Sunday, February 2, 2014

MWANAMKE AMWACHA MTOTO MCHANGA KWA KONDAKTA NA KUTOWEKA

Kulizuka kizaazaa katika kituo cha mabasi mjini Karatina mwanamke alipomuachia kondakta mtoto mchanga na kutoweka.
Kulingana na walioshuhudia kisa hicho, mwanamke huyo alimuacha mtoto akisema ameenda kutoa pesa katika duka la M-Pesa ili kumnunulia mwanawe chakula.
Kondakta aliye achiwa mtoto

“Aliniomba nimshikie mtoto ili aweze kutoa hela katika duka la M-Pesa za kumnunulia mwanawe maziwa,” alisema Bw Karungaru.
Kondakta huyo alieleza kuwa baada ya kumuacha mtoto huyo, mama alitoweka kabisa na ilimbidi kukaa na mtoto siku nzima huku akiomba angalau mama mtoto arejee.

Baada ya kuona mama harejei, kondakta aliamua kumpelekea mkewe mtoto huyo ili amtunze.
Baadaye alienda katika kituo cha polisi cha Karatina kupiga ripoti ambapo maafisa walimwambia aendelee kuishi na mtoto huyo huku wakiendelea kufanya uchunguzi zaidi kuhusu kisa hicho.

Kulingana na Bi Milka Muthoni, ambaye ni mkewe Bw Karungaru, wako tayari kuendelea kumtunza mtoto huyo.
“Mimi sina shida kulea mtoto. Iwapo mama yake atakataa kurudi nitamchukua kama mwanangu,” alisema Bi Muthoni.

Kumlea

Hata hivyo, Bw Karungaru anahofia kuwa hata kama wanaweza kumlea, jamaa wa mtoto wanaweza kuamua kumchukua atakapokuwa mtu mzima.

“Hofu yetu ni kuwa kwa vile hatujui alipotoka mama huyo, tunaweza kumlea mtoto huyu lakini baada ya miaka kadha familia yake idai kupewa mtoto wao,” alisema Bw Karungaru.

Hata hivyo, alisema kuwa wanafanya kila juhudi kuhakikisha wamefuata sheria na kumchukua na kuishi naye kwa njia halali.
Maafisa wa polisi wanafanya uchunguzi ili kufahamu alipotorokea mama mtoto.

MCHIMBA RIZIKI

0 maoni:


Copyright © 2014. Mchimba Riziki- All Rights Reserved

Map

Live score