa polisi hazichukuliwi hatua. Inakuaje watu wanaoumiza watu wetu hawakamatwi? Polisi wanatakiwa kuzingatia sheria na kanuni kwa wote,” alisema Benson.

Kasulumbayi apata dhamana

Mahakama ya Wilaya ya Kahama jana mchana ilimwachia kwa dhamana Kasulumbayi aliyekuwa ameshikiliwa kwa tuhuma za kuwacharanga mapanga wafuasi wa CCM kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani wilayani Kahama.

Mchimba Riziki

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score